Tarehe 7 Dhulhija miaka 1321 iliyopita, aliuawa shahidi
Imam Muhammad Baqir AS mjukuu mtukufu wa Mtume wa Uislamu Muhammad (SAW)
na mmoja wa Maimamu watoharibu katika kizazi chake. Imam Baqir AS
alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika
uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya
zama na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya "Baqir" yaani mchimbua elimu.
Kipindi cha uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa
utawala wa Bani Umayyah, suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea
Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa
ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea
wagonjwa. Redio Tehran inatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote kwa
mnasaba huu mchungu wa kuuliwa shahidi Imam Baqir (AS).
Siku kama ya leo miaka 827 iliyopita mwafaka na tarehe 2
Oktoba 1187, Swalahuddin Ayyubi kamanda wa jeshi la Kiislamu alifanikiwa
kuikomboa Baitul Muqaddas katika Vita vya Msalaba. Baitul Muqaddas, ni
kibla cha kwanza cha Waislamu na mahala ambako Mtume Mtukufu Muhammad
SAW alianzia safari yake ya 'Miiraji' kuelekea mbinguni. Awamu ya kwanza
ya Vita vya Msalaba ilianza mwaka 1095 Miladia na vilimalizika kabisa
mwaka 1270 baada ya kushindwa kikamilifu jeshi la Msalaba.
Siku kama ya leo miaka 110 iliyopita sawa na tarehe Pili
Oktoba 1904, alizaliwa mwandishi wa Uingereza Graham Greene. Vitabu vya
msomi huyo viliakisi mpambano baina ya mema na mabaya na aliandika
kwenye kitabu chake kinachoitwa 'Nguvu na Utukufu' kwamba subira,
uvumilivu na mateso ni njia ya wokovu. Graham Greene ameacha vitabu
vingi kama 'Mtu wa Tatu', 'Utawala wa Hofu' na 'Muuaji wa Kukodishwa'.
Mwandishi huyo Muingereza alifariki dunia mwaka 1991.
Na siku kama ya leo miaka 73 iliyopita sawa na tarehe Pili
Oktoba 1941, kiongozi wa Ujerumani ya Kinazi Adolph Hitler, alitoa amri
ya kuanza awamu ya pili ya mashambulizi ya jeshi la hiyo dhidi ya Urusi
ya zamani. Kwenye awamu ya kwanza ya mashambulizi ya jeshi la nchi hilo
iliyoanza tarehe 22 Juni 1941, Ujerumani iliweza kuikalia kwa mabavu
sehemu ya ardhi ya Urusi. Lengo la kufanywa shambulio hilo la dikteta
Hitler, lilikuwa ni kurahisisha operesheni za kijeshi, kudhoofisha nguvu
za Jeshi Jekundu na kudhibiti ardhi zaidi za Urusi hasa Moscow mji mkuu
wa nchi hiyo.
0 toamaon yako: