
Jeshi la Cameroon limetangaza habari ya
kutiwa mbaroni kiongozi mwengine mwandamizi wa kundi la Boko Haram,
nchini humo. Jeshi la Cameroon limemtaja kiongozi huyo kuwa ni Ababakar
Ali maarufu kwa jina la Moustapha Oumar na kwamba alitiwa mbaroni
kaskazini mwa nchi hiyo akiwa na walinzi wake wawili waliofahamika kwa
majina ya Muhamed Ali na Issiaka Gare. Viongozi wa usalama nchini
Cameroon wamesema kuwa, Ababakar Ali alikuwa akijishughulisha na
ukusanyaji wa ripoti kwa ajili ya kundi hilo kwa lengo la kufanya
mashambulizi na kusimamia shughuli za wanachama wa kundi hilo lenye
uelewa potofu kuhusiana na mafundisho sahihi ya dini ya Kiislamu. Aidha
jeshi hilo limefanikiwa kunasa maficho ya silaha katika operesheni za
kumtia mbaroni kiongozi huyo wa Boko Haram. Ababakar Ali ni mmoja wa
viongozi wa kundi hilo ambaye pia alikuwa amekodi jengo na kulitumia
kama maficho ya silaha za kundi hilo. Inaelezwa kuwa katika nyumba hiyo
kumekutwa silaha mbalimbali zikiwemo bunduki na makombora na kwamba
jeshi la Cameroon limefaniwa kumtia mbaroni kiongozi huyo kwa
ushirikiano wa wananchi waliotilia shaka mienendo ya mtu huyo.
0 toamaon yako: