Katika mfululizo wa maandamano na malalamiko ya raia nchini Bahrain, maeneo kadhaa ya nchi hiyo yameendelea kushuhudia maandamano ya amani yanayofanywa na wananchi dhidi ya utawala wa kidikteta wa Aal-Khalifa. Wananchi wa Bahrain jana usiku walifanya maandamano katika maeneo ya ad-Diyah, an-Nuwaidirat na Kuranah na kutoa wito wa kuachiwa huru wafungwa wa kisiasa na kuhitimishwa ukandamizaji wa kuchupa mipaka wa utawala wa Aal-Khalifa. Washiriki walisisitizia juu ya kuendelezwa maandamano hadi matakwa yao yatakapotekelezwa.
Wakati huo huo, vyama mbalimbali vya kisiasa vimewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maandamano ya leo yatakayoanzia katika eneo la ad-Dair. Jana Wizara ya Mambo ya ndani ya Bahrain ilipiga marufuku maandamano hayo ya amani ya leo. Maandamano ya amani ya wananchi nchini Bahrain, yalianza mwaka 2011 katika maeneo tofauti ya nchi hiyo ambapo hata hivyo yamekuwa yakikabiliwa na ukandamizaji wa kuchupa mipaka wa maafisa wa utawala wa kidikteta wa Aal Khalifa.
0 toamaon yako: