Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, uzoefu wa miaka minane ya vita vya kujihami kutakatifu umethibitisha kwamba licha ya kuwepo mashinikizo makubwa na uhaba wa fedha na matatizo mengine mengi, lakini inawezekana kukabiliana vilivyo na mabeberu na kuvunja ndoto zao zisizo na maana kwa kutegemea nia ya kweli na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu.
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo Jumatano wakati alipoonana na makamanda wa ngazi za juu wa kijeshi na kukitaja kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu kwamba kilikuwa ni nembo ya heshima kwa taifa la Iran.
Amesisitiza kuwa, kusimama kidete taifa la Iran katika vita hivyo vya miaka minane kulizidi kuimarisha nia na imani ya shakhsia muhimu na akili za wanaharakati wa nchi za Kiislamu na zisizo za Kiislamu wanaoamini kwamba inawezekana kujihami hata kwa mikono mitupu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekitaja kipindi cha kujihami kutakatifu kuwa ni suala muhimu na lenye vipengee tofauti na kuongeza kwamba, kumbukumbu, matukio na masomo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minane ya kujihami kutakatifu ni utamaduni wa kuendelea na ni chemchemu ambayo kama itaeleweka na kutumiwa vyema, bila ya shaka yoyote itakuwa ni kwa manufaa ya taifa la Iran na mustakbali bora wa nchi.
Aidha ameashiria hatua ya madola ya Mashariki na Magharibi na vibaraka wao katika eneo hili ya kuunda kambi kubwa ya kijeshi kwa ajili ya kukabiliana na Iran wakati wa vita hivyo na kuongeza kuwa, lengo la kambi hiyo lilikuwa ni kuudhoofisha na kuuondolea itibari mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuutumbukiza kwenye matatizo ya ndani na hatimaye kuandaa mazingira ya kuanguka Jamhuri ya Kiislamu, lakini mfumo huu wa Kiislamu na taifa la Iran lilikabiliana vilivyo na kambi hiyo na kutoka kwa heshima katika medani ya mapambano licha ya kwamba wakati huo Iran ilikuwa na matatizo mengi ukiwemo uchache wa suhula na zana za kijeshi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ameashiria gharama zilizosababishwa na vita hivyo hasa mashahidi watukufu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa, pamoja na kwamba gharama za kimaada na kimaanawi za vita hivyo vya kulazimishwa zilikuwa kubwa, lakini matunda yake kwa taifa la Iran yalikuwa makubwa mno ikilinganishwa na gharama hizo.
0 toamaon yako: