Duru za Mahakama nchini Sweden zimeeleza kuwa, raia mmoja wa Rwanda na mwingine Mswidi mwenye asili ya Kinyarwanda leo wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya kimbari yaliyofanyika mwaka 1994 nchini Rwanda.
Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Stockholm amesema kuwa, washukiwa hao wawili wametiwa mbaroni na wanaendelea kusailiwa kutokana na kukabiliwa na tuhuma za kuhusika na mauaji ya kimbari. Taarifa zaidi zinasema kuwa, watuhumiwa hao wamepinga kuhusika na jinai hizo.
Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Stockholm amesema kuwa, mtuhumiwa mmoja ni raia wa Rwanda na amekuwa akiishi nchini Sweden kisheria na mwingine ni Mswidi mwenye asili ya Rwanda.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, mwezi Juni mwaka huu Mahakama ya Rufaa nchini humo iliidhinisha hukumu ya kifungo cha maisha jela dhidi ya Stanislas Mbanenande raia wa Rwanda, ambaye alipatikana na makosa ya kushiriki kwenye mauaji ya kimbari yaliyopelekea watu wasiopungua 800,000 kuuawa katika kipindi cha miezi mitatu.
0 toamaon yako: