Rais Yoweri Museveni wa Uganda
amemfuta kazi Amama Mbabazi Waziri Mkuu wa nchi hiyo. Rais
Museveni
hakutaja sababu iliyomfanya amfute kazi Waziri Mkuu wa Uganda. Msemaji
wa serikali ya Uganda amesema kuwa kufutwa kazi Mbabazi ni katika fremu
ya marekebisho ya baraza la mawaziri. Pamoja na hayo, weledi wa mambo
wanaamini kuwa, Amama Mbabazi huwenda akawa miongoni mwa wapinzani wa
Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi ujao wa rais hapo mwaka 2016.
Amama Mbabazi ni miongoni mwa waitifaki wa siku nyingi wa Museveni na
duru za kisiasa za Afrika zinamuona kama ndiye shakhsia nambari moja
katika siasa za Uganda. Mbali na kuwa Waziri Mkuu, Amama Mbabazi alikuwa
pia Katibu Mkuu wa chama tawala cha Harakati ya Mapambano ya Kitaifa ya
Uganda (NRM). Baada ya Mbabazi kuuzuliwa katika kiti cha Katibu Mkuu wa
chama tawala mwezi Machi mwaka huu, weledi wa masuala ya kisiasa
waliitaja hatua hiyo kuwa ni ishara ya awali ya kuweko mivutano na
hitilafu kati ya Museveni na muitifaki wake wa siku nyingi. Hivi sasa
baada ya kufutwa kazi Amama Mbabazi katika kiti cha Waziri Mkuu wa
Uganda na nafasi yake kuchukuliwa na Ruhakana Rugunda, aliyekuwa Waziri
wa Afya, imebainika wazi kwamba hitilafu zimejitokeza kati ya waitifaki
hao wawili wa siku nyingi.

Baadhi ya duru za habari zinasema kuwa
muswada wa serikali uliopasishwa bungeni hivi karibuni ni moja ya sababu
zilizozusha hitilafu hizo. Wawakilishi wa chama tawala ambao wana viti
vingi katika Bunge la Uganda, hivi karibuni walipasisha muswada ambao
umemruhusu Yoweri Museveni, kiongozi wa chama tawala, kuwa mgombea pekee
wa chama hicho katika uchaguzi ujao. Museveni ambaye yuko madarakani
huko Uganda tangu mwaka 1986, iwapo atashinda katika uchaguzi mkuu wa
mwaka 2016, basi ataitawala Uganda kwa zaidi ya miaka 30. Kwa msingi
huo, tunaweza kumtaja Museveni kuwa ni mmoja wa viongozi wa siku nyingi
katika bara la Afrika ambao hawana nia ya kuondoka madarakani. Wakati
huo huo Yoweri Kaguta Museveni amekuwa akiwashinda mahasimu wake katika
chaguzi zote za rais wa Uganda kwa kuchaguliwa kwa kura za wananchi,
japokuwa vyama vya upinzani vinakituhumu chama tawala kuwa kimekuwa
kikifanya udanganyifu na kutokuwa na mpangilio katika upigaji kura.
Kwa vyovyote vile, kuna dhana kuwa
kufutwa kazi aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uganda Amama Mbabazi ni katika
jitihada za kufuta ushindani katika uongozi wa chama tawala katika
uchaguzi mkuu ujao wa rais.
0 toamaon yako: