Mtume Muhammad SAW Nuru ya Uongofu (1)

Kisa cha Mwaka wa Tembo kinaanzia pale Abraha mfalme wa Habasha na Yemen, alipowaona Waarabu wakihiji Makka na ibada hii ya Hijja ikaufanya mji wa Makka kuwa kitovu cha biashara.
Mfalme Abraha alidhamiria kuihamisha ibada ya Hijja kutoka Makka na kuipeleka katika milki ya hi maya yake ya Yemen. Ili kutekeleza mkakati wake huu alijenga kanisa kubwa sana na kulipamba kwa mapambo ya fakhari ili watu wavutike na kuja kufanya ibada ya Hijja hapo. Baada ya ujenzi huo, akawaamrisha watu waje kuhiji hapo, amri hii ikawa nzito kwa Waarabu kuitekeleza na hawakuiridhia.
Ili kuonyesha chuki yao dhidi ya amri hiyo, alitoka mtu mmoja wa kabila la Kinanah na kufanya haja kubwa ndani ya kanisa hilo. Kitendo hiki cha kulichafua kanisa kilimkasirisha sana Mfalme Abraha, hasa baada ya kugundua kwamba, mhusika wa kitendo hicho alikuwa mtu kutokea pande za Makka.
Aliandaa jeshi kubwa lililokuwa limesheheni tembo wengi ili kwenda kuivunja al-Kaaba na yeye mwenyewe alikuwa amempanda tembo mkubwa sana kuliko wote. Waarabu wa Makka waliliogopa sana jeshi lile.
Jeshi la Abraha lilipofika katika viunga vya mji wa Makka likawakuta ngamia, kondoo na mbuzi wa watu wa Makka na wengine walikuwa ni milki ya babu yake Mtume Mzee Abdul-Muttalib, Abraha akachukua mifugo ile yote. Mzee Abdul-Muttalib kiongozi wa kabila la Kureish, mtumishi wa al-Kaaba na mtawala wa Makka akamuendea Abraha na kumtaka amrejeshee mifugo yake aliowachukua. Abraha alimshangaa sana Mzee Abdul - Muttalib na kumwambia: "Mimi nilidhani kwamba umekuja kuniomba nisiivunje al-Kaaba, kumbe umekuja kunitaka nikurudishie wanyama wako!" Mzee Abdul - Muttalib akamjibu: "Mimi wa kwangu ni hawa wanyama, ama hii nyumba yupo mwenyewe (Mwenyezi Mungu) atayeihami."
Kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu alilishushia jeshi la Abraha jeshi la ndege lililodondosha mawe. Mtu yeyote ailiyepatwa na jiwe alisagikasagika yeye na tembo wake na kuwa kama majani yaliyoliwa na kutapikwa kama tunavyosoma ndani ya Qur'ani. Tokea hapo Waarabu wakawa wanaitaja kalenda yao kwa kuinasibisha na tukio hili kubwa na hii ndio maana tunasema Bwana Mtume alizaliwa katika Mwaka wa Tembo. Mwenyezi Mungu anaeleze kisa hicho katika Qur'ani kwa kusema: "Kwani hukuona jinsi Mola wako Mlezi alivyowatenda wale wenye tembo? Kwani hakujaalia vitimbi vyao kuharibika? Na akawapelekea ndege makundi kwa makundi, Wakiwatupia mawe ya udongo wa Motoni. Akawafanya kama majani yaliyoliwa." Al-Fiil 105:1-5
Adhama ya Kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW)
Maulidi (kuzaliwa) ya Mtume Mtukufu si tukio la kihistoria tu, bali lilikuwa tukio muhimu mno la kuainisha hatima ya mwanadamu. Matukio yaliyoambatana na maulidi hayo matakatifu kama ilivyoripotiwa katika historia yenyewe yalikuwa ni ishara ya wazi iliyobainisha maana halisi na uhakika wa mwana aliyezaliwa.
Imenukuliwa kwamba, katika zile sekunde za kuzaliwa Mtume Mtukufu (rehema za Allah ziwe juu yake na Aali zake) nembo za kufru na shirki zilikumbwa na matatizo katika sehemu mbalimbali duniani. Moto wa Fars (Uajemi) ambao ulikuwa unawaka kwa muda wa miaka elfu bila ya kuzimika, ulizimika siku hiyo ya kuzaliwa Mtume. Masanamu yaliyokuweko kwenye maabadi na masinagogi mbalimbali yalianguka na kuwafanya watawa na wahudumu wa masinagogi na maabadi hayo wachanganyikiwe na kushindwa kujua nini kinatokea! Matukio hayo yaliyosadifiana na lahdha ya kuzaliwa Mtume yalikuwa ishara ya kuporomoka misingi ya shirki na ukafiri.
Mtume Muhammad SAW alizaliwa huko Makka katika Bara Arabu. Baba yake ni Abdullah mwana wa Abdul Muttalib mwana wa Hashim. Mama yake ni Bi. Amina Bint Wahab. Babu yake Abdul Muttalib alikuwa na wake wengine watano, na Abdullah na Abu Talib walitoka katika tumbo moja. Alizaliwa akiwa yatima, kwani baba yake yaani Abdullah alifariki dunia miezi mitatu kabla ya kuzaliwa Mtume SAW.
Katika upande mwingine kasri la wafalme majabari na washirikina wa wakati huo wa
Iran lilikumbwa na mtetemeko mkubwa na mabaraza ya Kasri la Madain - yale mabaraza 14 - yaliporomoka. Hiyo ilikuwa ni ishara nyingine ya kimaanawi iliyothibitisha kuwa kulitokea jambo kubwa na lisilo la kawaida na kwamba, maulidi na kuzaliwa Bwana Mtume ulikuwa ni utangulizi wa mazingira ya kupambana na ukafiri na mataghuti duniani. Ule ni upande wa umaanawi na uongofu wa moyo na fikra kwa mwanadamu na huu ni upande wa miongozo ya kijamii na kivitendo kwa ajili ya matabaka mbalimbali ya mwanaadamu. Kupambana na dhulma, kupambana na utaghuti, kupambana na utawala usio wa haki wa madhalimu wanaokandamiza watu, hizo zilikuwa ni ishara za kimaanawi na adhama ya kuzaliwa Mtume.
Maulidi na kuzaliwa Bwana Mtume SAW kwa kila Muislamu ni nukta na jambo muhimu mno katika historia. Kwani kuzaliwa mtukufu huyo ndiko baadaye kulikopelekea kutokea harakati kubwa isiyo na kifani katika historia ya mwanadamu. Kila fadhila, neema na baraka zilizoko katika ulimwengu huu chanzo chake ni kubaathiwa Mtume na kusimamishwa misingi ya tabia njema kwa baraka za kuweko kwake. Kila Muislamu anatambua kwamba, hakuna nukta na jambo bora la kuukutanisha pamoja umma wa Kiislamu ghairi ya itikadi na imani yao kwa Mtume wa Uislamu. Wafuasi wa madhehebu mbalimbali huweka kando hitilafu zao ndogo ndogo na kuafikiana kutokana na baraka za kuweko Mtume wao mmoja. Kwani Waislamu wote wanampenda Mtume na yeye kwa hakika amekuwa mhimili na nguzo imara na madhubuti ya umma wa Kiislamu katika kipindi chote cha historia. Basi ni kwa kuzingatia hilo ndio maana tunasema kuwa, maulidi na kuzaliwa Mtume SAW ni muhimu kwetu sote.
Kuzaliwa Mtume (S.A.W) Tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal kabla ya Hijra kwa mujibu wa riwaya nyenye nguvu zaidi, au tarehe 12 Mfunguo Sita kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, alizaliwa shakhsia mkubwa na aliyetakasika na ulimwengu ukapata fakhari kubwa kwa kuzaliwa shakhsia huyo. Mtu huyo alikuwa si mwingine bali ni Mtume Muhammad (SAW).
Baba yake ni Abdullah mwana wa Abdul-Muttalib mwana wa Hashim. Mama yake Mtume Muhammad (SAW) ni Amina Bint Wahab. Babu yake Abdul-Muttalib alikuwa na wake wengine watano, na Abdullah na Abu Talib walitoka katika tumbo moja. Alizawa yatima, kwani baba yake, yaani Abdullah, alifariki dunia miezi mitatu kabla ya kuzaliwa Mtume SAW.
Mtume Muhammad SAW alizaliwa huko Makka katika Bara Arabu katika kipindi ambacho wanadamu walikuwa wamezama katika kuabudu miungu bandia, ujinga na ukatili wa hali ya juu. Akiwa katika kipindi cha utotoni, watu wa karibu yake walitambua kwamba, Muhammad angekuwa mtu mashuhuri na mwenye kuheshimika sana. Hii ilitokana na haiba na nuru aliyokuwa nayo kijana huyo mdogo.
Kuzaliwa kwa Muhammad kulibadilisha simanzi iliyokuwa imetawala jamii hiyo na kuwa na furaha isiyo na kifani, na hakuna aliyekuwa amefurahi zaidi kuliko mama yake yaani Bi Amina na babu yake yaani Abdul-Muttalib ambao walikuwa wameshtushwa mno na kifo cha ghafla cha Abdullah (baba yake Mtume).
Kuzaliwa kwa Mtume kuliambatana na bashasha na furaha katika nyumba yake na kuifanya nyumba hiyo ianze kipindi kingine.
Malezi ya Mtume (S.A.W)
Katika zama hizo ilikuwa ni ada na desturi kwamba, watoto wa jamii yenye kuheshimika kwa kawaida walikuwa wakikabidhiwa kwa mlezi mwenye afya na nguvu, ambaye angemfunza tabia na adabu njema. Mtoto Muhammad aliwekwa chini ya usimamizi na uangalizi wa Halima bint Saadiya. Baada ya miaka mitano Bi Halima alimrejesha Muhammad kwa mama na babu yake.
Kila mtu alikuwa na furaha isiyo kifani wakati mtoto huyo alipoanza kukua akiwa mwenye furaha, mwerevu na mwenye akili na busara, kinyume kabisa na watoto wengine wa rika lake. Tangu awali Muhammad alipendwa mno na watu kutokana na haiba, shakhsia na mwenendo wake mzuri. Hali hiyo ilimfanya mtoto Muhammad apendwe na kila mtu kwani alikuwa akivutia kisura na kitabia. Tabia njema pamoja na uaminifu wake vilimfanya apewe lakabu ya Mkweli na Mwaminifu.
Mama na Babu wa Mtume Wafariki
Alipofikisha umri wa miaka sita, mama yake alimpeleka Muhammad huko Yathrib ili akatembelee ndugu na jamaa zake. Ummu Aiman ambaye alikuwa yaya wao, alifuatana nao katika safari hiyo ya Yathrib. Akiwa katika mji wa Yathrib, kijana Muhammad alipata fursa ya kuliona na kulizuru kaburi la baba yake ambaye hakuwahi kumwona katika kipindi cha uhai wake. Kwa hakika ilikuwa ni huzuni kubwa kana kwamba, ndio
kwanza baba yake Muhammad alikuwa amefariki. Mama na mwana, yaani Muhammad na mama yake, walikuwa na huzuni na simanzi kubwa.
Baada ya kukaa kwa siku kadhaa mjini humo, walianza safari ya kurejea nyumbani, lakini Bi Amina yaani mama yake Mtume, alianza kuugua wakiwa njiani kurejea Makka. Msafara ulisimama ili kumuuguza, lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya kadiri siku zilivyokuwa zikisonga mbele. Maradhi yalimzidi na hatimaye akafunga kauli na kufariki dunia. Bi Amina alizikwa mahala panapojulikana kwa jina la Abwaa, eneo ambalo lipo baina ya Madina na Makka.
Mtume Muhammad (SAW) alikumbwa na majonzi na simanzi kubwa kutokana na kuondokewa na mama yake kipenzi. Wakati huo Muhammad alikuwa na umri wa miaka sita tu. Hivyo Muhammad akiwa na umri huo mdogo, alikuwa tayari ameondokewa na wazazi wake wawili (baba na mama) na kubakia yatima.
Abu Talib Achukua Jukumu la Kumlea Mtume
Kufariki dunia Bi Amina bint Wahab ulikuwa mwanzo wa kipindi kingine kipya cha maisha ya Muhammad tena akiwa bado kijana mdogo wa miaka sita, kipindi ambacho bado mtoto huyo alikuwa akihitajia mapenzi ya baba na mama pamoja na malezi yao. Kabla ya kufariki dunia, Abdul-Muttalib alimuagiza mwanae Abu Talib, kuhakikisha kwamba, anachukua jukumu la kumlea mjukuu wake huyo.
Hivyo Abu Talib alichukua jukumu la kumlea Muhammad na kuishi naye kama watoto wake wengine na kuhakikisha kwamba, hahisi hali ya uyatima na upweke wa kuondokewa na wazazi wake. Mke wa Abu Talib yaani Fatima bint Assad ambaye ndie mama wa Imam Ali bin Abi Twalib, alimlea Muhammad kwa mapenzi makubwa kama mwanawe wa kuzaa. Hali hiyo ilimfanya Muhammad asahau pengo la kufiwa na wazazi wake. Watu wote ndani ya nyumba walimpenda sana Muhammad hasa kutokana na uhodari, tabia, mienendo yake mizuri na maadili mema ambayo yalikuwa yakimvutia na kumfurahisha kila mtu.
Ulimwengu wa Kiislamu Fursa na Changamoto (1)
Kwa jina Allah Mwingi wa rehema Mwenye Kurehemu
Assalaam
Alaykum wasomaji na wapenzi wa Redio Tehran Idhaa ya Kiswahili Sauti ya
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Huu ni mfululizo wa makala za Ulimwengu wa
Kiislamu, Fursa na Changamoto ambao utatupia jicho na kuchunguza fursa
pamoja na changamoto zinazoukabili Ulimwengu wa Kiislamu.Ulimwengu wa Kiislamu si jina geni katika fasihi, maandiko, istilahi za kisiasa na kiutamaduni na hata katika masikio ya walimwengu pia. Kabla ya neno Ulimwengu wa Kiislamu kubainisha hali ya eneo fulani kijiografia, linabeba maana na kuweka wazi utambulisho wa jamii fulani ya watu wapatao bilioni moja na nusu ambao wana mitazamo, dini, utamaduni,ustaarabu, mila na desturi zinazoshabihiana. Mbali na sifa maalumu ulionao ulimwengu wa Kiislamu kijiografia, ulimwengu huu una maliasili na utajiri mkubwa, utajiri ambao umeufanya kufahamika kuwa, eneo lenye utajiri mkubwa kabisa duniani. Sifa hiyo na suhula ulizonazo ndiyo zilizoufanya ulimwengu wa Kiislamu kwa karne kadhaa kuwa na nafasi muhimu katika uhusiano wa kimataifa. Hapana shaka kuwa, pana haja ya kuainishwa malengo na mipango madhubuti ambayo itasaidia kustafidi vizuri na suhula hizo na kwa njia sahihi na iliyo bora.
Katika mfululizo huu wa รข'Ulimwengu wa Kiislamu, Fursa na Changamoto'' tutazungumza na kujadili fursa na suhula zilizopo katika nchi za Kiislamu ambazo bila shaka kutumiwa kwake vyema kutaimarisha nafasi ya Waislamu katika nyanja mbali mbali ulimwenguni iwe ni kiuchumi au kisiasa na vile vile kuyaleta na kuyakurubisha pamoja mataifa ya Kiislamu na wafuasi wa dini hii tukufu. Aidha tutatupia jicho pia changamoto zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu zikiwemo za kiutamaduni, kiuchumi, kisiasa, kielimu na kadhalika.
Matukio ya hivi sasa ulimwenguni yamebainisha kwamba, madola ya kibeberu hayataki kuona ulimwengu wa Kiislamu ukiwa na nafasi muhimu katika matukio mbalimbali duniani. Madola yanayopenda kujitanua daima yanatafakari na kutaamali ni namna gani yataweza kuudhibiti ulimwengu wa Kiislamu. Ndio maana madola hayo yakawa hayako tayari kuukubali utamaduni asili na tajiri wa Kiislamu, hasa kutokana na kuwa, utamaduni huo si tegemezi wala hauigi tamaduni za mataifa au watu wengine. Masuala hayo na mengineyo, ndiyo yaliyoufanya Ulimwengu wa Kiislamu leo hii ukabiliwe na vitisho na migogoro ya kupandikizwa kuliko karne za nyuma; na hapana shaka kuwa, yote hayo yanatokana na njama za maadui wa Uislamu. Ili ulimwengu wa Kiislamu uinue nafasi na kiwango chake pamoja na kudiriki utambulisho wake halisi, pana haja ya kuweko mitazamo mipya, mwamko, kuwa macho pamoja na mipango imara na madhubuti. Ili tuwe na taswira ya mustakbali wa huko tuelekeako, kuna haja ya ulimwengu wa Kiislamu kufahamu nafasi yake halisi ya hivi sasa, suala ambalo litasaidia mno kufikiwa malengo muhimu na aali na yenye mafanikio makubwa. Kama tulivyoashiria mwanzoni mwa makala hii Ulimwengu wa Kiislamu ni jina ililopewa jamii ya Waislamu yenye idadi ya takribani watu bilioni moja na nusu ambao wanapatikana na kuishi katika nchi za Kiislamu na zisizo za Kiislamu. Kinachoifungamanisha pamoja jamii hiyo licha ya kuwa na makabila, lugha na rangi tofauti ni dini tukufu ya Kiislamu. Bara la Asia ndilo linaloongoza kwa kuwa na Waislamu wengi ambao idadi yao inakadiriwa kufikia bilioni moja. Barani Afrika kuna Waislamu wapatao milioni 391. Amma katika bara la Ulaya takwimu zinaonyesha kwamba, kuna Waislamu wapatao milioni 20 na wengine zaidi ya milioni 27 wanapatikana nchini Russia. Kadhalika kuna idadi nyingine ya Waislamu takribani milioni tisa huko Amerika ya Latini, Marekani na Canada.
Kuna baadhi ya mataifa na lugha ambazo zina nafasi muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu. Kwa mfano lugha za Kiarabu, Kifarsi na Kituruki zinahesabiwa kuwa lugha muhimu mno katika ulimwengu wa Kiislamu. Waaidha Waislamu wengi wanaopatikana katika nchi za Pakistan na India wanazungumza lugha ya Ki-Urdu. Karibu asilimia 14 ya idadi ya Waislamu katika Ulimwengu wa Kislamu wanapatikana katika nchi za Indonesia na Malaysia na wanazungumza lugha ya Kimalayu au Kimalay. Moja kati ya maeneo ya kiistratejia katika ulimwengu wa Kiislamu, ni eneo la Mashariki ya Kati ambayo ni njia fupi zaidi ambayo inayaunganisha mabara ya Asia na Ulaya. Lango bahari na vivuko muhimu vya kiistratejia kama vile Kanali ya Suez, Malango Bahari ya Jabal Twariq na Hormoz ni baadhi ya njia muhimu za mawasiliano ya baharini baina ya mabara mbalimbali, ambazo zinapatikana katika ulimwengu wa Kiislamu. Kuweko maliasili, nishati na utajiri wa madini na bidhaa mbalimbali za mazao ni baadhi tu ya mambo yanayouongezea umuhimu Ulimwengu wa Kiislamu na kuufanya uzingatiwe mno kimataifa. Kama inavyofahamika, mataifa ya Kiislamu yanaundwa na lugha na makabila mbalimbali. Katika nchi 19 za Kiislamu, asilimia kubwa ya wakazi wake ni Waarabu na Wasemiti. Hata hivyo, kuna watu wengine wa makabila ya wachache kama vile Waturuki katika nchi za Kiarabu kama vile Iraq na Syria. Katika nchi za Kiafrika ambazo wakazi wake ni Waarabu wanapatikana pia watu wa jamii ya Wabarbari.
Ulimwengu wa Kiislamu una jumla ya nchi 57 na nchi yenye wakazi wengi zaidi ni Indonesia na ile yenye wakazi wachache ni Maldives. Mbali na Afghanistan, Iraq na Palestina nchi zote za Kiislamu zimejikomboa kutoka katika makucha ya wakoloni na wavamizi. Mpenzi msomaji sina shaka utakuwa umefahamu japo kwa mukhtasari, jiografia ya kimakazi na kisiasa ya ulimwengu wa Kiislamu. Makala zetu zitakazofuata zitazungumzia kwa urefu nafasi ya nchi za Kiislamu katika masuala mbalimbali ulimwenguni.
0 toamaon yako: