Ijumaa, 26 Septemba 2014 12:50
Waziri Mkuu wa Morocco, Abdelilah Benkirane amesema kuwa, wakoloni ndio sababu ya machafuko yanayoshuhudiwa katika baadhi ya nchi za dunia hii leo. Benkirane ameyasema hayo akihutubia kikao cha 69 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York na kuyataka madola hayo kuamiliana kwa usawa na nchi zinazoinukia kiuchumi hususan za bara la Afrika. Amesema kuwa, nchi hizo zinatakiwa kuzisaidia nchi masikini badala ya kuzinyonya kama inavyoshuhudiwa hii leo. Ameongeza kuwa, ni suala la kusikitisha kwamba katika dunia ya leo hakuna mipango yoyote ya kuzisaidia nchi masikini kuinukia kiuchumi. Amefafanua kuwa hii leo kila nchi inaangalia maslahi yake binafsi katika njia ya kuelekea kwenye ustawi, suala ambalo limezifanya nchi nyingi kusalia nyuma kimaendeleo.
Akizungumzia hali ya machafuko na mauaji duniani, Waziri Mkuu wa Morocco amesema kuwa, wakoloni ndio wanaobeba dhima ya kihistoria ya yale yanayojiri ukiwemo umasikini, machafuko na mauaji yanayoendelea katika nchi mbalimbali zikiwemo za Kiafrika.
0 toamaon yako: