Leo ni Alkhamisi tarehe 14 Dhilhaji 1435 Hijria inayosadifiana na tarehe 9 Oktoba 2014.
Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, yaani tarehe 9 Oktoba 1962, nchi ya Uganda ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kuanzia mwaka 1890 Uganda ilikuwa nchini ya makampuni ya Kiingereza yaliyokuwepo Afrika Mashariki, na baada ya kupita miaka kadhaa, ikatawaliwa rasmi na Uingereza. Baada ya kutawaliwa na mkoloni Muingereza, wananchi wa Uganda walipigania uhuru na hatimaye walifanikiwa kujipatia uhuru wao mwaka 1962 katika siku kama ya leo.
Miaka 47 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa Ernesto Che Guevara mwanamapinduzi mashuhuri wa Amerika ya Latini pamoja na wenzake kadhaa. Che Guevara alizaliwa mwaka 1928 nchini Argentina. Fikra za Che Guevara za kuanzisha mapambano dhidi ya ubepari ilizidi kupanuka baada ya kushuhudiwa umaskini na ubaguzi uliotokana na siasa za kipebari za Marekani za kuyanyonya mataifa ya Amerika ya Latini. Ernesto che Guevara alikutana na Fidel Castro huko Mexico na viongozi hao wawili ndio walioongoza mapinduzi ya Cuba hadi kupatikana ushindi. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Cuba mwaka 1959, Che Guevara alielekea Bolivia na kuasisi kundi la wapiganaji wa msituni. Alianza kupambana na serikali ya nchi hiyo iliyokuwa tegemezi kwa Marekani. Lakini katika siku kama ya leo mwaka 1967, wanajeshi wa Bolivia wakisaidiwa na shirika la ujasusi la Narekani CIA waligundua maficho ya Che Guevara na kumuuwa kwa kummiminia risasi.
Na miaka 20 iliyopita katika siku kama leo inayosadifina na tarehe 14 Dhilhaji mwaka 1415 Hijria alifariki dunia Dakta Ahmad al Malt mmoja kati ya viongozi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri baada ya kukamilisha ibada ya Hija katika mji mtakatifu wa Makka. Dakta al Malt alikutana na Hassan al Banna, mwasisi wa Ikhwanul Muslimin wakati walipokuwa masomoni na baadaye akajiunga na kundi hilo. Dakta Ahmad al Malt alishiriki vilivyo katika medani ya vita vilivyojiri kati ya Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel mwaka 1948. Vilevile alishiriki katika vita vya kuwafukuza wavamizi wa Kiingereza katika mfereji wa Suez na katika jihadi ya wananchi wa Afghanistan dhidi ya Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani.
0 toamaon yako: