Tanzania swahili radio

IQRA FM RADIO

IQRA FM RADIO
IQRA FM RADIO ELIMU NA MATENDO UIMARA WA RADIO IQRA UPO MIKONOMI MWAKO CHANGIA RADIO IQRA KWA MPESA 0762118805TIGO PESA 0658118804

Tuesday, September 23

Uislamu na Mtindo wa Maisha

Posted by mkachu  |  Tagged as:

zamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nami katika sehemu ya kwanza ya kipindi kipya cha Uislamu na Mtindo wa Maisha. Kipindi hiki kitachunguza na kutupia jicho mtazamo na mafundisho ya dini kuhusu medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu na kuainisha mtindo wa maisha ya kiumbe huyo katika mtazamo wa Uislamu. Ni matumaini yetu kuwa mtakuwa nasi hadi mwisho wa safari ndefu ya makala hizi.    
XXXX
Hapana shaka kuwa maarifa tajiri ya Uislamu ambayo yanapata ilhamu kutoka kwenye Qur'ani Tukufu na Hadithi za Mtume (saw) na Ahlubaiti wake watoharifu yanaainisha njia sahihi na ya wazi kwa ajili ya kufikia kwenye saada na ufanisi wa dunia na Akhera. Katika kipindi cha sasa suala la kuainisha kigezo cha mtindo wa maisha wa Kiislamu ndio njia na wenzo bora zaidi wa kuweza kukabiliana na hujuma ya kiutamaduni ya Magharibi katika nchi na jamii za Waislamu. Kuelewa mbinu na mtindo wa maisha wa Kiislamu kunaweza kutayarisha uwanja mzuri wa kuhuishwa ustaarabu wa Kiislamu na maendeleo ya pande zote ya Waislamu.
Suala la kuzingatiwa mafunzo ya dini katika kuainisha mtindo wa maisha wa Kiislamu lina umuhimu mkubwa kwa kadiri kwamba, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei anasisitiza sana juu ya udharura wa kutiliwa maanani jambo hilo katika jamii za Waislamu. Ayatullah Khamenei amesena: Kila ustaarabu una sehemu mbili ambazo ni sehemu ya nyenzo na sehemu ya asili. Sehemu ya nyenzo ya ustaarabu ni maendeleo ya kiviwanda, kielimu na kiuchumi, na sehemu yake ya asili inahusiana na mbinu na mtindo wa maisha. Anasema: Sehemu ya nyenzo ina maana ya masuala ambayo hii leo tunayatambua kuwa ni maendeleo ya nchi kama elimu, uvumbuzi, viwanda, siasa, uchumi, nguvu ya kisiasa na kijeshi na heshima na hadhi ya kimataifa, vyombo vya propaganda na kadhalika. Vyote hivyo ni sehemu ya nyezo na zana za ustaarabu. Na sehemu kuu na asili ya ustaarabu ni mambo yanayohusu moja kwa moja maisha yetu wenyewe yaani mbinu na mtindo wa maisha. Hii ndiyo sehemu muhimu na asili ya ustaarabu kama suala la familia, namna ya kuona na kuanzisha familia, mtindo wa ujenzi wa nyumba na makazi, aina ya mavazi, kigezo cha matumizi, aina ya chakula, namna ya mapishi, burudani, hati na maandishi, lugha, kazi, mwenendo wa watu maeneo ya kazi, mwenendo wao katika vyuo vikuu na mashuleni, mwenendo wa watu katika shughuli na harakati za kisiasa, mwenendo wao katika michezo, mwenendo wetu katika vyombo vya habari, mwenendo wetu mkabala wa baba, mama, mke na watoto, mwenendo wetu mkabala wa viongozi na mwenendo wa viongozi mkabala wa raia wao, mwenendo wetu mbele ya polisi na vyombo vingine vya dola, safari zetu, usafi wa watu, mwenendo wetu mkabala wa adui, marafiki, wageni na kadhalika."
Mjadala wa mtindo wa maisha na kanuni na desturi za Kiislamu kuhusu mtu binafsi na jamii ni miongoni mwa masuala yenye umuhimu mkubwa ya kijamii. Hii ni kwa sababu nguzo kuu za utambulisho wa jamii yoyote ile ni itikadi, imani, thamani na mtindo wa maisha wa jamii husika. Hapana shaka pia kuwa uso na wajihi wa utambulisho wa jamii yoyote ile ni mtindo wa maisha wa jamii hiyo. Kila jamii inaweza kuonesha matunda ya itikadi na imani zake wakati mtindo wa maisha yake utakaponasibiana na kuwiana na itikadi na imani zake.
Inasikitisha kuwa hadi sasa jamii za Waislamu hazijaweza kujenga uhusiano sahihi na kamili baina ya itikadi zake za kimsingi na mtindo wa maisha yake katika nyanja mbalimbali za kijamii. Mtindo wa maisha katika aghlabu ya jamii hizo umeathiriwa na mila na desturi zisizo za Kiislamu na wakati mwingine zinazopingana na Uislamu. Katika makala hii hatutaki kuchunguza kwa kina sababu ya kuwepo mpasuko huo na mtengano kati ya mtindo wa maisha wa jamii za Kiislamu na mila na desturi za Uislamu, lakini inaonekana kuwa, miongoni mwa sababu muhimu za suala hilo ni ukosefu wa maarifa na utambuzi sahihi wa itikadi za Uislamu. Kwa maana kwamba, watu wengi katika jamii za Waislamu hawana utambuzi sahihi na maarifa ya kina kuhusu mila na desturi na pia mtindo wa maisha wa Uislamu na kwa msingi huo hawatumii mtindo huo katika maisha yao ya kila siku. Suala hili lina taathira kubwa sana katika maisha ya mtu na hata katika imani yake kwa ujumla. Hii ni kwa sababu wakati watu wanaposhindwa kujenga uhusiano sahihi baina ya mtindo wa maisha yao na itikadi zao za kidini yumkini baada ya muda wakatupilia mbali hata itikadi zao wenyewe na kuzitambua kuwa hazifai tena; na ili kuhalalisha hatua yao ya kufuata mtindo wa maisha usiowiana na itikadi na dini yao, watu hao huzitupia lawama itikadi na thamani za kidini na kudai kuwa zinafungamana na zama zilizopita au zisizokuwa na maendeleo.
 XXXX
Kutupilia mbali mtindo wa maisha wa kidini kumezielekeza jamii za Waislamu katika maisha ya Kimagharibi. Kwa msingi huo kuna udharura wa kuarifisha zaidi mafundisho ya Uislamu ambayo aghlabu yana sura ya kijamii hususan katika kipindi hiki ambapo Wamagharibi wanafanya jitihada za kuibana dini na mafundisho yake katika maisha ya mtu binafsi. Uislamu ambayo ni dini kamili na inayohusu pande zote za maisha ya mwanadamu, umekuja na sheria na kanuni zinazohusu maisha yote ya mtu binafsi na jamii kuanzia maisha ya familia, uchumi, jamii, siasa na hata kuhusu chakula, burudani, safari, jinsi ya mwanadamu anavyopaswa kuamiliana na nafsi yake mwenyewe, mazingira na watu wengine. Sheria na kanuni hizo zinaainisha mwenendo wa maisha ya Mwislamu.
Wapenzi wasikilizaji lengo la kipindi hiki ni kuarifisha mafundisho na mtazamo wa Uislamu kuhusu mbinu na mtindo wa maisha katika nyanja mbalimbali chini ya kivuli cha mafundisho ya Qur'ani na sira ya Mtume Muhammad (saw) na Ahlubaiti zake watohaifu. Katika kipindi hiki tutazungumzia sifa za mtindo wa maisha wa Kiislamu na sababu za kujitokeza kwake, nafasi na mchango wa itikadi za kidini katika maisha na vilevile mwenendo wa mwanadamu na nafsi yake kuanzia namna ya kufikiria kwake hadi namna ya mavazi na nguzo zake. Vilevile tutaeleza mafundisho ya dini kuhusu mwenendo wa mwanadamu na wanadamu wenzake kuanzia uhusiano wake na familia yake, majirani, ndugu zake katika dini na hata uhusiano wake na wasio Waislamu. Tutazungumzia jinsi ya kutumia wakati wa mapumziko na burudani salama na sahihi na kadhalika.
Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa kuashiria matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei akieleza udharura wa kuweka wazi na kuarifisha kwa njia sahihi mtindo wa maisha wa Uislamu na kujiepusha kufuata kibubusa utamaduni wa Magharibi. Anasema: Kuna udharura wa kujiepusha kukalidi na kuiga mitindo na utamaduni wa Magharibi. Anasema ili kuweza kujenga ustaarabu mpya wa Kiislamu, tunapaswa kujiepusha na taklidi na kuiga kibubusa mitindo ya Wamagharibi ambao wanafanya jitihada za kuyatwisha na kuyalazimisha mataifa mengine kufuata mbinu na mitindo yao ya kimaisha. Hii haina maana kwamba tunapaswa kufanya uadui dhidi ya Magharibi, bali ni kwa sababu kufuata utamaduni wa Magharibi hakukuwa na matunda kwa nchi zilizoamua kufanya hivyo isipokuwa maafa na madhara makubwa hata kwa zile nchi ambazo kidhahiri zinaonekana kuwa zimepiga hatua kubwa za maendeleo ya kiviwanda lakini zinazofuata na kuiga kibubusa utamaduni wa Kimagharibi. Sababu ya matokeo hayo ni kwamba utamaduni wa Magharibi ni utamaduni unaohujumu tamaduni za mataifa mengine. Utamaduni wa Magharibi unaangamiza na kuua tamaduni nyingine. Kwa sababu, mahala popote Wamagharibi walipoingia walihujumu na kufanya jitihada za kuua utamaduni asili wa maeneo hayo, wakaangamiza misingi na nguzo za kijamii na kubadilisha historia, lugha, hati na maandishi  za mataifa hayo kadiri walivyoweza."
XXXX
Wapenzi wasikilizaji muda uliotengwa kwa kipindi chetu cha leo umefikia ukingoni. Msikose kuwa nami wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Uislamu na Mtindo wa Maisha. Kwaherinini
Uislamu na Mtindo wa Maisha (1)





Uislamu na Mtindo wa Maisha (2)



Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine ya kipindi cha Uislamu na Mtindo wa Maisha. Katika kipindi chetu cha leo tutazungumzia mafhumu na maana ya mtindo wa maisha. Tafadhali endeleeni kuwa kando ya redio zenu kusikiliza niliyokuandalieni.
XXXX
Neno mtindo wa maisha au kwa kimombo Life Style lina maana ya mfumo wa maisha ambao humpa mtu, familia au jamii utambulisho makhsusi. Mfumo wa maisha unaweza kutambuliwa kuwa ni majmui kamili na yenye uwiano ya utendaji na mwenendo wa kila siku wa mtu. Vitu kama namna ya utumiaji wa vitu mbalimbali, mwenendo wa mtu, aina ya mavazi yake, maneno na mazungumzo yake, burudani zake, jinsi ya kutumia wakati wa mapumziko, mapambo na kidhahiri ya mtu, mila na desturi zinazohusiana na kula chakula, ujenzi wa miji, masoko, nyumba na kadhalika vyote vinaingia katika mtindo wa maisha yetu.
Kwa hakika mwenendo wetu ndio unaodhihirisha shakhsia yetu katika uwanja wa maisha na kuonesha itikadi, imani, thamani na mahusiano yetu, na mkusanyiko wa yote hayo huwa kielelezo cha shakhsia ya mtu binafsi na jamii.
Mtindo wa maisha ni mwenendo unaotokana na itikadi na thamani zinazotokana na mtazamo wa mwanadamu kuhusu dunia. Pale mwanadamu anaposifu na kupendelea aina makhsusi ya maisha au kukosoa vikali aina fulani ya maisha, basi suala hilo huwa kielelezo cha mfumo wa thamani zake ambao huwa na umuhimu na taathira kubwa katika kuchagua mtindo wake wa maisha. Kwa msingi huo haiwezekani kutenganisha baina ya mtindo wa maisha ya mtu na thamani, itikadi na imani zake.
Mambo mengi yanayochangia katika kutengeneza mtindo wa maisha huwa ya khiyari na wala si ya kulazimishwa. Kwani mtu anayelazimishwa kuwa na mwenendo kwa mujibu wa aina makhsusi ya maisha katika kambi ya kazi za kulazimishwa au katika hali ya kutekwa nyara na chini ya mashinikizo, hawezi kutambuliwa kuwa ana mtindo wake wa maisha. Mtindo wa maisha ni jambo linalochaguliwa, na mtu mwenyewe anapaswa kuwa na mchango asili katika kuarifisha, kupanga na kujenga mfumo huo kwa mujibu wa mfumo wake wa kiitikadi na thamani zake. Pamoja na hayo vyombo vya habari daima hutangaza picha mpya za mtindo wa maisha kwa mujibu wa mitazamo na imani za wamiliki wa vyombo hivyo, na kuzishawishi akili na fikra za watu kwa ajili ya kuchagua na kufuata mtindo huo.
Nukta nyingine ya kutiliwa maanani hapa ni kuwa, mtindo wa maisha ni jambo ambalo linaweza kutengenezwa na kubadilishwa; hii ni kwa sababu ni uamuzi wa mtu binafsi ambao unaweza kubadilika. Hata hivyo inatupasa kuelewa kuwa, wakati mwingine yumkini hali na mazingira ya kijamii yakatatiza sana suala la kubadili mtindo wa maisha. Ukiachilia kipindi cha utotoni ambapo shakhsia ya mtu inakuwa bado haijaumbika na kupata sura na utambulisho kamili, si rahisi kupata mwanadamu asiyekuwa na mila na desturi au mtindo wa maisha. Kwa maneno mengine ni kuwa, kila mtu ana mila na mtindo wake wa maisha na hata kama mwanadamu hatakuwa amepata malezi sahihi, lakini atakuwa pia na mila na mtindo wa maisha japo zitakuwa mbaya na zisizofaa. Hivyo basi kama hatukuchagua wenyewe aina makhsusi ya mwenendo na mtindo wa maisha, tutajikuta - kwa kujua au bila ya kujua - katika mitindo ya maisha iliyoainishwa na watu wengine katika maisha ya kijamii. Hivyo basi ni vizuri kwa mtu kuainisha mwenyewe taratibu na mtindo wa maisha yake na asiruhusu mazingira kuathiri na kuburuta maisha yake.     XXXX
Mtindo wa maisha huarifisha utambulisho wa mtu wa kijamii. Mtindo huo hujenga shakhsia za watu kwa maana kwamba, mwanadamu huainisha utambulisho wake kupitia mahusiano yake, aina ya kazi yake, vitu anavyotumia na mambo mengine anayochagua yeye mwenyewe. Katika upande mwingine kila mtu kwa mujibu wa mtindo wa maisha, (yaani vitu anavyokula, mavazi yake, mahala anakoishi, gari analotumia na aina ya watu anaokuwa na uhusiano nao) taratibu huanza kuwa na ada na mienendo ya aina fulani ambazo huumbika ndani ya nafsi yake. Jambo hili hupelekea kujitokeza mfumo makhsusi wa thamani na itikadi ndani ya nafsi yake.
Uchambuzi na unyambuzi wetu kuhusu shakhsia na utambulisho wa watu wengine kwa kiasi fulani hufungamana na vielelezo hivyo vya kidhahiri. Ili kuweza kutoa hukumu kuhusu utambulisho na shakhsia ya mtu kwa kawaida tunapaswa kujibu maswala kadhaa ambayo majibu yake hutupa ufahamu mpana na wa kuaminika kwa kiasi kikubwa kuhusu shakhsia yake. kwa mfano swali kwamba anafanya kazi ipi? Ana kipato kiasi gani? Anatumia gari aina gani? Anaishi katika eneo gani, anatembea na kuamiliana zaidi na akina nani na kadhalika vinatupa taswira ya kuaminika kwa kiwango kikubwa kuhusu utambulisho na shakhia ya mtu husika. Kwa njia hii tutaweza kujua misimamo, mwenendo, maamuzi ya kijamii, uwezo wa kiuchumi, mitazamo ya kisiasa na kadhalika ya watu wengine.
Katika medani kubwa ya jamii, mtindo wa maisha hupatikana kwa ushirikiano. Kwa kawaida watu ambao wameishi pamoja kwa miaka mingi taratibu huwa na fikra zinazofanana na kupenda au kuchukia vitu vinavyoshabihiana. Ushirika huo hufikia kiwango cha kuwa na misimamo na maamuzi yanayofanana ya kijamii, kiutamaduni na kimaadili na kuunda kambi moja au nguvu iliyojificha ya kijamii.
Hapa linajitokeza swali kwamba, mtindo wa maisha unaumbika vipi? Na ni vitu au mikono gani ya siri inayoongoza mtindo wa maisha?
Hapana shaka kuwa vinara wa jamii kama wasomi, maulamaa, wahadhiri wa vyuo vikuu, watawala, wazee wenye busara, watu wenye vipawa vya kielimu, kiutamaduni, wanamichezo mashuhuri, wasanii na kadhalika wana taathira na mchango mkubwa katika kuundika kwa mtindo wa maisha. Hata hivyo kiwango cha taathira ya makundi hayo kinatofautiana. Vilevile tunapaswa kutambua kuwa, mtindo wa maisha wa jamii huathiriwa sana na vyombo vya habari hususan televisheni. Katika maisha ya dunia ya sasa vyombo vya habari vimekuwa na mchango mkubwa sana katika maisha ya mwanadamu. Takwimu zilizofanyika kote duniani zinazonesha kuwa, utumiaji wa vyombo vya habari ndio kazi ya tatu inayofanywa zaidi ya wanadamu baada ya usingizi na kazi za kudhamini mahitaji ya kimaisha. Vyombo vya habari vinachukua sehemu kubwa katika maisha ya kila siku ya watu. Kwa sababu hiyo vyombo vikubwa na mashuhuri vya habari na mawasiliano ya umma vimekuwa na mchango mkubwa sana katika kueneza na kupigia debe mtindo wa maisha wa Kimagharibi katika dunia ya leo sambamba na kuharibu au kudhoofisha itikadi na thamani za kidini. Kwa kadiri kwamba baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa, kwa sasa dunia imo katika vita vya kimataifa vya vyombo vya habari dhidi ya itikadi na imani za kidini hususan itikadi na mafundisho ya Uislamu. Kanali mbalimbali za runinga, televisheni za satalaiti, mitandao ya intaneti, magazeti na majarida kila siku zinarusha matangazo na vipindi vinavyoimarisha na kueneza mtindo wa maisha wa kimagharibi na kuharibu utamaduni unaopinga mtindo huo wa maisha. Vyombo hivyo vya habari vinafanya jitihada kubwa kuwaelekeza walimwengu katika maisha ya Kimagharibi na kuyadhihirisha kuwa ndio matarajio makubwa ya mwanadamu wa sasa. Kwa sababu hiyo ni mara chache sana kuona vyombo hivyo vikikosoa mtindo wa kimaisha wa Kimagharibi. Wamiliki wa vyombo vya habari vya Magharibi wanaelewa kwamba iwapo vyombo hivyo vitaonesha kwa njia ya moja kwa moja mtindo wa maisha ya Kimagharibi kwa watu wanaoshikamana barabara na mafundisho ya dini yao watu hao hawatakubali suala hilo na kwa njia hiyo wanatumia mbinu ya kutangaza hatua kwa hatua vielelezo vya mtindo wa maisha ya Kimagharibi kupitia televisheni za satalaiti, runinga, intaneti, vitabu, magazeti, mitindo ya mavazi, usanifu majengo, matumizi ya vyakula na kadhalika.   
XXXX
Kama tulivyotangulia kusema, mtindo wa maisha wa kila mtu na jamii huathiriwa na aina ya itikadi, thamani na imani ya dini inayotawala jamii husika. Itikadi za kimaada na thamani zinazojali anasa za dunia hapana shaka kwamba zitakuwa na mtindo makhsusi wa kimaisha. Hivyohivyo itikadi za kidini zinazotegemea mafundisho ya Mwenyezi Mungu na thamani aali zinazolenga kumfikisha mwanadamu kwenye saada na ufanisi wa dunia na Akhera, zina mtindo makhsusi wa kimaisha. Katika hatua ya kwanza dini hutoa mtazamo wake kamili wa kiitikadi na kiaidiolojia ambao huwa msingi wa maisha ya kidini ya jamii husika. Katika hatua inayofuata dini hutoa maamrisho na mafundisho yake yanayohusu pande zote za maisha ya mwanadamu ambayo huyapa mwelekeo maisha yote ya kiumbe huyo. Kwa msingi huo mafundisho kama ya aina ya mavazi ya mtu, chakula, mapambo, mwenendo wa mtu kuhusu familia yake, mwenendo mtu na majirani zake, mwenendo wake na wafuasi wa dini yake na isiyo yake, mahusiano kati ya dini na dini na dini na madhehebu mbalimbali yote hayo ni kwa ajili ya kujenga mtindo wa maisha wa kidini.   
XXXX
Wapenzi wasikilizaji muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi chetu cha leo umemalizika. Ni matumaini yangu kuwa mtakuwa nami tena juma lijalo katika sehemu nyingine ya makaha hii. Kwaherini.



Uislamu na Mtindo wa Maisha (3)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (3)
Hamjambo wasikilizaji wetu wapenzi na karibuni kuwa nami katika sehemu ya tatu ya kipindi hiki cha Uislamu na Mtindo wa Maisha. Kipindi chetu cha leo kitaendelea kuarifisha maana ya mtindo wa maisha katika mafundisho ya Uislamu. Karibuni.   
XXXX
Kama tulivyosema katika kipindi cha wiki iliyopita mtindo wa maisha wa mtu au jamii fulani huathiriwa na aina ya itikadi, imani na thamani zinazotawala fikra za mtu au jamii hiyo. Itikadi na aidiolojia za kimaada na thamani zilizojengeka kwa mujibu wa fikra za kupenda anasa na kudhamini maslahi ya kimaada huwa na mtindo makhsusi wa maisha. Vivyohivyo itikadi na aidiolojia za mbinguni na thamani zinazotaka kudhamini saada na ufanisi wa dunia na Akhera huunda mtindo wake makhsusi wa maisha.
Hii leo na licha ya kufanyika juhudi kubwa na za muda mrefu za kielimu na kisayansi za kutaka kumjua mwanadamu na maana ya maisha ya kiumbe huyo lakini wasomi wa anthropolojia (elimu ihusuyo habari za asili na maendeleo ya mwanadamu) wameshindwa kutoa jibu sahihi na kamili kuhusu maswali mengi muhimu yanayomhusu mwanadamu na mambo mbalimbali ya maisha yake. Ukweli wa mambo ni kuwa, itikadi na aidiolojia ya mwanadamu katika jamii na tamaduni mbalimbali inampa kiumbe huyo taswira tofauti kuhusu maana ya maisha ambayo kwa mujibu wake maisha ya mwanadamu hupata au kukosa maana. Kwa mfano iwapo katika taswira inayotolewa kuhusu maisha mwanadamu kiumbe huyo hatakuwa na lengo linalokubalika kiakili ambalo katika kipindi chote cha maisha yake hufanya harakati za kulifikia, au kama taswira hiyo itamuarifisha mwanadamu kuwa ni kiumbe anayetezwa nguvu katika amali na matendo yake na asiye na khiyari ya kujiamulia na kuchagua hatima yake, basi maisha ya kiumbe huyo hayatakuwa na maana na yatakuwa upuuzi mtupu. Wakati huo huo pale tutakapotoa taswira inayomdhihirisha mwanadamu kuwa ni kiumbe mwenye malengo yanayokubalika kiakili, mwenye uwezo wa kuchagua hatima yake na anayeweza kufikia malengo yake kwa juhudi zake mwenyewe, basi maisha ya kiumbe huyo yatakuwa na maana.
Katika mtazamo wa dini za mbinguni maisha ya kiumbe mwanadamu katika dunia hii hayaishii katika uhai wa kimaada tu, na mwanadamu anapaswa kuepuka mambo ya kipuuzi ili aweze kufaidika kikamilifu na uhai wake, na suala hili haliwezi kutimia isipokuwa kwa kujibu maswali kuhusu falsafa ya kuishi yaani amekuja kutoka wapi, yuko wapi na anaelekea wapi? Dini inatoa majibu ya wazi kwa maswali hayo muhimu na kuondoa shaka na dukuduku zinazojitokeza kuhusu maisha ya mwanadamu. Akili ya mwanadamu pia inaweza kujibu maswali hayo kwa kiasi fulani, lakini ufinyu wake unamfanya mwanadamu asiweze kufikia ufumbuzi wa mwisho na kamili wa maswali hayo.
Mafundisho ya dini katika uwanja huo yametoa taswira kamili na ya wazi kuhusu malengo na kiwango cha uwezo wa mwanadamu wa kuchagua na uhuru wake, na kila mtu anaweza kuarifisha kirahisi maana ya maisha yake chini ya kivuli cha uhuru na uwezo aliopewa wa kujiamulia mambo na mustakbali wake. Taswira hiyo inaweza kupatikana katika mafundisho ya dini yanayohusiana na tauhidi, utume na Siku ya Mwisho.
Katika itikadi na aidiolojia ya Kiislamu, mwanzo wa mwanadamu na Siku ya Mwisho vimetambuliwa kuwa sehemu mbili kuu katika ujudi na uwepo wa kiumbe huyo na kumebainishwa na kuwekwa wazi masuala yote yanayohusiana na maisha ya mwanadamu katika dunia hii na mwanzo na mwisho wake. Katika mtazamo wa itikadi na aidiolojia ya Kiislamu kumewekwa wazi uhusiano uliopo baina ya sehemu zote za maisha ya mwanadamu na kubainishwa pande zote za uhai wake wa kimaada na kiroho ikiwa ni pamoja na siku zake za huko nyuma, za sasa na mustakbali wake. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana wanafalsafa wa Kiislamu wameitaja hoja madhubuti zaidi ya udharura wa kutumwa mitume kuwa ni udharura wa kutaka kujua uhusiano uliopo baina ya dunia na Akhera na yanayopaswa na yasiyopaswa kufanywa ambayo yana taathira kubwa katika saada na ufanisi wa mwanadamu.    
 XXXX
Moja ya matunda muhimu ya kubaathiwa na kutumwa Nabii Muhammad (saw) ni mafundisho ya kiroho aliyokuja nayo ambayo yalibadili mtazamo na aidiolojia ya wafuasi wa dini ya Uislamu na kutayarisha uwanja mzuri wa kujitokea mtindo makhsusi wa maisha wenye uwiano na mlingano. Ili kuweka wazi zaidi suala hili tunalazimika kusema kuwa, katika maisha yake ya kila siku mwanadamu daima anafanya jitihada za kuarifisha uhusiano wake na viumbe wengine. Mfano wa jitihada hizo za mwanadamu ni mbinu zake za kutaka kudhibiti maumbile ya dunia kwa kutumia sayansi na teknolojia. Katika hali kama hii iwapo utamaduni wa jamii ya mwanadamu huyo haukuwa na mfungamano wowote na mafundisho ya dini au utakuwa unapingana na kukabiliana nayo, hapana shaka kuwa suala hili litazalisha mtindo wa maisha na mwenendo ambao hatua kwa hatua, utaimarisha udhibiti na nguvu ya teknolojia juu ya irada ya mwanadamu, kwani wakati huo mwanadamu atakiona kila kitu kuwa ni tegemezi na chenye kufungamana na teknolojia. Kwa maneno mengine ni kuwa, udhaifu wa mwanadamu mbele ya maumbile ya dunia uliokuwapo katika miaka mingi ya huko nyuma utabadilika na kuwa udhaifu na kusalimu amri mbele ya sayansi na teknolojia, suala ambalo kwa upande mwingine ni dhihirisho la udhaifu wa irada ya mwanadamu mbele ya nafsi na matamanio yake.
Mkabala wa hali hiyo, mtazamo anaoupata mfuasi wa dini kutokana na mafundisho yake humpa uwezo na nguvu ya kukabiliana na ladha za kupita za dunia na matamanio ya nafsi. Kwa hakika ladha na anasa zisizo na lengo za ustaarabu wa kimaada ambazo ni matunda ya udhibiti wa dunia ya kimaada, hudhibitiwa na kuwa na mlingano katika mtindo wa maisha uliojengeka kwa mujibu wa mafundisho ya dini. Kwa msingi huo, ustawi wa kimaada unaokubalika katika mtazamo wa itikadi na aidiolojia ya Kiislamu ni ule unaokuwa sababu ya kumuimarisha mwanadamu kiroho na kimaanawi. Kwa maneno mengine ni ustawi unaomsaidia zaidi mwanadamu katika njia yake ya kuelekea kwenye lengo la mwisho la kuumbwa kwake.
Moja ya sifa makhsusi za aidiolojia ya Kiislamu ni kuwa, kwa kutegemea itikadi ya tauhidi na kumpekesha Mwenyezi Mungu, dini hiyo inamtambua Mungu Mmoja kuwa ndiye mwenye athari halisi na asili katika dunia hii. Vilevile Qur'ani Tukufu katika uchambuzi wake wa matukio ya kijamii na maisha ya jamii ya mwanadamu, daima inasisitiza kuwa vitu vyote hivyo vina uhusiano na Mwenyezi Muumba na mwanzo wa kila kitu. Ukamilifu na lengo la mwisho la mwanadamu katika mtazamo wa Qur'ani ni saada na ufanisi wa mwisho wa kiumbe huyo.
Katika itikadi na mafundisho yake Uislamu unamfundisha mwanadamu kwamba dunia yake inafungamana kikamilifu na mwanadamu na wakati huo huo inamwambia kuwa maisha yake hayaishii hapa duniani. Kwa utaratibu huo Uislamu unaweka wazi uhusiano wa mwanadamu na mwisho na hatima yake. Hivyo basi mwanadamu anapaswa kulinda uhusiano huo wa dunia na maisha yake ya milele huko Akhera. Katika mtazamo wa Uislamu dunia ni utangulizi na wenzo anaopaswa kutumiwa na mwanadamu kwa ajili ya kufika kwenye saada na ufanisi wa kweli huko Akhera.
Katika fremu hiyo pana inayoainisha uhusiano wa mwanadamu na Mwenyezi Mungu kumebainishwa pia uhusiano wa mwanadamu na nafsi yake, wanadamu wengine na maumbile ya dunia.
Katika mtazamo wa Qur'ani dunia na Akhera ni awamu mbili za maisha ya mwanadamu. Awamu ya kwanza ni ya maisha ya sasa na ya karibu zaidi ya kiumbe huyo, na ya pili ni ya mbali na kamili zaidi. Awamu ya kwanza ya maisha ya mwanadmu ambayo ni dunia inatambuliwa kuwa ni utangulizi na daraja la kuelekea kwenye awamu ya pili ambayo ni kamili na ya asili ya mwanadamu. Hivyo hapana shaka kuwa mtindo wa maisha wa mwanadamu Muislamu utaathiriwa na itikadi na mafundisho hayo.
XXXX
Wapenzi wasikilizaji, muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi chetu cha leo unaelekea ukingoni. Tukutane tena wiki ijayo panapo majaaliwa ya Mwenyezi mungu. Kwaherini.

Uislamu na Mtindo wa Maisha (4

Uislamu na Mtindo wa Maisha (4)
Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki ambacho kinazungumzia nafasi ya dini katika mtindo wa maisha ya mwanadamu. Katika kipindi chetu cha leo tutatupia jicho sifa za fikra zinazotawala mtindo wa maisha katika nchi za Magharibi. Karibuni. XXXX
Bila shaka bado mnakumbuka kwamba katika vipindi vilivyopita tulisema kuwa mtindo wa maisha wa mtu au jamii hutokana na itikadi na aina ya mtazamo wao kwa dunia na vilivyomo. Hii ni kutokana na kuwa malengo yanayochaguliwa na watu katika maisha yao huainishwa kwa mujibu wa mtazamo na tafsiri yao kuhusu maisha. Hivyo watu wenye mtazamo wa itikadi za kimaada kuhusu ulimwengu na kutilia maana ladhaa na anasa zisizokuwa na mpaka hapa duniani tu, mtazamo huo hutengeneza mtindo makhsusi wa maisha. Hivyohivyo, mtazamo na itikadi zilizojengeka kwa mujibu wa mtazamo wa kidini na imani ya Mwenyezi Mungu huwa na mtindo wake makhsusi wa maisha. Hivyo basi tafsiri na ufahamu wa kila mtu kuhusu maana ya maisha huainisha malengo yake maishani.
Kwa msingi huo kabla ya kuingia katika maudhui ya mtindo wa maisha wa kidini na Kiislamu na wajibu wa mtu binafsi na jamii katika uwanja huo, tunalazimika kwanza kuzungumzia mtazamo wa Uislamu kuhusu maisha, dunia na mwanadamu ili kwa njia hiyo tuweze kutambua maana na malengo ya maisha na vilevile nafasi aali na ya juu ya mwanadamu katika itikadi ya tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu.
Katika kipindi kilichopita tulizungumzia kwa kiasi maudhui hii na kusisitiza juu ya umuhimu mkubwa wa imani ya Mwenyezi Mungu katika maisha ya Kiislamu na uhusiano mkubwa uliopo baina ya dunia na Akhera. Tulisema kuwa katika aidiolojia na itikadi zake, dini ya Uislamu inamfunza mwanadamu kwamba, kwa upande mmoja ujudi na uwepo wake unafungamana kikamilifu na Mwenyezi Mungu, na kwa upande mwingine maisha yake hayaishii katika maisha ya dunia. Tulisema kuwa mtazamo huo unaarifisha uhusiano wa mwanadamu na mwanzo, yaani Mwenyezi Mungu, na mwisho wake yaani Siku ya Kiyama. Hivyo, mwanadamu anawajibika kulinda uhusiano wa dunia na maisha ya milele ya Akhera. Tulisisitiza kuwa katika mtazamo wa Uislamu maisha ya dunia ni utangulizi na daraja la kufika kwenye saada na ufanisi wa milele huko Akhera na kwamba mwanadamu anapaswa kuyatumia vizuri maisha yake ya dunia.
Mtazamo wa mwanadamu kuhusu ujudi na ulimwengu ni miongoni mwa mitazamo muhimu sana na yenye taathira kubwa katika mtindo wa maisha wa kiumbe huyo. Kila mtu anaitazama dunia kwa njia yake na kupanga malengo na njia yake ya maisha kwa mujibu wa mtazamo huo.
Mtazamo wa Kiislamu kuhusu ujudi na dunia pia haukwenda kinyume na kaida hiyo. Kwani kadiri mtazamo wa watu na jamii kuhusu ujudi na uwepo wa dunia na vilivyomo unavyooana na kuwiana na mafundisho ya Kiislamu, na mafundisho hayo yakatawala sheria na kanuni za watu na jamii husika, basi hapana shaka kuwa mtindo wa maisha wa watu au jamii hiyo utakaribia sana mtindo wa maisha wa Kiislamu. Kuwa na imani ya ghaibu, kumwamini Mwenyezi Mungu Mmoja, hakika ya Utume na Siku ya Kiyama, nafasi aali ya mwanadamu katika dunia hii, dunia kuwekwa chini ya udhibiti wake na wadhifa wake wa kuwa mja wa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kufikia daraja za juu zaidi ni miongoni mwa mambo ambayo yana taathira kubwa katika mtindo wa maisha wa Kiislamu.
Hapa mpenzi msikilizaji, ndipo tunaposhuhudia waziwazi tofauti iliyopo baina ya fikra za kidini na fikra za kisekulari katika mtindo wa maisha. Kwani moja kati ya vielelezo na nguzo kuu za mtindo wa maisha wa kisekulari ni kuiweka dini kando, kuiona kama suala la mtu binafsi na kuishushia hadhi kwa kuiona kama silika au matashi ya mtu bila ya kuitambua kama kigezo muhimu cha thamani katika vipengee vyote vya maisha ya mwanadamu. Mwenyezi Mungu na itikadi za kidini hazina nafasi yoyote katika fikra za kisekulari na nafasi ya masuala hayo yamechukuliwa na mwanadamu na fikra za Humanism. Neno hili la humanism lina maana ya kumtambua mwanadamu na matakwa yake kuwa ndiye asili na kipimo cha kila kitu badala ya mafundisho ya dini.
Mitazamo finyu na ya kupindukia mipaka ya viongozi wa kanisa katika karne zilizopita iliwafanya watu wa Magharibi wajielekeze katika fikra za humanism kwa ajili ya kujikomboa na kujiondoa katika mafundisho magumu ya kanisa. Baadhi ya wanafikra wa Kimagharibi walipinga kikamilifu mafundisho ya dini na kumtenganisha mwanadamu na itikadi za Kikristo huku akili na tajiriba ya mwanadamu vikichukua nafasi ya dini. Hii ni pamoja na kuwa akili ya mwanadamu pia inashindwa kutoa majibu ya maswali mengi kuhusu kiumbe huyo. Wanafikra hao walimpandisha juu mwanadamu na kumuondoa kabisa katika hali ya kuwa mja wa Mwenyezi Mungu. Kwa mujibu wa fikra za humanism, mwanadamu ndiye msingi na nguzo ya kila kitu. Wanamuona mwanadamu kuwa ni kiumbe anayejikimu kikamilifu na asiyewajibika mbele ya yeyote. Mwanadamu huyu katika mtazamo wa kisekulari anaruhusiwa kufanya kila kitu na kutumia nyenzo zote kwa ajili ya kudhamini maslahi yake ya   kibinafsi.
Fikra za kihumanism zinakana kikamilifu fikra zote za metafizikia kama wahyi na ufunuo wa Mwenyezi Mungu na dini za mbinguni, na zinamtambua mwanadamu kuwa ni mtawala mutlaki wa maumbile yote. Msingi mkuu zaidi katika fikra za humanism ni kuwa, akili ya mwanadamu inachukua nafasi ya Mwenyezi Mungu na dini, na masuala ya kiroho pamoja na dini yanaondolewa kabisa katika maisha ya mwanadamu au kupewa nafasi ya chini na finyu sana. Lengo la mwisho la mwanadamu katika mtazamo wa fikra za humanism linafasiriwa kwa mujibu wa maisha ya kimaada ya dunia hii. Lengo la maisha kwa mtazamo huo ni kupata ladha zaidi, maslahi ya kibinafsi na kutumia neema za maumbile kadiri inavyowezekana na bila ya kujali lolote. Mtindo wa maisha wa Magharibi mpenzi msikilizaj umeumbika kwa mujibu wa fikra na mtazamo huu.
Inasikitisha kuwa katika kipindi chote cha zaidi ya karne mbili zilizopita wakoloni wa Magharibi walidhibiti nchi za Kiislamu na za ulimwengu wa tatu na kueneza kwa kiasi kikubwa mtindo wa maisha wa Kimagharibi katika nchi hizo. Suala hilo limesababisha matatizo mengi ya kijamii.
Mwanafikra wa Kiirani Rahim Pour Azghadi anasema: Matunda makubwa zaidi ya demokrasia ya kiliberali ya nchi za Magharibi katika nchi za Kiislamu ni fikra za kisekulari kwa maana ya kuiondoa dini katika maisha ya kijamii ya Waislamu. Hali hiyo iliyotokea katika nchi za Magharibi yapata miaka 200 iliyopita na taathira zake zikazikumba nchi za ulimwengu wa Kiislamu zilijengeka juu ya msingi wa fikra za kiliberali. Anaendelea kusema kuwa, Wamagharibi walielewa mapema kwamba, ili kuweza kulinda mamlaka na ushawishi wao katika nchi hizo wanapaswa kueneza mtindo wao wa kimaisha katika makoloni yao na katika njia hiyo wanatumia nyenzo zote hususan wenzo wa sanaa".
Rahiim Pour Azghadi anaendelea kuashiria mbinu zinazotumiwa na Wamagharibi kwa ajili ya kueneza mtindo wa maisha wa kisekulari katika nchi mbalimbali akisema: Wanatumia sana vyombo vya habari, filamu, michezo ya kuigiza, mahusiano ya mume na mke, mtindo wa mahusiano ya kijamii na kifamilia na kadhalika na kwa utaratibu huo wanatuainishia sisi mtindo wa maisha yetu. Anasema inasikitisha kuwa katika kipindi cha miaka 150 iliyopita Waislamu wamedhoofika sana ikilinganishwa na kipindi cha kustawi ustaarabu wa Kiislamu na kwamba ulimwengu mzima wa Kiislamu umetekwa na kudhibitiwa kwa namna moja au nyingine na Wamagharibi na majeshi yao.
XXXX

Wapenzi wasikilizaji muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki umemalizika. Tukutane tena wiki ijayo kukamilisha maudhu hii ya leo. Kwaherini.

Uislamu na Mtindo wa Maisha (5

Uislamu na Mtindo wa Maisha (5)
Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi cha Uislamu na Mtindo wa Maisha. Kipindi chetu cha wiki hii kitakamilisha sehemu iliyopita na kutazama itikadi zenye taathira katika mtindo wa maisha katika aidiolojia ya Kiislamu. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuwa kando ya redio zenu kusikiliza niliyokuandalieni.
XXXX
Miongoni mwa sababu za kuenea mtindo wa maisha wa Kimagharibi katika jamii ya Kiislamu ni maendeleo ya kisayansi na kiviwanda huko Ulaya na Marekani. Magharibi inawaonesha walimwengu maisha ya kisasa na imeweza kuteka macho na roho za watu wengi katika jamii mbalimbali kutokana na maendeleo makubwa ya kiuchumi na kielimu. Mafanikio haya yanawafanya watu wengi waamini kuwa mtindo wa maisha wa Wamagharibi ndio bora na unaofaa zaidi kuliko mtindo wao wenyewe wa maisha. Katika fikra za Kisekulari lengo la mwanadamu ni kupata ladha na anasa zaidi maishani. Shabaha kubwa na ya mwisho ya mwanadamu mwenye fikra za kisekulari ni maisha yake ya kiuchumi. Kwa msingi huo malengo ya kiuchumi ndio yanayoelekeza na kuongoza maisha yake. Katika mtazamo wa Kimagharibi mwanadamu hufuatilia maslahi na faida binafsi na kama hakufanya hivyo basi kwa hakika atakuwa hajafuatilia lengo lake kuu, na katika njia hiyo anapaswa kuangamiza na kuondoa kizuzuizi chochote kinachosimama kati yake na lengo lake kuu. Kama wanavyosema wao wenyewe, mwanadamu ana akili, na akili hiyo inaweza kumfikisha kwenye ladha na anasa zake kwa njia bora zaidi.
Ni kweli kwamba Wamagharibi wamefanikiwa katika masuala mengi katika kutumia akili na tajiriba lakini wakati huo huo hatupaswi kusahau kwamba wanakabiliwa na matatizo chungu nzima katika masuala mengine mengi kutokana na kuweka kando ufunuo na mafundisho ya mbinguni.
Mtindo wa maisha wa Kiislamu, tofauti na ule wa Kimagharibi, unapinga hatua yoyote ya kuweka kando na kutupitilia mbali wahyi na mafundisho ya dini, sawa kabisa na unavyopinga hatua yoyote ya kupuuza akili na tajiriba ya mwanadamu. Akili na tajiriba pamoja na wahyi na mafundisho ya dini ndivyo vinavyoweza kumfikisha salama mwanadamu katika pwani ya saada na ufanisi.
Maisha ya Kimagharibi yamejitenga na kuwa mbali na masuala ya kimaanawi na kiroho na matunda ya maisha kama hayo yaliyojitenga na Mwenyezi Mungu na masuala ya kiroho ni kuporomoka utu, upendo na ubinadamu katika maisha ya mtu binafsi na ya kijamii. Yaani badala ya Mungu, dini na masuala ya kiroho kutoa mwongozo wa nini la kufanya katika taasisi za kijamii na kuwa msingi na lengo lake katika uchumi, bunge, siasa, vyombo vya habari, familia, vyuo vikuu na kadhalika, masuala hayo ya kiroho yamekuwa na nafasi finyu na ndogo sana. Kwa maneno mengine ni kuwa, dini kwa Wamagharibi si jambo linayoyapa maana maisha ya mwanadamu. Hivyo kujitenga na Mwenyezi Mungu na mafundisho ya dini kumekuwa sababu ya matatizo mengi huko Magharibi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran Ayatullah Ali Khamenei anasema kuhusu suala hilo kwamba: "Kumpenda Mwenyezi Mungu kunayapa maana maisha ya mwanadamu na kujaza pengo la kiroho la maisha ya kiumbe huyo. Mwenyezi  Mungu na dini humpa mwanadamu mafanikio katika medani na nyanja zote za maisha na hapana shaka kuwa, sababu ya kuona mambo kama fedha, nguvu za kijeshi na maendeleo ya kisayansi yameshindwa kumdhaminia mwandamu ufanisi na utulivu wa kiroho na kinafsi katika nchi kama Marekani ni huko kujitenga na kujiweka mbali na Mwenyezi Mungu na masuala ya kiroho." Mwisho wa kunukuu.
Aidiolojia ya Kiislamu ambayo ndiyo msingi wa mtindo wa maisha wa Uislamu imejengeka juu ya nguzo kadhaa ikiwemo itikadi ya tauhidi na Mungu Mmoja, imani ya Siku ya Mwisho na malipo na imani ya Mitume wa Mwenyezi Mungu waliotumwa kuwaongoza wanadamu na kuwaelekeza katika saada na ufanisi wote katika dunia na huko Akhera. Nguzo hizi kwa hakika zinatoa majibu ya maswali ya kimsingi na muhimu yanayoulizwa na kila mwanadamu mwerevu. Wanadamu wa aina hii daima hujiuliza kwamba: Ni nini chanzo na muumba wa ulimwengu na vilivyomo? Na je mwisho wa maisha haya ya dunia utakuwaje, je mwanadamu anawezaje kuelewa njia bora zaidi na taratibu nzuri za maisha?
Wasifu unaotolewa na aidiolojia ya dini ya Uislamu kuhusu maisha ya dunia ndiyo kamili zaidi na imesimama juu ya misingi kadhaa. Hapa tutataja misingi muhimu zaidi kati yao ambayo ni imani ya ghaibu. 
XXXX
Kuamini ghaibu kunajumuisha mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kumwamini Mwenyezi Mungu, kuwa na imani ya kuwepo Malaika wake, majini, shetani, roho, barzakhi, Siku ya Kiyama, pepo na moto. Sehemu moja ya ulimwengu ni dunia hii inayotuzunguka ambayo ni dunia ya kimaada na inayoonekana kama ardhi, mbingu, nyota, bahari na kadhalika. Hata hivyo sehemu nyingine na kubwa zaidi ya ulimwengu ni ule wa ghaibu na usioonekana ambao hauwezi kulinganishwa na ule wa maada kwa ukubwa na una taathira kubwa zaidi. Japokuwa sisi wanadamu wa kawaida yumkini tukashindwa kuuelewa na kuudiriki vyema ulimwengu huo mkubwa zaidi wa ghaibu kutokana na mahusiano yetu ya kila siku na ulimwengu wa maada, lakini hapana shaka kuwa ulimwengu huo upo, na matatizo mengi ya mtindo wa maisha wa wanadamu yanatokana na kutotaamali na kuamini mambo ya ulimwengu huo wa ghaibu na usiohisika kwa hisi za kimaada. Vilevile iwapo mtu yeyote atashindwa kutatua suala hili la imani ya ulimwengu wa ghaibu, basi hawezi kuwa na itikadi halisi kuhusu Uislamu wala kutekeleza mafundisho ya dini hiyo. Kwani mambo kama Mwenyezi Mungu, Siku ya Kiyama, pepo na moto wa Jahannam, Malaika, shetani, roho na kadhalika ni vitu ambavyo havina eneo au zama makhsusi na havibanwi na zama wala eneo. Kwa maneno mengine ni kuwa ni vitu visivyohisika kwa hisi za kimaada. Vyote hivyo pia ni vielelezo vya ulimwengu wa ghaibu.
Katika maisha yake ya duniani, mwanadamu anaweza tu kuelewa baadhi ya vielelezo vya ulimwengu wa ghaibu na vielelezo vingine vitadhihirika kwake katika ulimwengu wa barzakhi na ulimwengu wa Akhera.
Mwenyezi Mungu (sw) pia ni ghaibu na haonekani kwa macho lakini wanadamu wanapaswa kumwamini na kujua kwamba yupo kupitia ishara na aya zake. Aya na ishara hizo ziko nyingi sana na Qur'ani Tukufu imetaja baadhi yake. Kwani kiumbe kidogo zaidi kuliko vyote hadi kikubwa kuliko vyote ni aya na alama za kuwepo Mwenyezi Mungu Muumba.
Katika aidiolojia na itikadi za Kiislamu imani ya tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu inapaswa kuwa msingi na nguzo na kutawala pande zote za maisha ya muumini. Ni kwa sababu hii ndiyo maana katika itikadi ya Uislamu si kila maisha yanatambuliwa kuwa ni kuwa hai, kwa sababu kama Mwenyezi Mungu si msingi na nguzo ya kila kitu basi maisha hayo huwa ni maasi na udhalili bali ni sawa na kutokuwa hai. Imam Swadiq (as) anasema: Kufa katika njia ya Mwenyezi Mungu ni kutamu zaidi kuliko kuishi katika maasia, umaskini katika kumtii Mwenyezi Mungu ni bora zaidi kuliko utajiri wakati unamuasi Mola na mashaka na balaa katika njia ya kumtii Allah ni kheri kwangu mimi kuliko uzima na afya katika maasia. Vilevile Imam Hussein (as) amesema: Kufa kwa izza na heshima ni bora zaidi kuliko kuishi kwa madhila.
XXXX
Kuufanya mtindo wa maisha kuwa wa kitauhidi kuna maana kwamba mtindo huo utayarishe uwanja wa kuwa mjaa wa kweli wa Mwenyezi Mungu. Kwa utaratibu huo ada na desturi za Kiislamu zinamtayarisha mtu kuwa mja wa Mwenyezi Mungu katika kila kitu maishani mwake. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei anasema: Itikadi ya tauhidi si nadharia ya kifalsafa na kifikra tuu bali ni mbinu ya maisha kwa ajili ya wanadamu. Maana ya imani ya tauhidi ni kumfanya Mwenyezi Mungu mtawala wa kila kitu katika maisha yako na kutupilia mbali nguvu nyingine yoyote. Anaendelea kusema kuwa: Kalima ya "Laa ilaha illallah" ambayo ndio ujumbe mkuu wa Mtume wetu na Mitume wote wa Mwenyezi Mungu, ina maana kwamba katika maisha na katika njia na katika kuchagua mtindo wa maisha mwanadamu anapaswa kutupilia mbali kabisa nguvu zote za kitwaghuti na kujiepusha na kila kitu kisichofungamana na Mola Muumba. Kama tauhidi itatawala maisha ya jamii basi bila shaka dunia ya mwanadamu pia itapata ustawi na itahudumia malengo aali na ya ukamilifu wa mwanadamu. Ayatullah Khamenei anamalizia kwa kusema: "Iwapo tutakuwa na itikadi ya tauhidi lakini hatukutekeleza tauhidi katika matendo yetu na hatukuwa waja wa kweli wa Mola, basi amali zetu hazitakuwa za kitauhidi au za mtu anayeamini ghaibu, na wakati huo kutakuwepo pengo kubwa baina ya itikadi na amali na matendo yetu."   
XXXX
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu cha leo unaelekea ukingoni. Msikose kuwa nasi tena juma lijalo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki.
Kwaherini.


Uislamu na Mtindo wa Maisha (6)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (6)
Hii ni sehemu ya sita ya kipindi cha Uislamu na Mtindo wa Maisha. Katika sehemu ya wiki iliyopita tuliendelea kuzungumzia misingi muhimu ya aidiolojia ya Kiislamu ambayo ina taathira kubwa katika mtindo wa maisha wa mwanadamu.
Katika fikra za Kisekulari lengo la mwanadamu ni kupata ladha na anasa zaidi maishani. Shabaha kubwa na ya mwisho ya mwanadamu mwenye fikra za kisekulari ni maisha yake ya kiuchumi. Kwa msingi huo malengo ya kiuchumi ndio yanayoelekeza na kuongoza maisha yake. Wanasema mwanadamu ana akili, na akili hiyo inaweza kumfikisha kwenye ladha na anasa zake kwa njia bora zaidi. Hata hivyo tulisema Wamagharibi wamefanikiwa katika masuala mengi katika kutumia akili na tajiriba lakini wakati huo huo hatupaswi kusahau kwamba wanakabiliwa na matatizo chungu nzima katika masuala mengine mengi kutokana na kuweka kando ufuo na mafundisho ya mbinguni.
Katika kipindi cha wiki iliyopita pia tulisema mtindo wa maisha wa Kiislamu, tofauti na ule wa Kimagharibi, unapinga hatua yoyote ya kuweka kando na kutupitilia mbali wahyi na mafundisho ya dini, sawa kabisa na unavyopinga hatua yoyote ya kupuuza akili na tajiriba ya mwanadamu. Matunda ya maisha kama hayo yaliyojitenga na Mwenyezi Mungu na masuala ya kiroho ya mtindo wa maisha wa Kimagharibi ni kuporomoka utu, upendo na ubinadamu katika maisha ya mtu binafsi na ya kijamii. Yaani badala ya Mungu, dini na masuala ya kiroho kutoa mwongozo wa nini la kufanya katika taasisi za kijamii, imepewa nafasi finyu na ndogo sana. Tulizungumzia imani ya ulimwengu wa ghaibu na kugusia kwa ufupi jinsi imani ya tauhidi na Mungu Mmoja, Mitume Wake na Siku ya Kiyama, inavyopaswa kuwa msingi wa harakati zote za mwanadamu Mwislamu na taathira zake katika mtindo wa maisha wa wafuasi wa dini hiyo. Nguzo hizi kwa hakika zinatoa majibu ya maswali ya kimsingi na muhimu yanayoulizwa na kila mwanadamu mwerevu. Wanadamu wa aina hii daima hujiuliza kwamba: Ni nini chanzo na muumba wa ulimwengu na vilivyomo? Na je mwisho wa maisha haya ya dunia utakuwaje, je mwanadamu anawezaje kuelewa njia bora zaidi na taratibu nzuri za maisha?
Tulisema kuwa wasifu unaotolewa na aidiolojia ya dini ya Uislamu kuhusu maisha ya dunia ndiyo kamili zaidi na imesimama juu ya misingi kadhaa. Sehemu ya makala yetu ya leo itaendelea kuangalia misingi muhimu katika aidiolojia ya Kiislamu yenye taathira katika mtindo wa maisha wa wafuai wa dini hiyo. Karibuni.  XXXX
Miongoni mwa misingi muhimu ya aidiolojia ya Kiislamu yenye taathira katika mtindo wa maisha ni mfungamano uliopo baina ya dunia na Akhera, suala ambalo tuliligusia katika vipindi vilivyopita. Katika mtazamo wa itikadi za Kiislamu maisha ya dunia ni mithili ya shamba ambalo mwanadamu anapaswa kulilima na kupanda humo mbegu na mimea kadiri anavyoweza ili aweze kuvuna na kuchuma matunda yake kesho katika ulimwengu wa Akhera. Imam Ali bin Abi Twalib (as) anasema: Enyi waja wa Mwenyezi Mungu! Fanyeni jitihada za kukusanya masurufu katika siku hizi chache za dunia kwa ajili ya kipindi cha Akhera ambacho ni kirefu sana. Dunia ni nyumba ya amali na kazi na Akhera ni nyumba na kubakia na malipo. (al Kafi 8-174)
Vilevile anasema katika hotuba ya 133 ya Nahjul Balagha kwamba: "Dunia ni mwisho wa macho ya kipofu, kwani hawezi kuona chochote kati ya vilivyo nyuma yake. Mwenye macho yanayoona huvuka upeo wa dunia na kuelewa kwamba, nyumba halisi iko nyuma ya dunia. Mwenye macho huangalia yaliyonyuma ya dunia, na kipovu huangalia dunia yenyewe. .." mwisho wa hadithi.
Katika hadithi hizi Imam Ali bin Abi Twalib (as) anaashiria tofauti za mitazamo za mitindo miwili ya maisha inayotokana na aina mbili tofauti ya mitazamo. Mtazamo wa kwanza ni wa mtu anayeiona dunia kuwa ndio lengo lake kuu na hufanya jitihada zake zote kwa ajili ya siku kadhaa za dunia hii ya kupita. Mtazamo wa pili ni ule unaoitambua Akhera kuwa ndiyo nyumba ya asili ya mwanadamu na huyafanya maisha ya duniani kuwa daraja la kuvukia kwa ajili ya kuelekea Akhera. Hapa mpenzi msikilizaji, ndipo tunapoelewa ni kwa kiwango gani itikadi na aidiolojia zinavyokuwa na taathira kubwa katika mtindo wa maisha wa mwanadamu.
Katika itikadi na aidiolojia ya Kiislamu kutumia neema za kimaada kadiri ya haja si tu kwamba hakuna tatizo lolote, bali kunatambuliwa kuwa ni jambo la dharura kwa ajili ya kudumisha uhai wa kimaada. Hata hivyo dini hiyo imekemea na kukataza kuzama katika neema za kimaada na kuchupa mipaka katika kuipenda dunia. Mtume Muhammad (saw) anasema: "Waachieni dunia watu wake kwani anayechukua katika dunia zaidi ya haja yake huchukua pia kifo chake bila ya kujua." Hapa tunapenda kutoa maelezo kwamba, kwa mujibu wa itikadi ya Kiislamu, mwanadamu katika maisha ya dunia ni mithili ya msafiri ambaye anaelekea katika maisha ya Akhera. Maisha ya dunia kwake ni sawa na nyumba ya wageni na hapana shaka kuwa, raha ya mtu anayekuwa safarini ni kutokuwa na mzigo mkubwa unaomlemea njiani na kumchelewesha na huenda kumkwamisha kabisa.
Vilevile imepokewa kutoka kwa wasii na khalifa wa Mtume (saw) Imam Ali bin Abi Twalib kwamba kasema: Nakutahadharisheni na dunia, kwani ni laghai mkubwa, na pale inapotimiza matarajio ya watu wake, basi huwa kama alivyosema Mwenyezi Mungu SW kwamba: Wapigie mfano wa maisha ya dunia (kuwa) ni kama maji tuliyoteremsha kutoka mbinguni yakachanganyika na mimea ya ardhi (ikastawi na baadaye) ikawa majani makavu yaliyokatika-katika, yanayopeperushwa na upepo. Na Mwenyezi Mungu ana uwezo juu ya kila kitu.  (Suratul Kahaf: 45) (Nahju Saada: 3-284) Hapa inatulazimu kutaja nukta hii kwamba, mtindo wa maisha wa Kiislamu haumzuii mtu kuwa na maisha bora, bali Uislamu inawataka wafuasi wake kuwa na maisha bora na salama zaidi na kuwatahadharisha na raha za kupindukia zinazomsahaulisha mtu lengo lake asili na maisha yake ya milele.    
Nukta nyingine muhimu katika mtindo wa maisha wa Kiislamu ni kuwa na matumaini katika maisha. Maisha na uhai ni neema tuliyopewa na Mwenyezi Mungu. Hivyo basi tunapaswa kuithamini na kuwa na matumaini na mustakbali mwema. Vilevile kwa kutilia maanani mtazamo wa Uislamu kuhusu dunia, matatizo ya kimaada na kidunia hayapaswi kumfanya Mwislamu awe mtu aliyekata tamaa na kukosa matumaini. Katika mtindo wa maisha wa Kiislamu muumini anakatazwa kukata matumaini na kuzidiwa nguvu na matatizo ya kimaada. Muumini daima anapaswa kukumbuka ujira na thawabu za kustahamili mashaka na kuwa na matumaini na rehma za Mola Karima

0 toamaon yako:

    Author

    CONTACT ME FOR WEB AND BLOG DESIGNING...

    uislam na maisha yake

    uzayuni

    swahili radio

    uislam na maisha

    mohamed waziri

    Subscribe to our Mailing List

    We'll never share your Email address.
    +255 (762) 118-805 mohamedwaziri295@gmail.com