Tanzania swahili radio

IQRA FM RADIO

IQRA FM RADIO
IQRA FM RADIO ELIMU NA MATENDO UIMARA WA RADIO IQRA UPO MIKONOMI MWAKO CHANGIA RADIO IQRA KWA MPESA 0762118805TIGO PESA 0658118804

Sunday, September 28

UISLAM 6-8

Posted by mkachu  |  Tagged as:

Ulimwengu wa Kiislamu Fursa na Changamoto (6) 

Katika kuutambulisha ulimwengu wa Kiislamu katika jiografia yake ya kisiasa tunaweza kuugawa ulimwengu huo katika sehemu kuu nne ambazo ni Katikati mwa Ulimwengu wa Kiislamu, Mashariki mwa Ulimwengu wa Kiislamu, Kaskazini mwa Afrika na Kaskazini mwa Ulimwengu wa Kiislamu.
Eneo la Mashariki ya Kati ambalo linalojulikana kama kituo kikuu cha ulimwengu wa Kiislamu, linahesabiwa kuwa ni kitovu pia cha ulimwengu wa Kiislamu. Nchi kama Iran, Uturuki, Syria, Iraq, Saudi Arabia Lebanon, Palestina na Misri zipo katikati ya ulimwengu wa Kiislamu au katika Mashariki ya Kati. Eneo la Mashariki ya Kati ni njia na kituo cha mawasiliano ya mabara matatu ya Asia, Ulaya na Afrika. Katika eneo hili kuna bahari ya Mediterranean, Bahari Nyekundu, Bahari ya Oman na Ghuba ya Uajemi. Asilimia kubwa kabisa ya akiba ya mafuta na gesi duniani inaptikana katika eneo hili nyeti kabisa la ulimwengu wa Kiislamu.
Na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana eneo hili limekuwa likimezewa mate na nchi zenye uchu na tamaa na kuzingatiwa na madola ya kikoloni. Na ndio maana leo hii ukitazama unapata kuwa, eneo hili ndilo linalokabiliwa na mapigano, migogoro na machafuko mengi, ambayo bila shaka yanatokana na njama maalumu za maadui dhidi ya eneo la Mashariki ya Kati.
Baada ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Duniani, ili madola ya kikoloni yaweze kulidhibii eneo la Mashariki ya Kati yalifanya njama za kuzusha fitna, na hitilafu za kikaumu na kimadhehebu na kisha yakazigawanya nchi za Kiislamu katika nchi ndogo ndogo zisizo na nguvu, ili kwa njia hiyo yaweze kufikia malengo yao haramu. Ni kutokanana sababu hiyo ndio leo hii tukashuhudia Waislamu wakikabiliwa na machafuko na mapigano yasiyokwisha. Madola ya kikoloni ya Magharibi yakistafidi na hitilafu hizo, yamechukua hatua za kujikita na kujizatiti na hivyo kuimarisha misingi ya tawala zao. Idadi ya nchi zinazopatikana katika eneo hili ni takribani mara tatu ya nchi za Kaskazini mwa Afrika.
Eneo jingine ni la Mashariki mwa Ulimwengu wa Kiislamu linalojumuisha nchi kama vile Indonesia na Malaysia. Moja ya sifa na umuhimu mkubwa wa Indonesia ni kuwa kwake na Waislamu wengi zaidi duniani kwani takwimu zinaonyesha kwamba, kuna Waislamu milioni 215 katika nchi hiyo. Bahari ya Hindi ni moja ya njia muhimu za majini ulimwenguni.
Eneo la Kiistratejia la Mlango Bahari wa Malacca, mahala zinapokutana bahari mbili kubwa na bahari ya Hindi linapatikana baina ya nchi mbili za Indonesia na Malaysia. Kwenda na kurudi meli za abiria na zile zinazobeba mafuta zimekuwa zikitumia Mlango Bahari wa Malacca kwa ajili ya kusafirisha mafuta katika nchi zenye viwanda na zilizoendelea za Bahari ya Pacific kama vile Japan.
Aidha bidhaa za eneo hilo husafirishwa katika masoko ya nchi za Mashariki ya Kati kupitia lango hilo.
Eneo jingine ambalo linahesabiwa kuwa kituo kingine muhimu cha Waislamu ni la Kaskazini mwa Afrika. Nchi muhimu zinazopatika katika eneo hilo ni Misri, Libya, Tunisia, Algeria na Morocco. Kanali au mfereji wa Suez na Lango Bahari la Jabal Tariq ni vivuko viwili muhimu vya bahari katika eneo hilo muhimu. Mfereji wa Suez unaunganisha Bahari nyekundu na Bandari muhimu ya Port Said iliyoko pambizoni mwa bahari ya Mediterranean. Aidha mfereji wa Suez ni njia muhimu ya mawasiliano baina ya Bahari ya Hindi na Bahari ya Atlantic na njia fupi kabisa kwa watu wa nchi za Ulaya wanapotaka kuelekea Bahari ya Hindi. Aghalabu ya nchi zinazofanya biashara za baharini hutumia mfereji wa Suez. Lango Bahari la Jabal Tariq kutokana na kuweko mawasiliano baina ya bahari za Atlantic na Pacific ni njia ya bahari inayohesabiwa kuwa na msongamano mkubwa duniani.
Eneo la mwisho ni lile la Kaskazini mwa Ulimwengu wa Kiislamu ambalo linajumuisha nchi za Asia ya Kati, na Caucasia kama vile Turkmenistan, Kazakhstan, Tajikistan, Uzbekistan na Azerbaijan. Eneo hili pia kama yalivyo maeneo mengi ya Kiislamu lina utajiri mkubwa wa mafuta na gesi, ambazo ni nishati mbili muhimu duniani. Kiujumla tunaweza kusema kuwa, ukubwa wa ardhi za Kiislamu ni sawa na asilimia 24 ya ukubwa wote wa dunia. Ukubwa wa nchi hizo ni sawa na kilomita mraba milioni 30.
Kijiografia, kama tulivyoashiria katika vipindi vyetu vilivyotangulia, Ulimwengu wa Kiislamu upo katika eneo nyeti na tajiri na lenye suhula nyingi. Hapana shaka kuwa, kutumiwa suhula hizo vizuri na kwa njia sahihi kutaandaa uwanja wa kuwepo mtazamo mmoja katika ulimwengu wa Kiislamu na hivyo kukabiliana na hatari yoyote itakayoukabili ulimwengu huu.
Moja ya sifa muhimu za nchi za Kiislamu ni kuwa kwake katika eneo la kiistaratejia kijigrafia na kisiasa, suala ambalo kiuchumi na kisiasa limelifanya eneo hili kuzingatiwa mno kimataifa. Kama mnavyofahamu moja ya tano ya ardhi ya nchi kavu ni miliki ya Waislamu. Nusu ya maeneo 14 ya kiistratejia duniani yanapatikana katika ulimwengu wa Kiislamu.
Eneo la MashariKI ya Kati ni chimbuko la dini tatu kubwa za Mwenyezi Mungu yaani Uislamu, Uyahudi na Ukristo. Hata kama Mashariki ya Kati ni sehemu tu ya UliMwengu wa Kiislamu, lakini kupatika Nyumba ya Mwenyezi Mungu al-Kaaba na kuweko msikiti mtakatifu wa al-Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu ni mambo yanayolifanya eneo hili kuwa na umuhimu wa aina yake. Kuweko pia mito, malango bahari kadhaa kunazidi kulifanya eneo la Mashariki ya Kati kuwa na umuhimu mkubwa wa kiistraejia kisiasa na kijiografia. 


Ulimwengu wa Kiislamu Fursa na Changamoto (7) 

Tulisema katika makala yetu iliyotangulia kwamba, hata kama eneo la Mashariki ya Kati ni sehemu tu ya Ulimwengu wa Kiislamu, lakini kupatikana Nyumba ya Mwenyezi Mungu yaani al-Kaaba na kuweko msikiti mtakatifu wa al-Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu katika eneo hili, ni mambo yanayolifanya kuwa na umuhimu wa aina yake.
Hapana shaka kuwa, kuweko pia mito, malango bahari kadhaa kunazidi kulifanya eneo la Mashariki ya Kati kuwa na umuhimu mkubwa wa kisiasa na kijiografia. Kama mnavyojua, chanzo kikubwa cha nishati muhimu kabisa duniani yaani sehemu kubwa ya akiba ya mafuta inapatikana katika ulimwengu wa Kiislamu.
Nchi wanachama wa Opec zimekuwa na nafasi muhimu kutokana na kuwa na asilimia 70 ya akiba ya mafuta.
Ni kutokana na suala hilo, ndio maana eneo la Mashariki ya Kati likajulikana kama ghala na stoo ya mafuta ulimwenguni. Nishati ya mafuta ni maliasili na utajiri muhimu wa ardhini katika Mashariki ya Kati.
Takribani thuluthi mbili ya akiba ya mafuta ulimwenguni inapakatikana katika Mashariki ya Kati. Nchi za Ghuba ya Uajemi pekee zina asilimia 60 ya akiba ya mafuta yote duniani hali ambayo imethibitisha kwamba, akiba ya mafuta ya dunia ipo mikononi mwao. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana eneo la Ghuba ya Uajemi ambalo nchi zake ni za Kiislamu likawa na umuhimu mkubwa na kutazamwa na maadui kwa jicho la tamaa na uchu.
Leo hii ni watu wachache mno ambao hawatambui hali ya kisiasa inayotawala hivi sasa katika eneo hili ambalo ni sehemu muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu. Matukio ya leo ya kisiasa katika eneo la Mashariki ya Kati yameathiriwa na mafuta na nishati. Moja kati ya sababu kuu za madola ya Magharibi ya kuanzisha vituo vya kijeshi katika Ghuba ya Uajemi na kuikalia kwa mabavu Iraq ni kutaka kupora maliasili na utajiri uliopo katika eneo hili. Eneo la Mashariki ya Kati linaungana na Afrika kupitia jangwa la Sinai nchini Misri. Nchi za Kaskazini mwa Afrika zinaunda eneo la magharibi mwa ulimwengu wa Kiislamu. Nchi muhimu katika eneo hilo ni Misri, Libya, Algeria, Tunisia na Morocco.
Aidha kuna vivuko muhimu vinavyopatikana katika eneo la Kaskazini mwa Afrika kama vile mfereji wa Suez, Bab al Mandab na Jabal Tariq. Gharama za kusafirishwa mafuta ya Mashariki ya Kati na ya kaskazini mwa Afrika kuelekea katika madola ya Magharibi na kuingia kwa bidhaa za Ulaya katika eneo hili kupitia mfereji wa Suez ni nafuu zaidi zikilinganishwa na njia ya Rasi ya Tumaini Jema au Cape Town iliyoko kusini mwa Bara la Afrika.
Nchi za kaskazini mwa Afrika zina maliasili na utajiri mkubwa wa ardhini. Morocco moja ya nchi zilizoko katika eneo hilo ina zaidi ya asilimi 70 ya akiba ya fosfati au chumvi ya asidi duniani.
Nchi hiyo pamoja na Tunisia na nchi nyingine mbili za Togo na Senegal zinauza na kudhamini thuluthi mbili ya fosfati yote duniani. Madini ya chuma ya kobalti na manganizi yana umuhimu mkubwa nchini Morocco. Nchi za Algeria na Tunisia ni miongoni mwa nchi zinazozalisha na kuuza kwa wingi nje madini ya chuma. Sehemu fulani ya ardhi ya kaskazini mwa Afrika ina mafuta na gesi.
Katika makala zetu zilizotangulia tulizungumzia ingawa kwa mukhtasari sifa maalumu ya eneo la katikati mwa Ulimwengu wa Kiislamu yaani Mashariki ya Kati na lile la Magharibi ambalo linajumuisha nchi za kaskazini mwa bara la Afrika.
Kwa haraka haraka tunalitupia jicho pia eneo la mashariki mwa ulimwengu wa Kiislamu. Maeneo muhimu ya eneo hili ni pwani ya Bahari ya Hindi ambayo ni mali ya Waislamu.
Kwa maneno mengine ni kuwa, wakazi wa eneo hilo ni wafuasi wa dini tukufu ya Kiislamu. Eneo hilo kubwa lina kaumu na makabila tofauti pamoja na utamaduni, historia, mila, desturi na mifumo mbali mbali ya kisiasa na kiuchumi. Moja kati ya maeneo muhimu na ya kiistratejia katika ulimwengu wa Kiislamu, yaani Lango Bahari la Malacca linapatikana katika eneo hilo.
Kama tulivyoashiria katika makala zilizotangulia, lango bahari hili ni njia muhimu ya mawasiliano ya majini na ni mahala zinapokutana bahari mbili za Hindi na Atlantic na lango hilo lipo baina ya nchi mbili za Kiislamu za Indonesia na Malaysia. Pakistan, Bangladesh, Malaysia na Indonesia ni miongoni mwa nchi za Kiislamu zinazohesabiwa kuwa zipo mashariki mwa Ulimwengu wa Kiislamu, ambazo zina nafasi muhimu katika mabadilishano ya kibiashara ulimwenguni. Jamhuri ya Kiislamu ya Pakistan ina Waislamu milioni 157 na hivyo kuhesabiwa kuwa, moja ya nchi za Kiislamu zenye Waislamu wengi duniani. Mazao muhimu yanayolimwa nchini humo ni ngano, mahindi, pamba na mpunga.
Aidha nchini Pakistan zao la miwa linalimwa. Bidhaa muhimu za viwanda na madini ni baadhi ya vitu ambavyo hudhamini sehemu kubwa ya pato la fedha za kigeni la Pakistan.
Bidhaa nyingine katika uwanja huo ni plastiki, shaba nyekundu na vitambaa vya nguo. Katika kipindi chetu kijacho tutatupia jicho bidhaa na vifaa vinavyozipatia pato na fedha za kigeni nchi nyingine mbili muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu yaani Malaysia na Indonesia pamoja na mazao yanayolimwa kwa wingi katika nchi hizo

Ulimwengu wa Kiislamu Fursa na Changamoto (8) 

Katika makala yetu iliyopita tulianza kuzungumzia bidhaa na mazao yanayolimwa na kuzalishwa katika nchi za mashariki mwa ulimwengu wa Kiislamu na tulisema kuwa bidhaa muhimu za viwanda na madini ni baadhi ya vitu ambavyo huvipatia Pakistan pato na fedha za kigeni. Bidhaa nyingine tulizoziashiria katika uwanja huo ni plastiki, shaba nyekundi na vitambaa vya nguo.
Nchi nyingine muhimu za Indonesia na Malaysia ni nchi nyingine za Mashariki mwa Ulimwengu wa Kiislamu na kama mnakumbuka nilikuahidini katika kipindi kilichopita kuzungumzia mazao na bidhaa za nchi hizo katika makala yetu ya leo.
Malaysia ni nchi inayosifika kwa kuwa na viwanda vya kusindika vyakula, vifaa vya viwanda na vifaa vya umeme, mafuta na viwanda vya madawa na kemikali. Aidha nchi ya Malaysia ndio nchi inayozalisha zao la mpira kwa wingi duniani. Zao la Mpira linahesabiwa kuwa moja ya mazao ya biashara nchini humo. Amma Indonesia ambayo ndiyo nchi yenye Waislamu wengi duniani, yenyewe inahesabiwa kuwa ni moja ya nchi zinazosafirisha gesi kwa wingi duniani.
Nchi hii pia ndio yenye mjumuiko wa visiwa vikubwa. Indonesia ina visiwa vitano vikubwa ambavyo ni Sumatra, Kalimantan, Irian Jaya, Sulawesi na Java. Aidha nchi hiyo ina visiwa vingine zaidi ya 13,000 na lugha au makabila 365. Nafasi muhimu ya kiistratejia na kijiografia, ardhi nzuri na yenye rutuba nzuri kwa kilimo, madini yenye thamani, na utajiri mkubwa wa mafuta na gesi, ni mambo yaliyowafanya wakoloni katika miaka ya nyuma waliowahi kuidhibiti Indonesia kubaki kwa muda mrefu nchini humo wakipora mali na utajiri wa nchi hiyo.
Ulimwengu wa Kiislamu kwa kuwa na wakazi wapatao bilioni moja na nusu, ina soko muhimu la nguvu kazi. Kama mnavyofahamu miongoni mwa mambo yenye athari kubwa katika uwanja wa kiuchumi na kiustawi ni nguvu kazi.
Leo hii katika hali ambayo, nchi zilizoendelea zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa nguvu kazi ya vijana na ya bei nafuu, Ulimwengu wa Kiislamu unasifika kwa kuwa na nguvu kazi kubwa ya vijana.
Hata hivyo cha kusikitisha ni kwamba, rasilimali hiyo hadi sasa haijatumiwa vizuri kama inavyotakiwa. Kwa kuandaliwa mazingira mazuri kwa ajili ya kuwandaa vijana wa Kiislamu na kuwapatia kozi na mafunzo , vijana hao baada ya kupata ujuzi wanaweza kuwa, nguzo na msingi imara kwa ajili ya ustawi na maendeleo kwa nchi zao; na hivyo kupunguza kama si kumaliza kabisa tatizo la ustawi na maendeleo. Utajiri na maliasili zisizohesabika katika Ulimwengu wa Kiislamu hasa katika baadhi ya nchi za Kiislamu ni jambo jengine lilizozifanya nchi za Kiislamu kuwa na uwanja mzuri na mwafaka kwa ajili ya uwekezaji vitega uchumi.
Hapana shaka kuwa, kufunguliwa milango kwa ajili ya uwekezaji vitega uchumi kwa njia sahihi na bora, ni mambo ambayo si tu kwamba, yatapelekea kukuza uchumi wa nchi husika, bali yatapelekea pia kuongezeka soko la ajira na nafasi za kazi.
Kila nchi katika ulimwengu wa Kiislamu inasifika kwa kuwa na zao au kuzalisha kwa wingi bidhaa fulani. Kiasi kwamba, baadhi ya mazao au bidhaa zimekuwa ndizo utambulisho wa nchi fulani pindi zinapotajwa. Kwa mfano nchi ya Tunisia ni mashuhuri mno duniani kwa kilimo cha Zeituni kiasi kwamba inashikilia nafasi ya kwanza katika ulimwengu wa Kiislamu.
Algeria nayo imeondekea kuwa mashuhuri kutokana na kulima, kusafirisha na kuuza kwa wingi nje ya nchi matunda ya zabibu na nchi hiyo inajulikana kuwa, kituo cha kuzalisha zabibu katika ulimwengu wa Kiislamu. Kutokana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa na mazingira na tofauti ya hali ya hewa na kimaumbile, imekuwa ikizalisha na kutoa mazao mengi ya wakati wa joto na wakati wa baridi. Iran ni mashuhuri mno kwa uzalishaji wa tende, pistachio na zafarani. Kwa upande wa Bangladesh yenyewe ni mashuhuri kwa ulimaji wa zao la katani na kuzalisha chai pamoja na kusafirisha kwa wingi zao hilo duniani. Pamba ya Misri ndiyo iliyoondokea kupendwa zaidi ulimwenguni. Pwani ya Jamhuri ya Sahara Magharibi kutokana na kuwa na samaki wengi inahesabiwa kuwa moja ya pwani muhimu kabisa ulimwenguni. Kutokana na Morocco kuvua kwa wingi samaki hasa samaki wa sadini ambao zaidi hupikwa na kutiwa kwenye makopo, pwani yake inahesabiwa kuwa tajiri kabisa ulimwenguni.
Aidha moja ya mambo yanayozipatia pato la fedha za kigeni nchi za Ghuba ya Uajemi ni kuvuliwa samaki aina ya kamba na lulu ambayo hutumika kuwa kito katika mapambano. Mambo hayo ni miongoni mwa fursa ambazo nchi za Kiislamu zinaweza kustafidi nazo kwa ajili ya kuinua kiwango cha maisha ya wananchi wake na kumaliza kabisa tatizo la ajira na ugumu wa maisha.
Ulimwengu wa Kiislamu mbali na kuwa na uwezo wa kiuchumi na kisiasa unabeba ujumbe mkubwa wa kiutamaduni katika karne ya 21. Katika Milenia ya tatu Ulimwengu unaonekana kuelekea katika masuala ya kimaanawi. Kiu hiyo ya kimaanawi inatokana na hamu na shauku ya kifikra ya wanadamu, ambao hawakupata majibu ya shubha na utata waliokuwa nao pindi walipokuwa katika maktaba na fikra za kimada. Kuongezeka kwa mtazamo wa Kiislamu katika nchi za Magharibi hasa baada ya matukio ya Septemba 11 nchini Marekani mwaka 2001 kunamaanisha kwamba, wananchi wa Magharibi hawana imani na madai na propaganda za vyombo vya habari vya nchi zao. Licha ya vyombo vya Magharibi kueneza propaganda kwamba, Uislamu haukumpa mwanamke haki zake anazostahiki, idadi ya wanawake waliosilimu na kuikubali dini ya Kiislamu katika nchi hizo ni kubwa ikilinganishwa na ya wanaume. Jarida la Times la Uingereza liliandika katika makala moja kwamba, nchini Marekani idadi ya wanawake wanaosilimu na kuingia katika Uislamu ni mara nne ya wanaume. Aidha utafiti uliofanywa na taasisi moja ya Kiislamu ya Uingereza unaonyesha kuwa, aghalabu ya watu wanaosilimu na kuingia katika Uislamu wana umri kati ya miaka 30 hadi 50, suala ambalo kwa hakika linabainisha ni kwa kiasi gani dini hii ni ya kimantiki na kiakili.

 

0 toamaon yako:

Author

CONTACT ME FOR WEB AND BLOG DESIGNING...

uislam na maisha yake

uzayuni

swahili radio

uislam na maisha

mohamed waziri

Subscribe to our Mailing List

We'll never share your Email address.
+255 (762) 118-805 mohamedwaziri295@gmail.com