Tanzania swahili radio

IQRA FM RADIO

IQRA FM RADIO
IQRA FM RADIO ELIMU NA MATENDO UIMARA WA RADIO IQRA UPO MIKONOMI MWAKO CHANGIA RADIO IQRA KWA MPESA 0762118805TIGO PESA 0658118804
Showing posts with label leo katka hisory. Show all posts
Showing posts with label leo katka hisory. Show all posts

Monday, October 20

Jumapili 24 Dhulhijjah 1435

Leo ni Jumapili tarehe 24 Mfungo Tatu Dhulhijjah mwaka 1435 Hijria, inayosadifiana na tarehe 19 Oktoba 2014 Miladia.
Jumapili 24 Dhulhijjah 1435Siku kama ya leo miaka 1426 iliyopita kwa mujibu wa riwaya mashuhuri Mtume Muhammad (saw) akiwa pamoja na binti yake Bibi Fatima (as), mkwewe Ali bin Abi Twalib (as) na wajukuu wake wawili Hassan na Hussain (as) aliondoka mjini Madina kwenda kufanya mdahalo na maapizano na viongozi wa Wakristo wa eneo la Najran juu ya dini ya kweli. Tukio hilo linaelezwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu katika aya za 60 na 61 za sura ya Aal Imran. Wakati viongozi wa Najran walipoona Mtume amekuja katika mdahalo huo akiwa na watu wanne tu wa Nyumba yake tukufu walipigwa na mshangao na kuelewa kwamba, dua ya laana ya mtukufu huyo kwa mtu ambaye angesema uongo ingekubaliwa. Katika hali hiyo askofu wa Najran alisema: "Ninaziona nyuso ambazo iwapo zitamuomba Mwenyezi Mungu aung'oe mlima mkubwa zaidi mahala pake basi dua yao itajibiwa papo hapo. Hivyo haitakuwa sahihi kufanya mdahalo na watu hawa watakatifu kwani yumkini kizazi chetu chote kikaangamia." Baada ya hapo askofu huyo wa Najran alimuomba msamaha Mtume (saw). Tukio hilo la kihistoria lilidhihirisha haki na ukweli wa dini tukufu ya Kiislamu na utukufu na nafasi aali ya Ahlulbait wa Mtume Muhammad (saw).
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, Ali Hassan Salameh mmoja kati ya viongozi wa juu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO aliuawa shahidi nchini Lebanon kupitia njama za vibaraka wa Shirika la Ujasusi la utawala haramu wa Israel MOSSAD. Salameh alikuwa afisa wa usalama wa PLO na aliuawa shahidi baada ya kuripuka bomu lililotegwa katika gari lake mjini Beirut. Jinai hiyo ya utawala haramu wa Kizayuni ndani ya Lebanon kwa mara nyingine iliweka wazi ugaidi na uvamizi wa Israel dhidi ya ardhi ya nchi nyingine.
Siku kama ya leo miaka 11 iliyopita, alifariki dunia Ali Ezzat Begovic, mwanasiasa na mwandishi wa Bosnia Herzegovina. Ali Begovic alizaliwa mwaka 1925 na kupata taaluma ya sheria katika Chuo Kikuu cha Sarajevo katikati mwa Bosnia. Alianza kupambana na utawala wa kikomunisti wa Yugoslavia ya zamani akiwa kijana mdogo na kufungwa jela mara kadhaa. Mwaka 1989 Ali Begovic aliasisi chama kipya cha siasa kwa jina la Democratic Action kilichokuwa na nafasi kubwa katika uhuru wa Bosnia mwaka 1991. Mwanasiasa huyo wa Kiislamu ambaye baada ya uhuru wa taifa hilo alichaguliwa kuwa rais, alikuwa na nafasi kubwa katika kuwatetea raia wa Bosnia, katika mashambulizi ya askari wa Serbia na dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.
Na siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, vita kati ya vikosi vya Japan na jeshi la Marekani vilianza katika visiwa vya Ufilipino. Itakumbukwa kuwa, wakati wa kuanza Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, Ufilipino ilishambuliwa na Japan na kwa muda mfupi ikawa imedhibitiwa na kukaliwa kwa mabavu. Hata hivyo baada ya kushindwa Ujerumani ya Kinazi katika Vita vya Pili vya Dunia, majeshi ya Marekani chini ya usimamizi wa Douglas MacArthur yaliishambulia Ufilipino na kuyatoa majeshi ya Japan katika ardhi ya nchi hiyo na kisha kuanzisha kambi za kijeshi nchini humo.
Read more »

Jumamosi, Oktoba 18, 2014

Jumamosi, Oktoba 18, 2014Leo ni Jumamosi tarehe 23 Mfunguo Tatu Dhil-Hija 1435 Hijria inayosadifiana na tarehe 18 Oktoba mwaka 2014 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, yaani tarehe 26 Mehr 1359 Hijria Shamsia, Shahidi Muhammad Ali Rajai Waziri Mkuu wa wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alihudhuria kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kutoa hotuba ndefu kuhusu taathira zilizosababishwa na vita vya kulazimishwa vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Shahidi Rajai pia alizungumzia masuala muhimu ya dunia, hususan kukaliwa kwa mabavu Palestina na utawala wa Kizayuni pamoja na njama za wakoloni duniani kote. Baada ya hotuba hiyo, wawakilishi wa serikali ya Marekani walitaka kukutana na kufanya mazungumzo na shahidi Rajai, lakini Waziri Mkuu wa Iran alikataa pendekezo hilo kutokana na siasa za kibeberu za Marekani na jinai ilizotenda katika pembe mbalimbali duniani.
Katika siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, msomi aliyegundua umeme aliyejulikana kwa jina la Thomas Edison alifariki dunia. Edison alizaliwa mwaka 1847 huko Marekani. Thomas Edison hakuwa na taalumu yoyote kutoka chuo kikuu bali ni tafiti na majaribio yake mengi pekee ndiyo yaliyopandisha juu kiwango chake cha elimu na maarifa. Akiwa kijana, Edison aliasisi maabara moja ya masuala ya kemia na kufanya majaribio makubwa katika maabara hiyo. Bidii ya msomi huyo ilimuwezesha kuvumbua mambo mengi ambapo muhimu kati ya hayo ni hatua yake ya kuvumbua umeme, kutengeneza lampu na gramafoni au santuri.
Miaka 92 iliyopita katika siku kama ya leo, redio ya BBC iliasisiwa huko Uingereza. Redio ya BBC awali ilikuwa ya mtu binafasi, lakini ilipofika mwaka 1927, redio hiyo ikawa chini ya usimamizi wa serikali na hivyo kuwa katika kalibu ya redio za serikali ya Uingereza. Bajeti ya redio za BBC ambazo zinatangaza kwa lugha mbalimbali za dunia inadhaminiwa na serikali ya Uingereza. Pamoja na kuwa BBC inadai kwamba haipendelei upande wowote katika matangazo yake, lakini katika kipindi cha nusu karne ya hivi karibuni, chombo hicho cha kupasha habari kimegeuka na kuwa wenzo wa serikali ya Uingereza na hivyo kuiandalia London uwanja wa kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine.
Na miaka 76 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria, Sheikh Abbas Qumi alimu na mpokezi mashuhuri wa Kiislamu alifariki dunia. Alizaliwa mwaka 1294 Hijria katika mji mtakatifu wa Qum Iran. Awali Sheikh Abbas Qumi alisoma mjini Qum na baadaye akiwa na lengo la kujiendeleza zaidi katika masomo ya dini alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf Iraq. Akiwa Najaf, Sheikh Abbas Qumi alinufaika na bahari ya elimu ya wanazuoni mahiri wa zama hizo. Baadaye alirejea nchini Iran na kujishughulisha na kazi ya kualifu vitabu. Kitabu mashuhuri na chenye thamani kubwa cha Sheikh Abbas Qumi ni kile cha dua cha Mafatihul Jinan ambacho kina mkusanyiko wa dua na ziara.

Read more »

Ijumaa, Oktoba 17, 2014

Ijumaa, Oktoba 17, 2014
Leo ni Ijumaa tarehe 22 Dhulhaji 1435 Hijria sawa na 17 Oktoba 2014.
Katika siku kama ya leo miaka 1375 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Maytham al-Tammar mmoja wa masahaba na wafuasi wa Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi. Awali Maytham al-Tammar alikuwa mtumwa na alinunuliwa na kuachiwa huru na Imam Ali bin Abi Talib (as). Imam Ali alikuwa akimpenda na kumthamini sana Maytham al-Tammar kama ambavyo Maytham pia alikuwa na mapenzi makubwa na Imam Ali. Hatimaye katika siku kama ya leo, sahaba huyo mwema wa Mtume (saw) aliuawa kinyama na watawala wa Bani Umayyah kwa kosa la kuwapenda na kuwaunga mkono Ahlul Bayt (as) na kufa shahidi katika siku kama ya leo.
Miaka 41 iliyopita katika siku kama hii ya leo nchi za Kiarabu zinazouza nje mafuta zilianza kutekeleza vikwazo vya mafuta dhidi ya Marekani, Uingereza na makampuni yanayouuzia mafuta utawala wa Kizayuni wa Israel. Hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na uungaji mkono mkubwa wa Marekani na Uingereza kwa utawala ghasibu wa Israel katika vita vya Israel dhidi ya Syria na Misri. Hatua hiyo ilipandisha sana bei ya mafuta katika masoko ya kimataifa na kutoa pigo kubwa kwa nchi hizo za Magharibi. Muda mfupi baadaye nchi za Kiarabu zilikiuka vikwazo hivyo vya mafuta na kuanza tena kuiuzia mafuta Marekani na Uingereza. Vikwazo hivyo vilionesha kuwa nchi za Kiislamu zina silaha muhimu inayoweza kutumiwa dhidi ya uungaji mkono mkubwa wa nchi za Magharibi kwa utawala katili wa Israel.
Na Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, aliaga dunia mtaalamu wa masuala ya jamii wa Kifaransa kwa jina la Raymond Aron. Aron alizaliwa mwaka 1905. Msomi huyo wa Kifaransa alikuwa akifundisha pia taaluma hiyo ya masuala ya jamii katika Chuo Kikuu cha Sorbonne, Paris kwa miaka kadhaa. Vilevile alikuwa akiandika makala katika majarida ya Le Figaro na Express mjini Paris. Raymond Aron ameandika vitabu vingi na hapa tunaweza kuashiria vitabu vyake vichache alivyovipa majina ya "Kuanza Vita vya Nyuklia, "Mapambano ya Kitabaka" na "Miaka ya Mwishoni mwa Karne"
Read more »

Alkhamisi, 16 Oktoba, 2014

Leo ni Alkhamisi tarehe 21 Dhulhaji 1435 Hijria sawa na tarehe 16 Oktoba 2014.
Alkhamisi, 16 Oktoba, 2014Siku kama ya leo tarehe 24 Mehr miaka 36 iliyopita, kulitokea maafa makubwa kwenye Msikiti Mkuu wa Kerman, huko amagharibi mwa Iran baada ya vikosi vya polisi na usalama vya utawala wa mfalme Muhammad Reza Pahlavi kuwashambulia kwa risasi wananchi waliokusanyika kwenye eneo hilo la msikitini kwa shabaha ya kuadhimisha 40 ya mashahidi waliouawa tarehe 17 Shahrivar mjini Tehran. Shambulio hilo la vikosi vya usalama vya Shah liliamsha hasira na wimbi jipya la harakati za wananchi za kupinga utawala kibaraka wa Mfalme Muhammad Reza Pahlavi.
Miaka 68 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 16 Oktoba 1946, kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Nuremberg walinyongwa viongozi 9 wa Ujerumani ya Wanazi baada ya kupatikana na hatia za kutenda jinai za kivita. Herman Goering aliyekuwa Kamanda Mkuu wa kikosi cha jeshi la anga la Ujerumani na msaidizi wa dikteta Adolphe Hitler ambaye alikuwa amehukumiwa adhabu ya kifo, pia aliamua kujinyonga yakiwa yamebakia masaa machache kabla ya kutekelezwa hukumu hiyo ya kifo. Hali kadhalika mahakama hiyo iliwahukumu adhabu ya kifungo cha muda mrefu viongozi wengine 9 wa Ujerumani ya Wanazi na wengine watatu hawakupatikana na hatia. Mahakama ya Nuremberg iliyoundwa na wawakilishi wa Marekani, Urusi ya zamani, Uingereza na Ufaransa kwa shabaha ya kuwahukumu maafisa 22 wa Manazi wa Ujerumani kwa tuhuma za kufanya jinai za kivita ilikamilisha shughuli zake tarehe 30 Septemba mwaka 1946.
Na miaka 867 iliyopita sawa na tarehe 21 Dhulhija mwaka 568 Hijria, alizaliwa Abulhassan Ali Bin Yusuph Sheibani maarufu kwa jina la 'Ibn Qefti, ambaye alikuwa mwandishi hodari wa Kiislamu katika mji mdogo wa Qeft nchini Misri. Baada ya kumaliza masomo alijishughulisha na kazi ya uhakimu. Ibn Qefti ameandika vitabu 26 vya kihistoria na kisayansi na mashuhuri zaidi ni kile alichokipa jina la Tarikhul Hukamaa. Mwandishi huyo wa Kiislamu alifariki dunia mwaka 649 Hijria.
Read more »

Jumatano, Oktoba 15, 2014

Jumatano, Oktoba 15, 2014Leo ni Jumatano tarehe 20 Dhulhaji 1435 Hijria, inayosadifiana na Oktoba 15, 2014.
Siku kama ya leo miaka 120 iliyopita yaani tarehe 15 Oktoba mwaka 1894, ilianza kesi ya Alfred Dreyfus mjini Paris, Ufaransa. Dreyfus alikuwa afisa wa jeshi la Ufaransa mwenye asili ya Kiyahudi ambaye kesi yake ni miongoni mwa matukio yaliyozusha makelele mengi katika karne ya 19 nchini humo. Afisa huyo wa jeshi alituhumiwa kuisaliti nchi yake na kutoa siri za jeshi la Ufaransa kwa Ujerumani. Alivuliwa cheo chake na akahukumiwa kifungo cha maisha jela. Baada ya kuhukumiwa kifungo hicho, ilithibitika kwamba Alfred Dreyfus hakuwa na hatia yoyote. Kwa utaratibu huo aliachiwa huru na kurejeshewa heshima na vyeo vyake. Hukumu ya kifungo cha maisha jela ya Dreyfus na kisha kutambuliwa kwake kuwa hakuwa na hatia, kadhia ambayo inatambuliwa kwa jina la Dreyfus Affair, ilitumiwa na Wazayuni katika propaganda za urongo kudai kwamba Wayahudi wamedhulumiwa barani Ulaya. Wazayuni walitumia vibaya kadhia hiyo kujiimarisha zaidi.
Tarehe 15 Oktoba miaka 170 iliyopita alizaliwa mwanafalsafa wa Kijerumani Friedrich Wilhelm Nietzsche. Baada ya kuhitimu masomo, Nietzsche alianza kufunza katika Chuo Kikuu cha Basel. Mwanafalsafa huyo alikuwa akipinga dini na misingi ya kimaadili na katika falsafa na mitazamo yake alikuwa akiamini nadharia ya "Superman", kwa maana ya mtu mwenye uwezo kupita kiasi. Nietzsche alikuwa akiamini kwamba, mtu mwenye uwezo kupita kiasi au Superman ni matokeo ya irada na matashi ya mwanadamu na huwa juu ya mema na mabaya yote. Mwanafalsafa huyo ameandika vitabu kadhaa ikiwa ni pamoja na Beyond Good and Evil, The Birth of Tragedy na Thus Spoke Zarathustra.  Katika kipindi cha mwishoni mwa uhai wake Friedrich Wilhelm Nietzsche alipoteza mlingano wa kifikra na alifariki dunia mwaka 1900.
Na siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, mwakilishi wa Imam Khomeini M.A na Imam wa Sala ya Ijumaa ya mji wa Kermanshah huko magharibi mwa Iran Ayatullah Ashrafi Isfahani, aliuawa shahidi na vibaraka wa kundi la MKO akiwa katika mihrabu ya ibada. Ayatullah Ashrafi Isfahani aliongoza wananchi wa Kermanshah katika harakati na mapambano ya Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala wa Shah. Aliteuliwa na Imam Khomeini kuwa Imam wa Sala ya Ijumaa ya Kermanshah baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na aliuawa shahidi katika mihrabu akisalisha Sala ya Ijumaa
Read more »

Jumanne, Oktoba 14, 2014

Leo ni Jumanne tarehe 19 Dhilhaji 1435 Hijria sawa na 14 Oktoba 2014.
Jumanne, Oktoba 14, 2014Siku kama ya leo miaka 15 iliyopita alifariki dunia kiongozi wa zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Nyerere alizaliwa Butiama mkoani Mara mwaka 1922. Mwaka 1955 aliingia katika ulingo wa siasa huku akiongoza chama cha Tanganyika African National Union (TANU). Mwaka 1961 Nyerere alikuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika na mwaka mmoja baadaye akawa rais wa nchi hiyo. Kutokana na juhudi zake mwaka 1964 ziliungana Tanganyika na Zanzibar na kuunda nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nyerere aliendelea kuongoza nchi hiyo hadi mwaka 1985 ambapo aliachia hatamu za uongozi. Hata hivyo Nyerere aliendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Tanzania hadi alipofariki dunia.
Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita Wazayuni wa Israel walivamia kijiji cha Qibya kilichoko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina na kufanya jinai kubwa za kutisha. Katika mashambulizi na uvamizi ulioendelea katika kijiji hicho kwa muda wa siku mbili, Wazayuni walifanya mauaji na ukatili mkubwa dhidi ya raia wa Kipalestina wasio na hatia. Mbali na Wazayuni hao kuwaua na kuwajeruhi kwa umati raia zaidi ya 42 wa Kipalestina, askari wa Israel waliokuwa wakiongozwa na waziri mkuu wa zamani wa utawala huo wa kigaidi Ariel Sharon walibomoa makumi ya nyumba na shule za kijiji hicho. Mauaji hayo ya halaiki ni miongoni mwa mifano ya ugaidi wa utawala ghasibu wa Israel hususan waziri mkuu wa zamani wa utawala huo Ariel Sharon.
Na tarehe 19 Dhulhija mwaka 1257 Hijria alizaliwa Ayatullah Sayyid Muhammad Tabatabai, mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu na wapigania uhuru wa Iran. Wakati wa mapinduzi ya kikatiba nchini Iran, Sayyid Muhammad Tabatabai alikuwa akihesabika kuwa miongoni mwa viongozi wakubwa wa mapinduzi hayo. Tabatabai alishirikiana na Sayyid Abdullah Behbahani ambaye naye alikuwa mmoja wa viongozi wa harakati ya kikatiba dhidi ya utawala wa Qajari nchini Iran.
Mbali na kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, Sayyid Tabatabai alikuwa mwanazuoni hodari na alifanya bidii kubwa kueneza mafundisho ya Kiislamu
Read more »

Monday, October 13

Jumatatu, Oktoba 13, 2014

Jumatatu, Oktoba 13, 2014Leo ni Jumatatu tarehe 18 Mfunguo 3 Dhilhija mwaka 1435 Hijiria, inayosadifiana na tarehe 13 Oktoba mwaka 2014 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1425 iliyopita yaani tarehe 18 Mfunguo Tatu, Mtume Muhammad (SAW) alimtangaza Imam Ali bin Abi Twalib (AS) kuwa Khalifa na kiongozi wa Waislamu baada yake. Siku hiyo Bwana Mtume alikuwa akirejea kutoka Makka alikokwenda kutekeleza ibada tukufu ya hija na iliyokuwa hija yake ya mwisho. Mtume alisimama mahala palipoitwa Ghadir Khum na baada ya kupanda sehemu yenye mwinuko aliuhutubia umma mkubwa wa Waislamu waliokuwa wamejumuika mahala hapo. Aidha Mtume (SAW) aliinua mkono wa Imam Ali na kusema: "Yule ambaye mimi ninayatawala mambo yake, huyu Ali ni Mwenye kuyatawala mambo yake pia, Ewe Mola! Mfanye kipenzi Mwenye kumfanya Ali kipenzi, mfanye adui Mwenye kumfanyia uadui na mnusuru mwenye kumnusuru." Ni kutokana na tukio hilo kubwa katika historia ya Uislamu, ndipo siku hii ikajulikana kuwa sikukuu ya Eidul Ghadir.
Siku kama ya leo miaka 2553 iliyopita mji wa kihistoria wa Babel ulitekwa na Korush, mwasisi wa utawala wa kizazi cha Hakhamaneshi nchini Iran. Ili kuweza kuudhibiti mji huo ambao ulikuwa na ngome kubwa na imara, Korush alitoa amri ya kubadilishwa njia ya maji ya Mto Tigris ambao ulikuwa ukipita ndani ya mji huo na kwa utaratibu huo askari wake wakatumia njia ya maji ya mto huo kuingia na kisha kuuteka mji huo. Mji huo ulioko kusini mwa eneo la Mesopotamia katika Iraq ya sasa ulikuwa katika kilele cha maendeleo na nguvu kubwa katika kipindi hicho.
Na miaka 50 iliyopita bunge la kimaonyesho la Iran lilipasisha sheria iliyowapa washauri wa kijeshi wa Marekani nchini kinga ya kutofikishwa mahakamani iwapo wangepatikana na hatia ya aina yoyote. Kwa mujibu wa sheria hiyo wahalifu wa Kimarekani wangehukumiwa nchini kwao kama watatenda jinai nchini Iran, na mahakama za Iran hazikuwa na haki ya kushughulikia kesi zao.
Sheria hiyo ilitambuliwa kuwa dharau kwa taifa la Iran na iliyokiuka wazi kujitawala kwa nchi. Kwa msingi huo hayati Imam Khomeini (MA) siku kadhaa baada ya kupasishwa sheria hiyo bungeni alitoa hotuba ya kihistoria akieleza taathira zake na kumshambulia vikali Mfalme Shah na Marekani. Baada ya hotuba hiyo Imam Khomeini alikamatwa na kupelekwa uhamishoni
Read more »

Sunday, October 12

Jumapili, Oktoba 12, 2014

Jumapili, Oktoba 12, 2014Leo ni Jumapili tarehe 17 Mfunguo Tatu Dhul-Hijja mwaka 1435 Hijiria, inayosadifiana na tarehe 12 Oktoba mwaka 2014 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 482 iliyopita wakoloni wa Kihispania walianzisha mashambulizi chini ya uongozi wa Francois Pizarro dhidi ya ardhi inayojulikana hii leo kwa jina la Peru. Wakati huo kaumu ya Inka ambayo ni moja kati ya kaumu za America ya Latini ndiyo iliyokuwa ikitawala eneo hilo. Viongozi wa kaumu hiyo hawakutilia maanani uvamizi wa Wahispania huku wakisalia bila kuchukua hatua zozote za kukabiliana na wavamizi hao. Baada ya kudhibitiwa ardhi ya Peru na wavamizi hao, Pizarro alimtaka mtawala wa Inka kuwa chini ya himaya ya Uhispania lakini akakataa pendekezo hilo. Pizarro alitoa amri ya mauaji ya umati dhidi ya watu wa kaumu hiyo mauaji yanayohesabiwa kuwa makubwa na mabaya zaidi katika historia ya America ya Latini. Ukubwa wa mauaji hayo ndio uliopelekea kuporomoka ustaarabu na utawala wa miaka mingi wa Inka.
Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, Guinea ya Ikweta (Equa torial Guinea) ilifanikiwa kupata uhuru wake kutoka kwa mkoloni Muhispania, na siku hii hutambuliwa kama siku ya kitaifa nchini humo. Equatorial Guinea iligunduliwa na mabaharia wa Ureno katika karne ya 15 Miladia. Ureno ulikikabidhi kisiwa hicho kwa Uhispania hapo mwaka 1778 Miladia, huku ukoloni wa Wahispania dhidi ya Equatorial Guinea ukiendelea hadi mwaka 1968 ambapo nchi hiyo ilijipatia uhuru wake. Equatorial Guinea inapakana na nchi za Gabon na Cameroon.
Siku kama ya leo miaka 15 iliyopita, Jenerali Parviz Musharraf, mkuu wa majeshi ya Pakistan alifanya mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu na kumuondoa madarakani Muhammad Nawaz Sharrif Waziri Mkuu wa Pakistan wa wakati huo. Baada ya mapinduzi hayo Musharraf ambaye alichukuwa wadhifa wa urais wa nchi hiyo, alivifanyia mabadiliko baadhi ya vipengee vya katiba ya nchi hiyo, na kuongeza nguvu za rais wa nchi. Lakini kutokana na kuongezeka mashinikizo ya ndani na nje, Musharraf alisalimu amri mwezi Novemba 2007 na kuamua kung'atuka kwenye wadhifa huo. Hata hivyo ilipofika mwezi Julai 2008, aliondoka kikamilifu madarakani ikiwa ni baada ya kushika kasi vyama vya upinzani na kushinda uchaguzi wa rais.
Leo ni tarehe 20 mwezi wa Mehri kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, ambayo inasadifiana na maadhimisho ya Khoja Shamsuddin Muhammad Hafez Shirazi, mshairi na malenga mkubwa wa Kiirani. Hafez alizaliwa mwaka 727 Hijiria Shamsia, mjini Shiraz moja ya miji ya kusini mwa Iran. Alikuwa mtaalamu katika Tafsiri ya Qur'an, falsafa na fasihi ya Kiarabu huku akiwa mashuhuri kwa jina la Hafez kutokana na kuhifadhi kwake Qur'an Tukufu kwa visomo tofauti. Mbali na elimu hizo, Khoja Shamsuddin Muhammad Hafez, alikuwa mtaalamu mkubwa wa elimu ya Irfan.
Read more »

Jumamosi, Oktoba 11, 2014

Jumamosi, Oktoba 11, 2014Leo ni Jumamosi tarehe 16 Mfunguo Tatu Dhil-Hija 1435 Hijria mwafaka na tarehe 11 Oktoba 2014 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 115 iliyopita vilianza vita vilivyokuwa na umwagaji damu baina ya wahajiri wa Uingereza na weupe wa Uholanzi waliojulikana kwa jina la Boer waliokuwa wakiishi nchini Afrika Kusini. Vikosi vya Uingereza vikiwa na shabaha ya kulikoloni bara la Afrika viliwasili Afrika Kusini mwaka 1841, na baada ya kujenga makazi vilibaki katika nchi hiyo. Baada ya kugunduliwa ya almasi na dhahabu nchini Afrika Kusini, wimbi la wahajiri kutoka Ulaya hasa Uingereza kuelekea nchini humo lilikithiri. Kutokana na wahajiri wa mwanzo nchini Afrika Kusini yaani wahajiri wa Kiholanzi waliojulikana kwa jina la Boer kupinga kuwasili wahajiri wengine, kulizuka vita baina yao na wahajiri wa Uingereza. Wahajiri wa Kiholanzi walishindwa katika vita hivyo kutokana na serikali ya Uingereza kuwaunga mkono wahajiri wa Kiingereza.***
Miaka 23 iliyopita katika siku kama ya leo, shughuli za Shirika la Ujasusi la Urusi ya zamani (KGB) zilifikia kikomo muda mfupi kabla ya kusambaratika nchi hiyo. KGB iliundwa mwaka 1954 kwa lengo la kukabiliana na harakati zilizokuwa na lengo la kuuangusha mfumo wa Kikomonisti wa Urusi ya zamani. Shirika hilo aidha lilikuwa na majukumu kama vile kuwakandamiza wapinzani wa chama cha Kikomonisti na kuendesha operesheni za kijasusi na zile zilizo dhidi ya ujasusi ndani na nje ya Muungano wa Kisovieti.***
Katika siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, Ayatullah Haji Mirza Khalil Kamarei mfasiri wa Qur'ani Tukufu na mhadhiri wa chuo kikuu alifariki dunia. Ayatullah Ka marei alijifunza elimu za fiqih, usul-fiqih na masomo mengine ya kidini katika Hauza ya kielimu ya mji mtakatifu wa Qum nchini Iran na baadaye alianza kufundisha falsafa. Mwaka 1341 Hijria Shamsia alikamatwa na kufungwa jela kutokana na kupinga siasa za kidhalimu na utawala wa Shah. Haji Kamarei ameandika vitabu vingi kwa lugha za Kifarsi na Kiarabu. Miongoni mwa vitabu hivyo ni tafsiri ya Qur'ani, sherhe ya Nahjul Balagha na kitabu cha maisha ya Imam Hussein AS na mashahidi wengine wa Karbala.
Na miaka 99 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Jean Henri Fabre msomi wa elimu ya sayansi na bingwa wa elimu ya wadudu au entomolojia. Fabre alizaliwa mwaka 1823 nchini Ufaransa. Msomi huyo ambaye pia alikuwa mwandishi amefanya utafiti mkubwa na kuandika vitabu kadhaa kwenye uwanja wa elimu ya wadudu.

Read more »

Ijumaa, Oktoba 10, 2014

Ijumaa, Oktoba 10, 2014Leo ni Ijumaa tarehe 15 Mfunguo Tatu Dhilhaji 1435 Hijria sawa na tarehe 10 Oktoba 2014 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1221 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa Imam Ali Naqi (AS) mashuhuri kwa lakabu ya al-Hadi, mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad SAW, katika mji mtakatifu wa Madina. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, yaani Imam Jawad AS, Imam Hadi alichukua jukumu zito la Uimamu na kuongoza Umma wa Kiislamu. Zama za Uimamu wake zilisadifiana na kipindi cha utawala wa ukoo wa Bani Abbas, na Mutawakkil ndiye aliyekuwa ameshika hatamu za uongozi wakati huo. Baada ya mtawala huyo kuhisi kuwa Imam Hadi (as) na wafuasi wake walikuwa hatari kwa utawala wake, aliamrisha Imam atolewe Madina na kuhamishiwa Samarra, Iraq ili amuweke chini ya uangalizi. Licha ya hayo yote, lakini Imam Naqi aliendelea kueneza mafunzo sahihi ya dini tukufu ya Kiislamu.
Miaka 283 iliyopita katika siku kama hii ya leo mnamo mwaka 1731, alizaliwa huko katika mji wa Nice, Henry Cavendish, mwanafalsafa na tabibu wa Kiingereza. Cavendish alikuwa mwalimu wa masomo ya fikizikia, kemia na udaktari. Henry Cavendish alikuwa mtu wa kwanza aliyethibitisha kuwa gesi ya hyadrogen ni nyepesi zaidi kuliko hewa ya kawaida. Cavendish aliaga dunia m waka 1810.
Na miaka 112 iliyopita katika siku kama ya leo, kilifanyika kikao cha kwanza cha Mahakama ya Kimataifa ya Upatanishi ya Hague huko Uholanzi. Mahakama ya Upatanishi ya Hague iliundwa mwaka 1899 kufuatia pendekezo la Tezar Nicolaus wa Pili, Mfalme wa Urusi ya zamani. Mahakama hiyo ni moja kati ya taasisi za kisheria za kimataifa na iko chini ya Umoja wa Mataifa. Mahakama hiyo ina majaji 15 ambao huchaguliwa na Baraza Kuu na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa bila ya kutilia maanani utaifa wao.
Miongoni mwa majukumu ya Mahakama ya Upatanishi ya Kimataifa ya Hague, Uholanzi ni kutatua hitilafu kati ya nchi mbalimbali na kuzuia vita kati ya nchi hizo.
Read more »

Alkhamisi, 09 Oktoba, 2014

Alkhamisi, 09 Oktoba, 2014
Leo ni Alkhamisi tarehe 14 Dhilhaji 1435 Hijria inayosadifiana na tarehe 9 Oktoba 2014.
Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, yaani tarehe 9 Oktoba 1962, nchi ya Uganda ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kuanzia mwaka 1890 Uganda ilikuwa nchini ya makampuni ya Kiingereza yaliyokuwepo Afrika Mashariki, na baada ya kupita miaka kadhaa, ikatawaliwa rasmi na Uingereza. Baada ya kutawaliwa na mkoloni Muingereza, wananchi wa Uganda walipigania uhuru na hatimaye walifanikiwa kujipatia uhuru wao mwaka 1962 katika siku kama ya leo.
Miaka 47 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa Ernesto Che Guevara mwanamapinduzi mashuhuri wa Amerika ya Latini pamoja na wenzake kadhaa. Che Guevara alizaliwa mwaka 1928 nchini Argentina. Fikra za Che Guevara za kuanzisha mapambano dhidi ya ubepari ilizidi kupanuka baada ya kushuhudiwa umaskini na ubaguzi uliotokana na siasa za kipebari za Marekani za kuyanyonya mataifa ya Amerika ya Latini. Ernesto che Guevara alikutana na Fidel Castro huko Mexico na viongozi hao wawili ndio walioongoza mapinduzi ya Cuba hadi kupatikana ushindi. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Cuba mwaka 1959, Che Guevara alielekea Bolivia na kuasisi kundi la wapiganaji wa msituni. Alianza kupambana na serikali ya nchi hiyo iliyokuwa tegemezi kwa Marekani. Lakini katika siku kama ya leo mwaka 1967, wanajeshi wa Bolivia wakisaidiwa na shirika la ujasusi la Narekani CIA waligundua maficho ya Che Guevara na kumuuwa kwa kummiminia risasi.
Na miaka 20 iliyopita katika siku kama leo inayosadifina na tarehe 14 Dhilhaji mwaka 1415 Hijria alifariki dunia Dakta Ahmad al Malt mmoja kati ya viongozi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri baada ya kukamilisha ibada ya Hija katika mji mtakatifu wa Makka. Dakta al Malt alikutana na Hassan al Banna, mwasisi wa Ikhwanul Muslimin wakati walipokuwa masomoni na baadaye akajiunga na kundi hilo. Dakta Ahmad al Malt alishiriki vilivyo katika medani ya vita vilivyojiri kati ya Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel mwaka 1948. Vilevile alishiriki katika vita vya kuwafukuza wavamizi wa Kiingereza katika mfereji wa Suez na katika jihadi ya wananchi wa Afghanistan dhidi ya Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani.
Read more »

Wednesday, October 8

Jumatano, Oktoba 8, 2014

Leo ni Jumatano tarehe 13 Dhilhaji 1435 Hijria sawa na tarehe 8 Oktoba 2014.
Jumatano, Oktoba 8, 2014Siku kama ya leo miaka 1436 iliyopita, sawa na tarehe 13 Dhilhaji mwaka mmoja kabla ya Mtume Mtukufu (S.A.W) kuhamia Madina, yalifanyika makubaliano muhimu ya pili ya Aqabah, kati ya Mtume Mtukufu (saw) na kundi la watu wa mji wa Yathrib ambao baadaye ulijulikana kwa jina la sasa la Madina. Makubaliano hayo yalifuatia makubaliano ya awali yaliyofanyika siku chache kabla. Vita vya muda mrefu kati ya makabila mawili ya Aus na Khazraj katika mji wa Yathrib, vilikuwa sababu ya kutafutwa mtu mwaminifu atakayeweza kurejesha amani na utulivu kati ya pande hizo mbili. Kwa utaratibu huo watu wa Yathrib yaani Madina ya sasa, walimtaka Mtume Muhammad (saw) aende kwenye mji wao ili kuwasuluhisha na kuunga tena udugu baina yao. Watu wa Yathrib pia walifunga mkataba wa kumhami Mtume hadi tone la mwisho la damu yao. Mkataba wa Aqabah ulikuwa na umuhimu mkubwa katika historia ya Uislamu na ulitayarisha uwanja wa Mtume (saw) na Waislamu kuhamia Madina wakitokea Makka na kufungua ukurasa mpya wa kueneza dini ya Uislamu.
Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, kwa mara nyingine tena utawala haramu wa Israel ulifanya jinai nyingine ya kinyama kwa kuwashambulia waumini wa Kipalestina waliokuwa wakisali ndani ya Msikiti mtukufu wa al-Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Wapalestina 20 waliuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa. Mauaji ya Wapalestina yaliyofanywa na utawala ghasibu wa Israel tena ndani ya Msikiti wa al-Aqsa, kwa mara nyingine tena yalilipua ghadhabu za walimwengu dhidi ya utawala huo katili. Hata hivyo kama kawaida, uungaji mkono wa Marekani kwa Israel ulizuia kuchukuliwa hatua yoyote ya kivitendo dhidi ya utawala huo.
Na miaka 9 iliyopita katika siku kama ya leo, mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokuwa na ukubwa wa 7.8 kwa kipimo cha Rishta uliyakumba maeneo ya kaskazini mashariki mwa Pakistan. Kitovu cha mtetemeko huo kilikuwa katika mji wa Muzaffarabad. Watu karibu 90,000 walipoteza maisha yao na wengine 3,300,000 kubaki bila makazi.

Read more »

Jumanne, Oktoba 7, 2014

Leo ni Jumanne tarehe 12 Dhilhaji 1435 Hijria sawa na Oktoba 7, 2014.
Jumanne, Oktoba 7, 2014Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita sawa na tarehe 7 Oktoba 2001, Marekani iliivamia Afghanistan. Uvamizi huo ulifanyika kwa kisingizio cha kuliangamiza kundi la wanamgambo wa Al-Qaida ambao kwa mujibu wa Washington walihusika na tukio la Septemba 11 2001 nchini Marekani. Katika kip indi cha wiki kadhaa, ndege za kivita za Marekani, zilifanya mashambulizi dhidi ya ngome za kundi la Taliban ambalo katika kipindi hicho lilikuwa likidhibiti eneo kubwa la ardhi ya Afghanistan sambamba na kuliunga mkono kundi la Al-Qaida lililokuwa likiongozwa na Osama bin Laden. Mashambulizi hayo mazito ya Marekani yaliua na kujeruhi maelfu ya raia wasio na hatia wa Afghanistan huku wengine wakilazimika kuwa wakimbizi. Hata hivyo pamoja na Marekani kusaidiwa na muungano wa vikosi vya kaskazini mwa Afghanistan na kufanikiwa kuuangusha utawala wa Taliban, hadi leo haijaweza kumtia mbaroni Mulla Omar na viongozi wengine wa kundi hilo la Taliban.
Miaka 65 iliyopita, Ujerumani ya Mashariki iliasisiwa na kuwa na mfumo wa Jamhuri ya Kidemokrasia. Katika miezi ya mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, Shirikisho la Umoja wa Sovieti liivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Ujerumani ya Mashariki, na madola ya Magharibi yakadhibiti sehemu ya magharibi mwa nchi hiyo. Hata hivyo baadaye Umoja wa Sovieti ulijitoa katika Baraza la Makamanda wa Waitifaki baada ya kutofautiana na madola ya Magharibi juu ya namna ya kuiendesha nchi hiyo.
Na siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, yaani tarehe saba Oktoba mwaka 1940 majeshi ya Ujerumani ya Kinazi yaliidhibiti na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Romania katika kipindi cha Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Kwa utaratibu huo, uwanja wa majeshi ya Ujerumani wa kuishambulia ardhi ya lililokuwa Shirikisho la Umoja wa Sovieti mnamo Juni 1941 ukawa umeandaliwa.
Read more »

Jumapili, 05 Oktoba, 2014

Jumapili, 05 Oktoba, 2014Leo ni Jumapili tarehe 10 Dhul-Hijja mwaka 1435 Hijria, sawa na tarehe 5 Oktoba mwaka 2014 Miladia.
Leo tarehe 10 Dhilhaj ni sikukuu ya Idul Adh'ha, moja ya sikukuu kubwa za Kiislamu. Katika siku hii mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu waliokwenda Makka, huchinja mnyama kwa ajili ya kutekeleza amri ya Mola wao na kuhuisha kumbukumbu ya Nabii Mtukufu Ibrahim (as). Mwenyezi Mungu aliijaribu imani na ikhlasi ya Nabii huyo kwa kumuamuru amchinje mwanawe kipenzi Ismail (as). Licha ya mashaka ya utekelezwaji wa amri hiyo, Nabii Ibrahimu (as) aliandaa mazingira ya utekelezwaji wake na kumlaza chini mwanaye huyo na kuanza kuikata shingo yake lakini kisu kilikataa kuchinja. Hapo ndipo akaambiwa na Mwenyezi Mungu kuwa amefaulu mtihani huo na akamtumia mnyama wa kuchinja badala ya mwanaye Ismail. Tukio hili lenye ibra na mafunzo tele linawapa wanadamu somo la kujitoa mhanga, kujisabilia kwa ajili ya Allah, kushinda matamanio na matakwa ya nafsi na kusalimu amri mbele ya amri za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu kote duniani kwa mnasaba wa sikukuu hii kubwa.
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, Imam Khomeini (MA) Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alihama Iraq na kuelekea Paris Ufaransa. Imam Khomeini aliamua kufanya hijra hiyo ya kihistoria wakati utawala wa zamani wa Iraq ulipoanza kumzuia ache harakati zake za mapambano dhidi ya utawala wa Shah. Serikali ya wakati huo ya Iraq ambayo ilikuwa ikilinda mahusiano na utawala wa Shah nchini Iran, ilimtaka Imam Khomeini ajiepushe na harakati zozote za kisiasa na za kimapinduzi dhidi ya utawala huo wa Shah. Hata hivyo Imam aliimbia serikali hiyo kuwa hilo lilikuwa ni jukumu lake la kisheria ambalo aliwajibika kulitekeleza na kusisitiza juu ya kuendeleza mapambano yake kwa kutoa hotuba na kutuma kanda za kimapinduzi nchini Iran.
Siku kama ya leo miaka 14 iliyopita, Slobodan Milosevic dikteta wa Yugoslavia na muhusika mkuu wa vita vya umwagaji damu huko Balkan, alijiuzulu baada ya miezi kadhaa ya malalamiko ya ndani na vikwazo vya kimataifa. Milosevic alikuwa rais wa Serbia tangu mwaka 1990 hadi 1997 na baadaye akawa rais wa Jamhuri ya Yugoslavia. Katika vita vya Bosnia, na kwa uungaji mkono wa kila upande wa Waserbia, Slobodan Milosevic alishiriki pakubwa katika kutekeleza mauaji ya kizazi dhidi ya Waislamu wa Bosnia. Slobodan Milosevic alikuwa kiongozi wa kwanza mtenda jinai za kivita kuwahi kufikishwa katika mahakama ya kimataifa kwa ajili ya kuhukumiwa.
Na siku kama ya leo miaka 150 iliyopita, alizaliwa Louis Jean Lumiere, mwanakemia mwanaviwanda mashuhuri wa Kifaransa. Mwaka 1895 akiwa pamoja na ndugu yake, aliyejulikana kwa jina la Auguste Lumiere, walifanikiwa kutengeneza kifaa ambacho kiliwasaidia kuchukua picha mbalimbali na kusajili harakati. Mwaka huo huo Lumiere alifanikiwa kuonyesha filamu yake ya kwanza au Motion Picture katika majumba ya sinema.
Read more »

Jumamosi, Oktoba 4, 2014

Leo ni Jumamosi tarehe  9 Mfunguo Tatu Dhil-Hija mwaka 1435 Hijria mwafaka na tarehe 4 Oktoba mwaka 2014 Miladia.
Jumamosi, Oktoba 4, 2014Leo ni siku ya Arafa tarehe 9 Dhil-Hija. Arafa ni jina la jangwa kubwa linalopakana na mlima wa Jabalur Rahma ulioko kusini mashariki mwa Makka. Tangu adhuhuri ya siku hii mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu al Kaaba husimama katika uwanja wa Arafa na hadithi nyingine za Kiislamu zimetaja fadhila na utukufu mkubwa wa kisimamo hicho. Hadithi zinasema kuwa Mwenyezi Mungu SW ameifa nya ardhi ya Arafa ambayo ilikuwa medani ya matukio mengi muhimu ya kihistoria, kuwa mahala pa kuwapokea wageni wake wanaokwenda Hija na ameweka meza na karamu yake pembeni ya mlima wa Jabalur Rahma. Ni vyema kukumbusha kuwa magharibi ya siku hii ya leo mahujaji wanaondoka uwanja wa Arafa na kuelekea Mash'arul Haram na kujitayarisha kwa ajili na amali nyingine za Hija. ***
Siku kama ya leo miaka 1375 iliyopita, Muslim bin Aqil binamu wa Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib AS aliuawa shahidi mjini Kufa Iraq. Alikuwa mmoja wa shakhsia wakubwa na wacha Mungu katika zama zake. Alielekea mjini al-Kufa, Iraq akiwa na lengo la kwenda kutathmini ni kwa kiwango gani watu wa mji huo walikuwa wakimtii Imam Hussen, baada ya watu wa mji huo kumwandikia maelfu ya barua Imam huyo wakimtaka aende mjini humo na kwamba wako tayari kumuunga mkono katika harakati yake dhidi utawala dhalimu wa  Yazid bin Muawiya. Watu wa Kufa walimsaliti Muslim bin Aqil baada ya kuhadaika kwa hila na uongo wa Ubeidullah bin Ziyad, mtawala wa wakati huo wa Kufa na wakamuacha Muslim bin Aqiil peke yake. ***
Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita nchi ya Kiafrika ya Lesotho ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza. Kabla ya uhuru, Lesotho ilikuwa ikijulikana kwa jina la Basutoland na kuanzia mwaka 1884 ikawa chini ya mkoloni Mwingereza. Uingereza iliendelea kuikalia kwa mabavu Lesotho hadi mwaka 1966 na hatimaye nchi hiyo ikapata uhuru kamili katika siku kama ya leo. Lesotho iko kusini mwa bara la Afrika huku ikiwa imezingirwa na jirani yake Afrika Kusini. ***
Miaka 57 iliyopita katika siku kama ya leo satalaiti ya kwanza ilirushwa angani na msomi wa Urusi ya zamani na kwa utaratibu huo zama za udhibiti wa anga zikaanza. Satalaiti hiyo iliyopewa jina la Sputnik 1 ilizunguka dunia mara 1400 kwa siku 92 na kwa mara ya kwanza ikafikisha ujumbe wa radio kutoka angani kuelekea ardhini. ***
Katika siku kama ya leo miaka 184 iliyopita  nchini ya Ubelgiji ilijitangazia uhuru wake. Kuanzia karne ya 18 Ubelgiji ilikuwa chini ya udhibiti wa Austria na mwishoni mwa karne hiyo hiyo ikawa chini ya udhibiti wa Ufaransa. Hata hivyo baada ya Napoleone Bonaparte kushindwa na madola ya Ulaya, mwaka 1815 Miladia, Ubelgiji na Uholanzi zilunda muungano. Hata hivyo muungano huo haukudumu baada ya Wakatoliki wa Ubelgiji kuanzisha uasi dhidi ya Waprotestani wa Uholanzi na kuitanga nchi yao kuwa huru. ***
Na tarehe 4 Oktoba mwaka 1963 yaani miaka 51 iliyopita kimbunga cheusi cha Caribbean kilianza na kuangamiza suhula zote za bandari na visiwa vya bahari ya Caribean. Kimbunga hicho angamizi kilikuwa na kasi ya kilomita 150 kwa saa na kwa ujumla kiliua karibu watu elfu sita wengi wao wakiwa raia wa Cuba na Haiti. *
Read more »

Ijumaa, Oktoba 3, 2014

 Ijumaa, Oktoba 3, 2014
Leo ni Ijumaa tarehe 8 Dhulhuja 1435 Hijria sawa na tarehe 3 Oktoba 2014.
Katika siku kama ya leo miaka 1375 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Imam Hussein bin Ali (AS), mjukuu wa Mtume SAW aliondoka Makka na kuelekea Kufa nchini Iraq baada ya kukataa kumbai na kutoa kiapo cha utiifu kwa Yazid bin Muawiya. Miezi minne kabla ya hapo, Imam Hussein alikuwa amewasili mjini Makka akiwa pamoja na familia yake na alikitumia kipindi cha kuweko waumini waliotoka katika pembe mbalimbali za dunia kwa ajili ya kufanya ziara katika nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu, kuwaamsha na kuwabainishia dhulma na ufisadi mkubwa uliokuwa ukifanywa wa utawala wa Yazid mwana wa Muawiya. Wakati huo huo kutokana na wito wa mara kwa mara wa watu wa Kufa na njama za utawala wa Yazidi za kutaka kumuuwa, Imam Hussein aliondoka Makka na kueleka Kufa. 

Miaka 82 iliyopita katika siku kama ya leo Iraq ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza.  Iran iliiweka Iraq chini ya mamlaka yake mwaka 539 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa (A.S). Iraq ilikuwa sehemu ya utawala wa kifalme wa Iran hadi ardhi hiyo ilipokombolewa na Waislamu mwaka 642 Miladia. Iraq iliendelea kudhibitiwa na utawala huo wa kifalme hadi mwishoni mwa utawala wa Bani Ummaya na mji wa Baghdad ukachaguliwa kuwa makao makuu sambamba na kuingia madarakani utawala wa Abbasiya.

Na miaka 36 iliyopita katika siku kama ya leo, baada ya Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu kuzuiwa kuendesha shughuli za kisiasa na kidini huko Iraq, mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliamua kuondoka Iraq na kuelekea Kuwait. Hata hivyo serikali ya Kuwait ilimzuia Imam kuingia nchini humo ili kulinda uhusiano wake na utawala wa Shah. Kufuatia hatua hiyo, Imam Khomeini siku kadhaa baadaye alielekea nchini Ufaransa. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, miamala na vitendo visivyo vya kibinadamu vya utawala wa Baath wa Iraq dhidi ya Imam Khomeini vilizusha hasira za wananchi wa Iran, ambao walikuwa katika kipindi nyeti cha kupambana na utawala dhalimu wa Shah hapa nchini.
Read more »

Thursday, October 2

Alkhamisi, 02 Oktoba, 2014

Alkhamisi, 02 Oktoba, 2014Leo ni Alkhamisi tarehe 7 Dhulhaji 1435 Hijria sawa na Oktoba 2, 2014.
Tarehe 7 Dhulhija miaka 1321 iliyopita, aliuawa shahidi Imam Muhammad Baqir AS mjukuu mtukufu wa Mtume wa Uislamu Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharibu katika kizazi chake. Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya "Baqir" yaani mchimbua elimu. Kipindi cha uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah, suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa. Redio Tehran inatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote kwa mnasaba huu mchungu wa kuuliwa shahidi Imam Baqir (AS).
Siku kama ya leo miaka 827 iliyopita mwafaka na tarehe 2 Oktoba 1187, Swalahuddin Ayyubi kamanda wa jeshi la Kiislamu alifanikiwa kuikomboa Baitul Muqaddas katika Vita vya Msalaba. Baitul Muqaddas, ni kibla cha kwanza cha Waislamu na mahala ambako Mtume Mtukufu Muhammad SAW alianzia safari yake ya 'Miiraji' kuelekea mbinguni. Awamu ya kwanza ya Vita vya Msalaba ilianza mwaka 1095 Miladia na vilimalizika kabisa mwaka 1270 baada ya kushindwa kikamilifu jeshi la Msalaba.
Siku kama ya leo miaka 110 iliyopita sawa na tarehe Pili Oktoba 1904, alizaliwa mwandishi wa Uingereza Graham Greene. Vitabu vya msomi huyo viliakisi mpambano baina ya mema na mabaya na aliandika kwenye kitabu chake kinachoitwa 'Nguvu na Utukufu' kwamba subira, uvumilivu na mateso ni njia ya wokovu. Graham Greene ameacha vitabu vingi kama 'Mtu wa Tatu', 'Utawala wa Hofu' na 'Muuaji wa Kukodishwa'. Mwandishi huyo Muingereza alifariki dunia mwaka 1991.
Na siku kama ya leo miaka 73 iliyopita sawa na tarehe Pili Oktoba 1941, kiongozi wa Ujerumani ya Kinazi Adolph Hitler, alitoa amri ya kuanza awamu ya pili ya mashambulizi ya jeshi la hiyo dhidi ya Urusi ya zamani. Kwenye awamu ya kwanza ya mashambulizi ya jeshi la nchi hilo iliyoanza tarehe 22 Juni 1941, Ujerumani iliweza kuikalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Urusi. Lengo la kufanywa shambulio hilo la dikteta Hitler, lilikuwa ni kurahisisha operesheni za kijeshi, kudhoofisha nguvu za Jeshi Jekundu na kudhibiti ardhi zaidi za Urusi hasa Moscow mji mkuu wa nchi hiyo.
Read more »

Jumatano, Oktoba Mosi, 2014

Leo ni Jumatano tarehe 6 Dhulhija 1435 Hijria inayosadifiana na tarehe Mosi Oktoba 2014.
Jumatano, Oktoba Mosi, 2014Tarehe 6 Dhilhaji mwaka 1407 Hijria yaani siku kama ya leo miaka 28 iliyopita mamia ya mahujaji wa Kiirani na mahujaji kadhaa wa nchi nyinginezo wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu waliuawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa serikali ya Saudi Arabia, walipokuwa wakitekeleza faradhi ya kujibari na kujiweka mbali na washirikina. Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu hutekeleza ibada hiyo kila mwaka wakati wa Hija, kutokana na mafunzo ya Kiislamu na Qur'ani Tukufu, ambapo sambamba na kutoa wito wa umoja na mshikamano baina ya Waislamu, hutoa tangazo la kujiweka mbali na maadui wa Uislamu hasa Marekani na utawala ghasibu wa Israel. Kwa kutilia maanani umuhimu wa suala hiyo mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayati Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) daima alikuwa akisisitiza katika ujumbe wake kwa wahujaji juu ya kufanya shughuli hiyo ya kujitenga na washirikina na mabeberu, na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Ali Khamenei pia amekuwa akisisitiza sana juu ya umuhimu wa kufanyika kwake na kwamba inawaamsha Waislamu na kudhihirisha uwezo na nguvu zao.
Miaka 29 iliyopita sawa na siku kama ya leo ya tarehe Mosi Oktoba mwaka 1985 ndege za kijeshi za utawala haramu wa Israel ziliyashambulia makao ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) huko Tunisia. Watu wapatao 70 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa kufuatia mashambulio hayo. PLO ilikuwa imehamishia makao yake Tunisia kutoka Lebanon baada ya mashambulio ya kijeshi ya utawala haramu wa Israel nchini humo mwaka 1982. Hata hivyo uungaji mkono wa Marekani kwa utawala huo ulilifanya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lishindwe kuchukua hatua zozote za maana dhidi ya Tel Aviv.
Na Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, nchi ya Nigeria ilipata uhuru. Wareno waliwasili Nigeria katika karne ya 15 na mkoloni Mwingereza naye akawasili katika nchi hiyo katika karne ya 16. Katika karne ya 17 ardhi ya Nigeria iligeuzwa na kuwa moja kati ya vituo muhimu vya biashara ya utumwa. Mwishoni mwa karne ya 19 vikosi vya jeshi la Uingereza viliidhibiti kikamilifu ardhi ya Nigeria. Mwaka 1914 Uingereza iliziunganisha nchi mbili za Nigeria ya Kaskazini na Kusini zilizokuwa chini ya udhibiti wake na kuunda koloni moja la Nigeria. Miaka 40 baadaye nchi hiyo ilijitangazia  utawala wa ndani. Hatimaye baada ya kupitia misukosuko mingi, Nigeria ilipata uhuru katika siku kama hii ya leo.
Read more »

Jumanne, Septemba 30, 2014

Jumanne, Septemba 30, 2014Leo ni Jumanne tarehe 5 Dhulhija 1435 Hijria, sawa na Septemba 30, 2014.
Tarehe 30 Septemba miaka 29 iliyopita alifariki dunia mvumbuzi wa kipimo kinachotumiwa kupimia nguvu ya mitetemeko ya ardhi Charles Richter. Charles Richter alishirikiana na mhakiki mwingine kusanifu nguvu ya mitetemeko kwa mujibu wa nishati inayotokana na mawimbi ya mitetemeko hiyo toka daraja moja hadi 9 na kusajili kipimo cha Rishta. Kabla ya hapo wataalamu walikuwa wakipima mitetemeko ya ardhi kwa mujibu wa athari zake, kipimo ambacho hakikuwa cha kuaminika.
Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita nchi ya Botswana ilifanikiwa kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Mwaka 1885 Botswana iliwekwa katika himaya ya mkoloni Mwingereza. Tangu mwaka 1920 mapambano makali ya wapigania uhuru nchini humo yalishadidi na Botswana ikapata uhuru mwaka 1966 na kukaundwa serikali ya jamhuri. Botswana inap atikana kusini mwa bara la Afrika na inapakana na nchi za Afrika Kusini, Zimbabwe na Namibia.
Na siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, alifariki dunia huko Najaf, Iraq Allamah Muhammad Hussein Kampani, mwanafalsafa, faqihi na mwanairfani mkubwa. Alizaliwa mwaka 1296 Hijria mjini Kadhimain nchini Iraq. Msomi huyo mkubwa pia alitabahari katika elimu za falsafa, tiba, irfan, historia, kijografia, mashairi na fasihi. Mbali na hayo Allamah Hussein Kampani alikuwa na fikra pevu na uwezo mkubwa wa kubainisha mambo. Msomi huyo ameandika vitabu kadhaa katika nyanja mbalimbali ikiwemo diwani ya mashairi akisifu viongozi wa Uislamu
Read more »

Jumatatu, Septemba 29, 2014

Leo ni Jumatatu tarehe 4 Mfunguo tatu Dhil-Hijja mwaka 1435 Hijiria inayosadifiana na tarehe 29 Septemba mwaka 2014 Miladia.
Jumatatu, Septemba 29, 2014
Siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, ulifanyika uchaguzi huru wa kwanza nchini Angola. Katika uchaguzi huo chama cha MPLA kilichokuwa kikiongoza nchini humo tangu mwaka 1976 kilipata ushindi na kiongozi wake Jose Edward Dos Santos akachaguliwa tena kuingoza nchi hiyo. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, Angola ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno hapo mwaka 1975. Vita vya ndani nchini humo vilihitimishwa rasmi mwaka 2002 baada ya kuuawa kiongozi wa chama cha upinzani cha UNITA Jonas Savimbi.
Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, muwafaka na tarehe 7 Mehr 1360 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Hujjatul Islam Sayyid Abdul Karim Hasheminejad mwanachuoni na mwana mapambano shupavu wa Iran katika mji wa Mashhad. Sayyid Hasheminejad aliuawa shahidi baada ya kupigwa risasi na mmoja wa wanachama wa kundi la Munafikiin. Mwanachuoni huyo alikuwa mstari wa mbele katika harakati za mapinduzi nchini Iran dhidi ya utawala wa Shah, na aliwahi kuteswa na kuwekwa gerezani mara kadhaa.
Siku kama ya leo miaka 113 iliyopita, alizaliwa mwanafizikia mashuhuri wa Italia Enrico Fermi katika mji wa Roma. Baada ya kukamilisha masomo ya chuo kikuu aliweza kuvumbua kanuni ya Mwendo wa Molekuli ya Gesi. Fermi alifanya uchunguzi kuhusu mabadiliko ya atomu na akafanikiwa kutengeneza betri ya atomu kwa kuipasua na kutoa nje nishati yake. Mwanafizikia huyo wa Italia alifariki dunia mwaka 1954.
Na miaka 96 iliyopita muwafa na leo, nchi ya Bulgaria ilisalimu amri baada ya kushindwa mara kadhaa katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Bulgaria ilikuwa pamoja na Ujerumani, utawala wa Othmania, Austria na Hungary na zilikuwa zikipigana dhidi ya Ufaransa, Russia, Uingereza na Italia. Baada ya Bulgaria kushindwa katika vita vya Macedonia, Desemba 15 mwaka 1918 ilitia saini Mkataba wa Salonica katika mji wenye jina hilo nchini Ugiriki ya leo
Read more »

Author

CONTACT ME FOR WEB AND BLOG DESIGNING...

uislam na maisha yake

uzayuni

swahili radio

uislam na maisha

mohamed waziri

Subscribe to our Mailing List

We'll never share your Email address.
+255 (762) 118-805 mohamedwaziri295@gmail.com