
Mwakilishi mpya wa Umoja wa Mataifa
nchini Sudan Kusini ametaka zifanyike juhudi kubwa za kulindwa usalama
wa raia wa nchi hiyo. Ellen Margrethe Loej ambaye ameteuliwa hivi
karibuni kuwa mjumbe mpya wa Ban Ki moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
nchini Sudan Kusini amesema kwamba, atalipa kipaumbele suala la
kulindwa usalama wa raia, na kusisitiza kwamba Sudan Kusini linakabiliwa
na changamoto nyingi likiwemo suala la wimbi la wakimbizi. Mwakilishi
wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini ameongeza kuwa,
kuna ulazima wa kutumiwa suhula zaidi kwa lengo la kudhaminiwa mahitajio
ya watu wanaohitajia misaada ya kibinadamu. Ellen Loej amesisitiza
kwamba watu waliotenda jinai za kivita au zilizo dhidi ya binadamu
wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria. Inafaa kuashiria hapa kuwa,
machafuko nchini Sudan Kusini yalianza mwezi Disemba mwaka jana, na hadi
sasa viongozi wa serikali ya Juba na waasi wanaoongozwa na Riek Machar
makamu wa zamani wa rais wameshatiliana saini makubaliano ya amani mara
nne, lakini makubaliano hayo yamekuwa yakikiukwa na pande hizo mbili.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP limetangaza kuwa, watu zaidi ya
milioni moja na nusu wa nchi hiyo wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na
nje ya nchi hiyo.
0 toamaon yako: