
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa
kesi za maambukizi ya ugonjwa wa Ebola zimeongezeka nchini Sierra Leone
huku nchi hiyo ikikabiliwa na tatizo la ukosefu wa vituo vya matibabu.
Mpango wa Dharura wa Kukabiliana na Ebola wa Umoja wa Mataifa (UNMEER)
umesema wiki hii kuwa, mfumuko wa ugonjwa wa Ebola umesababisha vifo vya
watu zaidi ya 1,060 nchini Sierra Leone huku maeneo yaliyoathiriwa
zaidi yakiwa ya magharibi mwa mji mkuu Freetown. Mpango huo aidha
umesema, ukosefu wa vitanda katika vituo vya kutibu Ebola umesababisha
familia kuangalia zenyewe wagonjwa majumbani, ambako waangalizi huwa
hawana uwezo wa kutosha wa kujilinda wasiambukizwe virusi vya ugonjwa
huo, na kwa sababu hiyo maambukizo yameongezeka.
Jumatano Shirika la Afya Duniani (WHO)
liliripoti kuwa, idadi ya kesi za maambukizo ya Ebola zinaongezaka
nchini Sierra Leone, ingawa ugonjwa huo umepungua katika nchi ya Liberia
huku nchini Guinea maambukizo yakiwa ya wastani.
0 toamaon yako: