Askari wa Israel wamevamia nyumba kadhaa
za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa
mabavu na kuwateka nyara vijana wasiopungua saba wa Kipalestina. Vijana
hao wa Kipalestina wametekwa nyara baada ya wanajeshi wa Israel kuvamia
nyumba zao katika
miji ya Baytullahm, Quds, Husan na al Khalil mapema
leo Jumapili. Wakazi wa maeneo hayo wamesema kuwa, vijana hao
wamepelekwa kusikojulikana. Watano kati ya vijana hao wanadaiwa
kuwalenga mawe wanajeshi wa utawala wa Kizayuni. Shirika la haki za
binadamu la Palestina limesema kuwa, hivi sasa utawala wa Kizayuni
unawashikilia Wapalestina 540 bila ya kuwafikisha mahakamani na kwamba
kasi ya kutekwa nyara Wapalestina imeongezeka sana katika miaka ya hivi
karibuni. Wazayuni wanaendelea kuwanyanyasa na kuwateka nyara kiholela
Wapalestina huku hivi karibuni yaani tarehe 7 Julai utawala huo ukiwa
umefanya mashambulizi ya kikatili dhidi ya Ukanda wa Ghaza na kuua mamia
kwa mamia ya watu wasio na hatia kwa madai yasiyothibitishwa kuwa
vijana watatu wa Kizayuni walitekwa nyara katika Ukingo wa Magharibi wa
Mto Jordan.
0 toamaon yako: