
Januari mwaka 2012 Umoja wa Ulaya ulisitisha kununua mafuta
ya Iran na ukaiwekea vikwazo Benki Kuu ya Jamhuri ya Kiislamu kwa
shabaha ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya Tehran na kubana shughuli za
kuzalisha nishati ya nyuklia hapa nchini. Baada ya uamuzi huo wa Umoja
wa Ulaya mali zote za Benki Kuu ya Iran barani Ulaya zilizuiliwa. Mbali
na hayo Jumuiya ya Kimataifa ya Kuhamisha Fedha Baina ya Mabenki kwa
kifupi (SWIFT) pia ilisitisha huduma zake kwa mabenki ya Iran.
Vikwazo hivyo vya Umoja wa Ulaya vilifuatia azimio la
Baraza la Usalama na wakati huo Baraza la Ulaya lilidai kuwa, miongoni
mwa sababu za kuiwekea vikwazo Benki Kuu ya Iran ni msaada wa benki hiyo
wa kuifanya Iran ikwepe vikwazo vya kimataifa. Iran kwa upande wake
iliwasilisha mashtaka kwenye mahakama za Umoja wa Ulaya na sasa mahakama
ya umoja huo imetoa hukumu kwamba, Baraza la Ulaya halikuwasilisha
ushahidi wowote wa kuthibitisha madai yake dhidi ya Iran na kwa msingi
huo vikwazo hivyo vinapaswa kufutwa.
Awali pia mahakama moja ya Ulaya ilitoa hukumu ikiamuru
kufutwa vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya makampuni saba ya Iran.
Mahakama ya hUlaya ambayo ni ya pili ya juu zaidi ya Umoja wa Ulaya
ilitangaza kuwa, umoja huo umeshindwa kuonesha ushahidi wa kuthibitisha
kuwa makampuni hayo yanajihusisha na shughuli za nyuklia za Iran.
Katika msimu wa joto kali wa mwaka uliopita, Mahakama ya
Juu ya Uingereza pia iliamuru kufutwa vikwazo vya serikali ya nchi hiyo
dhidi ya Benki ya Mellat ya Iran. Mahakama hiyo ilisema vikwazo vya
serikali ya Uingereza dhidi ya benki hiyo ya Iran si vya kisheria na
vinapingana na kanuni.
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita makampuni 14, benki
na vyuo vikuu vya Iran vimeondolewa katika orodha ya vikwazo vya Ulaya
na Marekani kutokana na juhudi zinazofanywa na serikali ya sasa ya
Tehran kwa ajili ya kuondolewa vikwazo vilivyowekwa na nchi hizo. Hukumu
ya sasa ya Mahakama ya Umoja wa Ulaya ya kufuta vikwazo vilivyowekwa na
nchi za bara hilo dhidi ya Benki Kuu ya Iran japokuwa ni ya mwanzo ya
mahakama hiyo na inaweza kukatiwa rufaa, lakini iwapo itapasishwa
inaweza kuwa na taathira kubwa nzuri katika mfumo wa fedha na miamala ya
kibiashara ya Iran. Kuondolea kwa vikwazo hivyo kutaiwezesha Iran
kurejesha nchini mamilioni ya dola za mauzo ya mafuta na bidhaa nyingine
kutoka nje kwa ajili ya ustawi wa nchi. Iwapo vikwazo hivyo vya Umoja
wa Ulaya vitafutwa, Iran itaweza kupeleka na kupokea fedha kutoka nchi
za kanda ya Euro. Vilevile Iran itazidisha kiwango cha biashara zake na
nchi za Ulaya, gharama za usafirisha wa fedha zitapungua sana na kasi ya
mabadilishano ya kifedha itaongezeka.
Inaonekana kuwa kutolewa hukumu ya Mahakama ya Umoja wa
Ulaya katika kipindi cha sasa cha duru mpya ya mazungumzo ya Iran na
kundi la 5+1 yanayofanyika kandokando ya mkutano wa kila mwaka wa Baraza
Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, hakukutokea kwa sadfa. Hukumu
hiyo inaweza kuwa ujumbe wa nchi za Ulaya kwa Marekani kwamba hazitaki
tena kuendeleza vikwazo dhidi ya Iran na kwamba yumkini Marekani
ikabakia peke yake katika kudumisha mashinikizo yake dhidi ya Jamhuri ya
Kiislamu.
0 toamaon yako: