Tanzania swahili radio

IQRA FM RADIO

IQRA FM RADIO
IQRA FM RADIO ELIMU NA MATENDO UIMARA WA RADIO IQRA UPO MIKONOMI MWAKO CHANGIA RADIO IQRA KWA MPESA 0762118805TIGO PESA 0658118804

Sunday, September 28

Jumapili, 28 Septemba 2014 13:27 Libya yaendelea kugubikwa na machafuko

Posted by mkachu  |  Tagged as:

Libya yaendelea kugubikwa na machafuko
Nchi ya Libya iliyoko kaskazini mwa Afrika ingali inakabiliwa na hali mbaya ya machafuko na ukosefu wa amani. Mapigano, utumiaji mabavu, mauaji na milipuko ni mambo ambayo yamegeuka na kuwa matukio ya kawaida kabisa yanayotokea kila siku nchini Libya. Serikali ya Tripoli nayo haina la kufanya ghairi ya kuinyooshea jamii ya kimataifa mkono wa kuomba msaada. Aguila Saleh Issa, Spika wa Bunge la Libya ameitaka jamii ya kimataifa iipatie silaha zaidi nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Kwani spika huyo anaamini kwamba, bila ya kuwa na silaha nchi hiyo haiwezi kukabiliana na ugaidi na vitendo vya utumiaji mabavu. Nukta nyingine ambayo imeashiriwa na Spika wa Bunge la Libya ni hii kwamba, jamii ya kimataifa imeitelekeza Libya katikati ya vurugu na machafuko na kupuuza kabisa hali ya mambo inayoikabili nchi hiyo. Filihali nchi ya Libya iko katika hali mbaya. Kwa sasa ni mara chache mno kushuhudia siku moja ikipita pasina ya nchi hiyo kushuhudia milipuko kadhaa. Siku mbili zilizopita watu sita waliuliwa katika mji wa Benghazi. Tukio hili lilijiri katika hali ambayo, mapigano makali kati ya makundi hasimu katika miji mbalimbali ya Libya ukiwemo Benghazi na mji mkuu Tripoli yangali yanaendelea kushuhudiwa. Kando ya matukio hayo hatari, inaonekana kuwa, kuna mauaji ya umati yanayofanywa na pande zinazopigana katika maeneo zinayoyadhibiti. Hivi karibuni kaburi la umati liligunduliwa kusini mwa Tripoli.  Fauka ya hayo, mashambulio ya makombora na yale ya anga ambayo katika siku za hivi karibuni yameshuhudiwa nchini Libya, yameifanya hali ya wananchi wa nchi hiyo kuwa mbaya mno. Mazingira na hali mbaya inayowakabiliwa wananchi wa Libya, imezifanya baadhi ya duru za kisiasa na asasi za kimataifa kutoa indhari juu ya uwezekano wa nchi hiyo kukabiliwa na maafa ya kibinadamu. Hata hivyo swali la kimsingi linaloulizwa na wengi ni kwamba, je ni kwa nini Libya imetumbukia katika kinamasi hiki? Je, sababu za ndani zimekuwa na mchango kati hili au kuna mikono kutoka nje ambayo inafanya njama za kuisukuma Libya katika korongo la mgogoro? Hapana shaka kuwa, sababu na matukio ya ndani yana nafasi maalumu katika kuibuka na kushadidi mapigano na hali ya mchafukoge nchini Libya. Kuzagaa maelfu ya silaha ambazo ni mabaki ya kipindi cha utawala wa Kanali Muammar Gaddafi, dikteta wa zamani wa Libya, lenyewe hilo ni tishio kwa nchi hiyo ambayo suala la taasubi za kikabila ndilo linaloongoza. Kwa sasa silaha na utumiaji mabavu ni wenzo unaotumiwa na makundi ya kikabila yanayobeba silaha kwa ajili ya kudai matakwa yao.           Makabila ambayo, tab’ani yanataka kuwa na hisa yao katika muundo wa kiutawala wa nchi hiyo. Katika upande wa pili wa sarafu ni kwamba, kutokuweko sheria madhubuti zilizoandaliwa kwa ajili ya kuiongoza nchi hiyo ni jambo linalotathminiwa na wapembuzi wa mambo kwamba, limekuwa na taathira katika hatima ya sasa ya nchi hiyo. Pamoja na hayo, inawezekana kusema kuwa, kitu ambacho kinaitesa zaidi Libya kwa sasa kuliko jambo jingine lolote ni vita vya madaraka baina ya makundi yenye taathira nchini humo. Serikali, wanamgambo, wanamapinduzi wa zamani na viongozi wa makundi mbalimbali ya kisiasa ni miongoni mwa pande ambazo zinataka kuwa na hisa katika muundo mpya wa kisiasa wa Libya. Licha ya hayo jambo ambalo halipaswi kupuuzwa ni kwamba, utajiri wa mafuta wa Libya nao umekuwa na taathira katika kuibuka mgogoro wa nchi hiyo. Libya inahesabiwa kuwa stoo ya mafuta na nishati barani Afrika. Ni kutokana na sababu hiyo, ndio maana madola ya Ulaya yameingiwa na uchu na tamaa ambayo imeyavuta na kuyafanya yajitumbukize katika kadhia na matukio ya Libya. Baadhi ya weledi wa mambo wanaamini kwamba, sehemu ya mgogoro huo inatokana na hizi harakati za madola ya kigeni ambayo yanatokwa na mate ya uchu wa mafuta ya Libya. Ni jambo lililo wazi kwamba, kuendelea machafuko nchini Libya kunaweza kuyasafishia njia madola ya Ulaya na Magharibi katika kufikia malengo yao.

0 toamaon yako:

Author

CONTACT ME FOR WEB AND BLOG DESIGNING...

uislam na maisha yake

uzayuni

swahili radio

uislam na maisha

mohamed waziri

Subscribe to our Mailing List

We'll never share your Email address.
+255 (762) 118-805 mohamedwaziri295@gmail.com