Ulimwengu wa Kiislamu Fursa na Changamoto (3)
Sehemu ya tatu ya makala ya Ulimwengu wa Kiislamu, Fursa na Changamoto
itaendelea kutupia jicho baadhi ya changamoto na sababu zilizozikwamisha
nchi za Kiislamu na kuzifanya zisiwe na mitazamo na misimamo mimoja.
Miongoni
wa matatizo makubwa yanayoukabili ulimwengu wa Kiislamu hii leo, ni
kutokuweko umoja, mshikamano na mitazamo ya pamoja ya kisiasa baina ya
nchi za Kiislamu. Kwa hakika suala hilo huenda likawa limesababishwa na
sababu mbalimbali.
Mosi ni kuwa, serikali nyingi zinazotawala katika
nchi za Kiislamu zinaamini kwamba, kwa kuzingatia hali ya kiuchumi na
kiteknolojia, na muhimu kuliko yote uwezo wa kijeshi wa Magharibi,
maslahi na manufaa yao yanaweza tu kudhaminiwa kwa serikali zao kuwa na
uhusiano na nchi za Magharibi. Katika upande mwingine, hali ya
kulegalega kisiasa na matatizo ya vita vya ndani pamoja na vitisho vya
kieneo katika baadhi ya nchi ni mambo yaliyoziongezea nchi hizo hasa
watawala wake woga na kuhisi kutokuwa na amani.
Ni kutokana na
sababu hiyo ndio maana nchi hizo zikaamua kuwatumia Wamagharibi ili
kulinda nafasi zao, kiasi kwamba, baadhi ya nchi hizo zinayategemea
madola hayo katika kukidhi mahitaji ya chakula, silaha na hata usalama
wao. Leo hii nchi zinazoendelea zimekuwa zikitenga bajeti kubwa ya
kununulia silaha na zana za kivita kutoka kwa madola makubwa.
Na
ndio maana nchi za Mashariki ya Kati leo hii zikahesabiwa kuwa wanunuzi
wakubwa wa silaha duniani. Katika kipindi cha vita vya kichokozi vya
Iraq dhidi Iran na Kuwait, takribani dola bilioni 200 za Kimarekani za
akiba ya fedha za kigeni za nchi za eneo kama Iraq, Kuwait na Saudi
Arabia zilitumika kununulia silaha na zana za kivita kutoka kwa madola
ya Magharibi. Hofu ya mashinikizo ya nchi zenye nguvu na satua za madola
ya Magharibi na vitisho vyao vya kuziwekea nchi nyingine vikwazo vya
kiuchumi na kifedha ni mambo mengine yaliyozifanya nchi za Kiislamu
kutokuwa na hamu ya kuanzisha uhusiano baina yao na kutiliana saini
mikataba ya ushirikiano. Hussein Abul Fadhli mwandishi wa kitabu cha
Mitazamo ya Pamoja ya Ulimwengu wa Kiislamu anaamini kwamba, rasilimali
ya kimaanawi huifanya nchi fulani kuwa na nguvu kazi yenye fikra
madhubuti. Ikiwa wasomi na wanafikra watalelewa katika misingi ya
kitamaduni na ustaarabu wao asilia na wakafanya shughuli zao katika
fremu ya matukufu na itikadi zao, hapana shaka kuwa, watakuwa wenzo na
nguzo muhimu ya desturi na utamaduni huo. Lakini kinyume na hivyo,
endapo watajitenga na kuwa mbali na utamaduni, mila na desturi za taifa
lao na wakawa na matatizo ya utambulisho wao ni wazi kuwa, watapelekea
jamii yao nayo kukumbwa na matatizo hayo.
Tukichunguza nafasi na
mchango wa wanafikra waliolelewa katika mifumo ya kisekula katika
kufungamana nchi zinazoendelea na Magharibi, tunaupata kuwa nao si
mdogo. Wasomi hao wa Magharibi bila kwanza ya kuwa na uelewa sahihi wa
mapungufu na kasoro pamoja mazuri na mabaya ya ustaarabu wa Magharibi
wamekuwa wakifuata kibubusa mifumo ya maisha ya Magharibi na kuifanya
mifumo hiyo kuwa, kioo na kiigizo chao katika ufumbuzi wa matatizo yao.
Natija
ya kuiga na kufuata mfumo huo ni kushindwa na kutokuwa na utambulisho
huru. Mbali na matatizo ya ndani, tukitazama kwa makini tunaona kuwa,
kuna matatizo na sababu za nje pia zilizopelekea nchi za Kiislamu kubaki
nyuma katika masuala mbalimbali. Ukoloni wa moja kwa moja na usikokuwa
wa moja kwa moja katika jamii za Kiislamu ulikuwa na nafasi muhimu
katika kudhoofisha imani na tamaduni za Kiislamu.
Kuenea kwa mbegu
za chuki baina ya kaumu na jamii mbalimbali za Kiislamu ni sababu
nyingine iliyopelekea mori, moyo wa izzah na ile hali ya kupigania
kujitawala na kujiamulia mambo ipungue katika nyoyo za jamii za wananchi
hao. Waislamu ambao kwa makumi ya karne walikuwa waking'ara katika
elimu mbalimbali, hivi sasa wanaonekana kubaki nyuma kutokana na njama
za wakoloni na hali hiyo inazidi kushuhudiwa kila uchao kutokana na nchi
za Kiislamu kuwa tegemezi kwa Wamagharibi. Leo hii kwa kuanzishwa hiki
kinachoitwa utandawazi inaonekana kwamba, madola yenye nguvu duniani,
yanataka kuutawala na kuudhibiti zaidi ulimwengu lakini kwa mbinu na
mtindo mpya. Katika mazingira kama hayo, hapana shaka kuwa, nchi za
ulimwengu wa tatu zikwemo nchi za Kiislamu zinakabiliwa na changamoto
nyingi.
Kwa mfano, kuwepo kwa utandawazi wa kiutamaduni kutaishia
kwa kutawaliwa nchi zote na utamaduni wa Magharibi ambao ni wa mambo na
masuala ya kimaada na isirafu katika matumizi. Hasa kwa kuzingatia
kwamba, utamaduni wa Magharibi ni wa kutangaza na kueneza vitu vya anasa
na vinavyoonekana kuwa ni vya kisasa katika kila pembe ya dunia. Na
hasa kwa kutilia maanani kuwa, nembo na vielelezo vya utamaduni wa
Magharibi kama vile sinema, intaneti, video, matangazo ya mitindo ya
mavazi ambazo vimetawala kwenye mtandao wa vyombo vya mawasiliano
duniani, hazitoi fursa ya uwiano wa kubadilishana utamaduni baina ya
ulimwengu wa Magharibi na nchi nyingine.
Katika uwanja huo, baadhi
ya wakosoaji wa utandawazi wanasema kuwa, mwenendo huo ni mtindo mpya wa
ubeberu wa kiutamaduni. Edward Said mhadhiri wa Vyuo Vikuu nchini
Marekani mwenye asili ya Palestina anaamini kwamba, Wamagharibi kwa
kutumia satua kwa mara nyingine tena wanafanya njama za kuukoloni
kiutamaduni ulimwengu wakitumia utamaduni wao. Makala zetu zijazo
zitaanza kuchunguza njia za kujiondoa na kujikwamua katika matatizo
hayo. Kwa leo tunaishia hapa. Wasalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh
Ulimwengu wa Kiislamu Fursa na Changamoto (4)
Miongoni mwa sifa za ubeberu wa kiutamaduni ni kueneza thamani za mfumo
wa ubeberu kama vile namna ya matumizi, mavazi, uhusiano wa kijinsia,
haki za binadamu na usekulari au mfumo wa kukana nafasi ya dini katika
mfumo wa kisiasa. Kwa utaratibu huo, utandawazi unatoa utamabulisho mpya
katika uwanja wa utamaduni, ambao kimsingi unaambatana na kupotea na
kuangamia kwa utamaduni na ustaarabu asili wa nchi husika. Jamii za
Kiislamu nazo zimekuwa wahanga wa kadhia hiyo. Katika uwanja wa
kiuchumi, utandawazi pia unaweza kudhoofisha muundo wa ndani wa kiuchumi
wa mataifa ya Kiislamu na kupelekea kuporwa maliasili na utajiri wa
nchi hizo. Uchumi wa asili wa jamii hizo unaweza kukabiliwa na matatizo
makubwa na ya kimsingi ya utandawazi kupitia mashirika ya kimataifa na
taasisi kama Shirika la Biashara Duniani WTO na mengineyo.
Hasa kwa
kuzingatia kwamba, nchi hizo hazina suhula za kutosha na muundo wao wa
kiuchumi hauna uwezo wa kushindana na madola makubwa na yenye nguvu
kiuchumi duniani. Ama kwa upande wa kisiasa, kutokea mihimili mipya
yenye nguvu duniani kama vile mashirika na makundi ya kimataifa hasa
vyombo vya mawasiliano kama vile Intaneti, satalaiti na mitandao mingi
ya vyombo vya habari kumepelekea kulegalega kwa mipaka ya kitaifa. Cha
kusikitisha zaidi ni kuwa, asasi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa
wakati mwingine zimekuwa zikitumiwa kama wenzo wa madola makubwa kwa
ajili ya kutekeleza matakwa ya madola hayo.
Ibn Khaldun alimu na
mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu, anazungumzia sababu muhimu za maendeleo
katika jamii akisema, mambo mawili ni muhimu kwa ajili ya maendeleo.
Mosi, kiongozi muadilifu na pili ni kuungana kwa jamii au kwa taifa na
taifa jingine. Kuhusiana na suala hilo, leo hii baadhi ya wanafikra
wamefikia natija hii kwamba, kutokuwepo tawala za kiadilifu na
kukosekana moyo wa kuwaunganisha pamoja watu na kushirikiana pamoja ni
miongoni mwa sababu zilizozifanya nchi nyingi kubaki nyuma kimaendeleo.
Mazingira
yanayotawala leo hii ulimwenguni yanazilazimisha tawala kuliko kipindi
kingine chochote kile kuwashirikisha wananchi katika nyanja mbalimbali
ili ziweze kukabiliana au kutatua matatizo yanayozikabili. Kwa hakika
suala hilo ni nguzo muhimu ya kuzihalalisha tawala zilizoko katika nchi
mbalimbali ulimwenguni zikwemo nchi za Kiislamu.
Katika kipindi cha
miongo mitatu iliyopita, kumetokea matukio tofauti katika masuala
mbalimbali ambayo yamepelekea mlingano wa dunia kukumbwa na mabadiliko
makubwa. Kutokea mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, kusambaratika Umoja
wa Kisovieti, maendeleo makubwa yaliyopatikana katika uwanja wa
teknolojia na mawasiliano, ni miongoni mwa matukio ambayo yaliibadilisha
mno sura ya miaka ya mwishoni mwa karne ya 20.
Mapinduzi ya
Kiislamu ya Iran si tu kwamba, yalivuruga mahesabu ya madola ya Maghribi
katika eneo muhimu na la kiistratejia la Mashariki ya Kati, bali
mapinduzi hayo, adhimu yalikuwa na taathira kubwa kwa Waislamu
ulimwenguni kote. Miongoni mwa mabadiliko makubwa yaliyotokea katika
ulimwengu wa Kiislamu ni kutokea ufahamu na mwamko mkubwa wa wananchi.
Dr Hasan Rahimpour Azghadi, mtafiti wa Kiirani na mhadhiri wa chuo kikuu
anasema hivi kuhusiana na suala hilo: "Ufahamu na mwamko huo ambao ni
mwamko wa kidini, huenda karne moja iliyopita, ulikuwako katika kundi
dogo la wanafikra waliobobea kwenye ulimwengu wa Kiislamu. Lakini leo
hii mwamko huo unaonekana kuenea katika uma wote wa Kiislamu." Mtafiti
huyo wa Kiirani anaendelea kusema, "mwamko huo hasa katika kipindi cha
miaka 100 ya mwisho, umetokea baada ya karne kadhaa za kusalimu amri na
kujilegeza mbele ya ukoloni. Leo hii Waislamu wanatambua vyema kwamba,
sababu kuu ya kubaki kwao nyuma kiuchumi na kielimu na mifarakano na
migawanyiko iliyopo katika ulimwengu wa Kiislamu imetokana na Waislamu
kuwa mbali na mafunzo aali ya dini yao tukufu." Mwisho wa kunukuu.
Kutokana
na Waislamu kubadilika kuhusiana na matukio mbalimbali yanayowazunguka,
leo hii tunaona kuwa, katika ulimwengu wa Kiislamu kumekuwa
kukipendekezwa masuala kama ya umoja wa uma wa Kiislamu, kuundwa asasi
na jumuia za Kiislamu, ustawi wa kieilmu ambao kimsingi ni maendeleo na
ustawi katika uga wa fikra za walimwengu kwenye ulimwengu wa Kiislamu.
Suala
hilo limeyafanya madola ya Kiislamu kufahamu kwamba, leo hii matakwa ya
wananchi yana daraja ya juu zaidi kuliko mahitaji yao ya kila siku.
Hata wito wa mabadiliko ya kisiasa wa Magharibi au mapendekezo yao ya
demokrasia ulimwenguni hasa katika Mashariki ya Kati, ni masuala
yanayotokana na kudhihiri mabadiliko ya kifikra katika ulimwengu wa
Kiislamu. Hapana shaka kuwa, madola ya Magharibi kamwe hayazingatii
matakwa ya wananchi wa mataifa ya Kiislamu, bali yanajaribu kuzipotosha
fikra za waliowengi kwa kutanguliza mbele matakwa ya wananchi hao, kumbe
wanataka kufikia malengo yao haramu ili kwa njia hiyo waweze kudhibiti
hali ya mambo katika eneo na matukio ya ulimwengu wa Kiislamu.
Mashambulio ya Marekani na washirika wake dhidi ya Iraq yalifanywa kwa
kisingizio cha kuwaletea demokrasia wananchi wa nchi hiyo, lakini
wavamizi hao hawajawaletea chochote wananchi hao ghairi ya machafuko na
mauaji. Hii ni katika hali ambayo, Marekani ilikuwa ikimuunga mkono
kijeshi, kisiasa na kiuchumi dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein.
Mpenzi
msomaji na mfuatiliaji wa makala hizi za Ulimwengu wa Kiislamu, Fursa
na Changamoto, sehemu ya nne ya makala yetu inaishia hapa. Sehemu ijayo
ya makala hii mbali na kuzungumzia umuhimu wa kuweko kambi moja au
mtazamo mmoja katika ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na
changamoto unazozikabili, itatupia jicho pia uwezo na suhula zilizoko
katika nchi za Kiislamu. Wassaalam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh.
Ulimwengu wa Kiislamu Fursa na Changamoto (5)
Miongoni mwa maudhui ambazo katika kipindi cha miongo miwili iliyopita
zimekuwa zikijadiliwa na hasa baada ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti
katika uga wa mfumo wa kimataifa, ni suala la kuwa na kambi yenye
mitazamo ya pamoja.
Nchi ambazo katika zama hizo zilijiunga na kambi
zenye nguvu ili kulinda na kuhifadhi maslahi yao, leo hii kwa kuanzisha
taasisi kama Umoja wa Ulaya, Muungano wa Nchi za Mashariki ya Asia ya
Kusini ASEAN na kadhalika, zinafanya jitihada za kuimarisha nguvu, satua
na nafasi zao kimataifa. Hata hivyo, cha kusikitisha ni kuwa, nchi za
Kiislamu licha ya kuwa katika eneo muhimu kijiografia na kistratejia na
kuwa na suhula nyingi ukiwemo utajiri wa nishati ya mafuta,
hazijastafidi ipasavyo na suhula hizo. Kwa mfano katika hali ambayo,
nishati ni chanzo kikubwa kabisa cha pato la fedha za kigeni duniani na
asilimia 75 ya akiba ya mafuta na gesi duniani, inapatikana katika nchi
za Kiislamu; lakini cha kusikitisha ni kwamba, nchi hizo hazijastafidi
kwa njia sahihi na utajiri huo.
Leo hii kwa kuzingatia mazingira
yanayotawala ulimwenguni, udharura wa kuweko kambi yenye misimamo mimoja
na ambayo itashirikiana katika ulimwengu wa Kiislamu kuhusiana na
masuala mbalimbali ulimwenguni unahisika zaidi kuliko kipindi kingine
chochote kile. Hasa kwa kuzingatia kwamba, madola ya Magharibi
yamezidisha hujuma, njama na propaganda zao dhidi ya nchi za Kiislamu.
Hapana
shaka kuwa, kudhalilishwa na kuvunjiwa heshima matukufu na itikadi za
Kiislamu katika vyombo vya Magharibi na mashambulio ya kijeshi ya
Marekani na kisha kuendelea kuweko kijeshi Washington katika ardhi za
Kiislamu za Afghanistan na Iraq au mashambulio ya kijeshi ya utawala
dhalimu wa Israel dhidi ya Lebanon na jinai za utawala huo kwa wananchi
madhulumu wa Palestina ni mifano ya wazi ya njama za hujuma za dhahiri
dhidi ya ulimwengu wa Kiislamu. Ni kwa kuzingatia hayo ndio maana leo
hii suala la umoja, mshikamano na nchi za Kiislamu kuwa na kambi na
mitazamo ya pamoja baina yao yakawa mambo ambayo yana umuhimu mkubwa
kuliko kipindi kingine chochote kile. Ni jambo lisilo na shaka kuwa,
kuna uwanja na mazingira mazuri kwa nchi za Kiislamu kuwa na kambi moja
na yenye misimamo na mitazamo mimoja katika nyanja za kiuchumi, kisiasa
na kielimu.
Miongo kadhaa iliyopita, istilahi ya mtazamo mmoja
ilikuwa ikitumiwa mno katika matini za kisiasa. Baada ya Vita Vikuu vya
Pili vya Dunia istilahi ya mtazamo wa pamoja ilianza kuzingatiwa mno na
nchi mbalimbali duniani. Katika uwanja huo, nchi za Ulaya Magharibi
zililipa kipaumbele suala la mtazamo wa pamoja wa kieneo katika siasa na
mipango yao. Soko la pamoja na kubadilishwa kwake kuwa Umoja wa Ulaya
ni natija ya jitihada za nchi za Ulaya katika uwanja huo.
Kumalizika
vita baridi na kusambaratika Umoja wa Sovieti kulipelekea kutokea
mabadiliko makubwa na muhimu katika muundo wa mfumo wa kimataifa na
muhimu kuliko yote ni mabadiliko ya kambi mbili na ni katika kipindi
hicho pia ambapo Marekani ilianza jitihada za kuanzisha mfumo wa dola
moja lenye nguvu.
Leo hii kutokana na hali mpya ya hivi sasa, nchi
nyingi zinazingatia suala la mtazamo mmoja wa kieneo au kambi moja ya
kisiasa, kiuchumi na kadhalika ya kieneo kuwa, moja ya njia bora za
kukabiliana na mfumo wa dola moja lenye nguvu wa Marekani. Kumejitokeza
mitazamo mbalimbali au kambi tofauti za kieneo katika sekta mbalimbali.
Mtazamo wa pamoja katika uhusiano wa kimataifa ni nadharia ambayo nchi
zinafanya jitihada za kushirikiana katika masuala mbalimbali kwa mujibu
wa maslahi yao ya pamoja. Hadi sasa mikataba kadhaa imetiwa saini katika
fremu ya ushirikiano wa kiuchumi na kisiasa. Mazingira yanayotawala leo
hii duniani kwa upande mmoja na hali ya mambo katika ulimwengu wa
Kiislamu kwa upande wa pili, ni mambo yanayozifanya nchi za Kiislamu
kuchukua hatua za kushirkiana zaidi. Nchi za Kiislamu zina mambo mengi
yanayoshabiana kama vile dini, utamaduni, na kuwa na mipaka ya pamoja,
na kuwa na suhula na fursa zinazofanana za kiuchumi, ni mambo ambayo kwa
hakika yanaziandalia uwanja mzuri nchi hizo, wa kuwa na mitazamo mimoja
katika masuala mbalimbali, hasa kwa kuzingatia kuongezeka
hivi sasa
njama za maadui wa Uislamu katika pembe mbalimbali duniani. Pendekezo la
kuweko na mtazamo mmoja na umoja katika istilahi za kisiasa kwenye
ulimwengu wa Kiislamu linarejea nyuma kabla ya karne moja. Kwa hakika
kuna mambo na sababu nyingi za ndani na za nje zilizowafanya wanaopenda
umoja katika ulimwengu wa Kiislamu kuona kuwa kuna udharura wa kuweko na
mtazamo na msimamo mmoja. Vitu kama dini na utamaduni wa pamoja na
tajiriba ya nchi zote za Kiislamu zilioipata kutokana na kukoloniwa,
hasa hatua ya Wazayuni ya kuzikalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina,
bila shaka ni mazingira ya kiutamaduni na kisiasa yanayoziandalia uwanja
nchi za Kiislamu kuwa na mtazamo mmoja.
Kwa upande wa nafasi ya
kijiografia, kiistratejia na uwezo wa kiuchumi, nchi za Kiislamu zina
mazingira mazuri na mwafaka ya kushirikiana na kuwa na misimamo ya
pamoja. Licha ya kuwa na mambo mengi yanayoziandalia mazingira mazuri
nchi za Kiislamu ya kushirikiana na kuwa na mitazamo ya pamoja, lakini
watafiti wa Ulimwengu wa Kiislamu wanasema kuwa, Uislamu na utamaduni
mkongwe wa nchi hizo ni mambo muhimu kabisa yanayoziandalia uwanja nchi
hizo kushirikiana na kuwa na mitazamo pamoja na malengo mamoja.
0 toamaon yako: