Serikali ya Misri inaendelea kutumia
mabavu dhidi ya wanachama wa Ikhwanul Muslimin. Hatua ya hivi karibuni
kabisa iliyochukuliwa na serikali ya Misri ni ile ya kuwahukumu kifungo
cha maisha jela, wanachama 73 wa kundi hilo. Maafisa wa mahakama wa nchi
hiyo wamedai kuwa, wanachama hao wamepatikana na hatia ya kufanya
vitendo vya uharibifu na uvunjifu wa amani. Abdullah Barakat, Mkuu wa
Chuo Kikuu cha Kiislamu ambaye pia ni miongoni mwa wanachama waandamizi
wa Ikhwanul Muslimin nchini Misri
naye amekumbwa na tuhuma hizo hizo na
amehukumiwa kifungo cha maisha jela na kulipa fidia ya dola 2,769. Hivi
karibuni pia kulisambazwa habari za kutiwa mbaroni wanachama 123 wa
Ikhwanul Muslimin katika mikoa 13 ya Misri. Inavyoonekana ni kuwa
watawala wa Misri wanatumia mahakama ili kuwabana zaidi na zaidi kisiasa
na kijamii wanachama wa Ikhwanul Muslimin. Hivi sasa viongozi wa daraja
la kwanza, wa daraja la pili na wa daraja la tatu wa kundi hilo, wote
wako jela wakiongozwa na Muhammad Morsi, Rais aliyechaguliwa na wananchi
na kupinduliwa na jeshi. Muhammad Badie, kiongozi mwingine mkubwa wa
Ikhwanul Muslimin naye ni miongoni mwa wanachama wa kundi hilo
aliyehukumiwa kifungo cha maisha jela. Itakumbukwa kuwa, wakati wa
kampeni za kuwania urais nchini Misri, Rais Abdul Fattah Sisi aliahidi
kuwa akichaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo ataiangamiza kikamilifu
Ikhwanul Muslimin nchini humo, na atahakikisha wanachama wote wa
harakati hiyo wanafutwa nchini Misri. Baada ya kutoa matamshi hayo,
wimbi la kuwatia mbaroni wanachama wa kundi hilo lilianza. Baadhi ya
duru za habari zimetangaza kuwa, zaidi ya wanachama 1,400 wa Ikhwanul
Muslimin wameshatiwa nguvuni hadi hivi sasa huko Misri. Kosa kubwa la
wanachama hao ni kushiriki katika maandamano ya amani. Hata hivyo
serikali ya Cairo inawabandika tuhuma za kuhatarisha usalama wa taifa na
kutoa adhabu kali dhidi yao ambapo wengi wao wamehukumiwa kifo au
kifungo cha maisha jela, adhabu ambazo zimelalamikiwa sana duniani.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imeelezea kusikitishwa sana na adhabu
zinazotolewa na serikali ya Misri dhidi ya wanachama wa Ikhwanul
Muslimin na kutaka wahukumiwe kiuadilifu. Shirika la Haki za Binadamu la
Kiarabu lenye makao yake nchini Uingereza nalo limetoa tamko likisema
kuwa adhabu hiyo ni uvunjaji wa wazi wa sheria za ndani ya Misri na za
kimataifa. Shirika hilo limezitaka taasisi za kimataifa ukiwemo Umoja wa
Afrika AU kuchukua hatua za haraka za kuwaokoa wanachama hao wa
Ikhwanul Muslimin. Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden naye amekosoa adhabu
zilizotolewa dhidi ya wanachama wa kundi hilo huko Misri na kuitaka
jamii ya kimataifa iingilie kati. Wakati huo huo harakati ya Ikhwanul
Muslimin ya Misri nayo imetoa tamko mjini London Uingereza na kuzitaja
adhabu kali zinazotolewa dhidi ya wanachama wa kundi hilo na wapinzani
wengine nchini Misri kuwa ni za kutisha na kusema kuwa harakati hiyo
itatumia njia zote za amani kuhakikisha inawag'oa madarakani majenerali
wa kijeshi nchini Misri.


Facebook
Twitter
RSS
0 toamaon yako: