
Serikali ya Algeria ambayo ni mpatanishi katika mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Mali na makundi ya waasi ya kaskazini mwa nchi hiyo imezitaka pande mbili hizo kutumia vyema fursa ya mazungumzo ya amani na kufikia makubaliano. Takwa hilo limetolewa na Ramtane Lamamra, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Algeria ambaye amesisitiza kwamba, pande hasimu za Mali zinapaswa kutumia vyema na kadiri ziwezavyo fursa ya mazungumzo ya amani. Amesema kuwa, mazungumzo ya amani ya Mali yanayoendelea katika mji mkuu wa Algeria Algiers yanapaswa kutumiwa vyema na pande hizo mbili hasimu na hivyo kutiliana saini makubaliano ya mwisho ya amani.
Duru ya nne ya mazungumzo ya amani ya Mali ilianza jana nchini Algeria ambapo duru mbalimbali za kisiasa zinazitaka serikali ya Bamako na makundi ya waasi kufanya juhudi ili kufikia makubaliano ya mwisho ya amani. Kutofikiwa mazungumzo kati ya pande mbili kumezitia wasi wasi nchi nyingi hasa zinazopakana na Mali ambazo zinahofia kupenya makundi ya waasi na kuingia katika nchi zao. Hivi karibuni Jeshi la Algeria liliimarisha usalama katika mpaka wake na Mali ili kuzuia upenyaji na uingiliaji wa magaidi kutoka kwa jirani yake huyo.
0 toamaon yako: