
Rais Hassan Sheikh Mohamoud wa Somalia ametangaza kuwa, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa 2014, kundi la wanamgambo wa al-Shabab litalazimika kuondoka katika maeneo na miji linayoidhibiti katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Mtandano wa Habari wa al-Yaum Sab’i umemnukuu Rais Hassan Sheikh Mohamoud akisema kwamba, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Desemba ujao jeshi la Somalia na vikosi vya kusimama amani vya Umoja wa Afrika AMISOM vitakuwa vimefanikiwa kuwafurusha wanamgambo wa al-Shabab na kuwalazimisha kuondoka katika maeneo wanayoyadhibiti.
Rais wa Somalia ambaye kwa sasa yuko nchini Denmark alikokwenda kushiriki mkutano wa kimataifa kuhusu Somalia amesema kuwa, wanamgambo wa al-Shabab watalazimika kurejea nyuma na kwenda katika vijiji vya mbali na hivyo mashambulio yao baada ya hapo yatakuwa ya hapa na pale. Rais Mohamoud amebainisha kwamba, serikali ya Somalia inafanya kila iwezalo ili kuhakikisha kwamba, hadi kufikia miezi mitatu ya awali ya mwaka ujao wa 2015 kusiweko eneo lolote nchini humo ambalo linadhibitiwa na wanamgambo wa al-Shabab.
0 toamaon yako: