
Muhammad Yussuf Haji Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na
Siasa za Kigeni wa Bunge la Seneti la Kenya amekutana na kufanya
mazungumzo na Alauddin Bourujerdi Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa
na Siasa za Kigeni wa Majlis ya Ushauri ya Kiislamu yaani ‘Bunge la
Iran’ mjini Tehran na pande hizo mbili kusisitiza juu ya kuimarisha
mashirikiano katika nyanja zote na hasa katika masuala ya kibunge,
kiuchumi na kibiashara. Akizungumzia vikwazo vya kidhuluma vilivyowekwa
na nchi za Magharibi dhidi ya Iran, Bourujerdi amesema kuwa, vikwazo
hivyo vilivyowekwa yapata miongo mitatu iliyopita, vimepelekea kuimarika
moyo wa kujiamini na kusimama kidete kwa wananchi na taifa la Iran.
Akizungumzia kuongezeka vitendo vya kigaidi vinavyotishia amani na
usalama duniani, Bourujerdi amesisitiza kwamba Iran inapambana na
itaendelea kupambana kwa nguvu zake zote dhidi ya ugaidi, kinyume na
Marekani na waitifaki wake ambao ndio wasababishaji wakuu wa kuongezeka
vitendo vya ugaidi duniani. Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na
Siasa za Kigeni wa Bunge la Iran amesema kwamba, Iran iko tayari
kuinufaisha Kenya kwa uzoefu wake katika masuala ya usalama. Naye
Muhammad Yussuf Haji ameeleza kufurahishwa na ziara yake hapa nchini na
kusisitiza kwamba, kuimarishwa mashirikiano katika nyanja zote na Iran,
nchi ambayo inahesabiwa kuwa muhimu na yenye taathira kubwa katika eneo
la Mashariki ya Kati, ni jambo linalozingatiwa na bunge na serikali ya
Kenya. Haji ameongeza kuwa, hali inayoshuhudiwa hivi sasa hapa nchini
inathibitisha wazi kwamba, licha ya kuwepo mashinikizo na vikwazo vya
Wamagharibi, Iran bado imepiga hatua kubwa katika nyanja mbalimbali
ikiwemo ya kujipatia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani.
0 toamaon yako: